Kisima kilichopo eneo la Matamwe Mkoa wa Kaskazini Unguja ambamo raia wawili wa Ufaransa wanasadikiwa kuuawa na kisha kufukiwa kwa zege. Picha na Mwinyi Sadallah
Zanzibar. Kazi ya kutafuta mabaki ya miili ya raia wawili wa Ufaransa waliouwawa kwa kukatwakatwa kwa mapanga na kutupwa katika kisima huko Matemwe katika Mkoa wa Kaskazini, imekamilika, imefahamika.
Akizungumza na Mwananchi jana, Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Pembe Juma Khamis, alisema kazi ya kufukuwa kisima hicho ilikamilika saa 9:00 alasiri ya juzi.Alisema kazi hiyo ilifanywa kwa ushirikiano wa Kikosi cha Zimamoto na Uokozi ,Polisi na wananchi wa shehiya hiyo.
Khamis alisema kwa sababu ya mazingira magumu katika kuvunja zege, ili kufika kina kikubwa cha kisima hicho, wataalamu wa uokoaji waliamua kutumia trekta la kuchimbia vifusi kuchimba na kufanikiwa kupata mabaki ya mifupa. Kwa mujibu wa mkuu huyo wa mkoa, mabaki hayo ni pamoja na fuvu moja na hivyo kufanya idadi ya mafuvu yaliyopatikana kuwa mawili. Alitaja mabaki mengi kuwa ni mifupa ya miguu na mbavu.
ENDELEA KUSOMA HABARI HII KWA KUBOFYA HAPA CHINI
“Kazi ya kutafuta mabaki ya miili imekamilika baada ya waokoaji kutumia kijiko cha kuchimbia vifusi. Tunashukuru kazi hiyo imemalizika salama na na kinachofuatia sasa ni uchunguzi wa kijinai unaofanywa na polisi”, alisema mkuu huyo wa mkoa.
Kuhusu kiini cha mauaji hayo, alisema anayepaswa kuzungumzia ni Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Zanzibar, Yussuf Ilembo.
Alipoulizwa kuhusu maendeleo ya uchungzi wa tukio hilo mkurugenzi huyo alisema msemaji ni Kamishana wa Polisi Zanzibar, Hamdani Khamis Omar.
Kwa upande wake, Kamishna Hamdani alisema hakuwa katika mazingira mazuri ya kutoa taarifa kuhusu kukamilika kwa kazi hiyo.
Raia wawili wa Ufaransa Francios Chererobert Daniel ambaye aliwahi kuwa mtumishi wa ngazi ya juu katika Serikali ya Ufaransa na mkewe Brigette Mary waliuawa na kufukiwa kisimani kwa kutumia zege.
Tayari watu watatu wanashikiliwa na polisi kwa kwa tuhuma za kuhusika na mauaji hayo.
Tukio hilo limekuja miezi kadhaa baada ya raia wawili ya Uingereza kumwagiwa tindikali mjini Unguja mwaka jana.
MWANANCHI