Dar es Salaam. Utata umeibuka kuhusu alipo mfanyabiashara maarufu nchini, Alex Masawe baada ya kuwepo kwa tetesi kuwa ameachiwa huru huko Dubai, Falme za Kiarabu (UAE) alikokuwa akishikiliwa.
Masawe ambaye alikamatwa katika uwanja wa ndege huko UAE akitokea Afrika Kusini, kati ya Juni 20 na 25, mwaka jana, anatuhumiwa kwa makosa mbalimbali yakiwamo ya mauaji.
Mkuu wa Shirika la Polisi la Kimataifa (Interpol) - Tanzania, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Gustav Babile alikiri kuwapo kwa taarifa kwamba Masawe ameachiwa huru na hayupo Dubai ingawa bado tawi la Interpol katika nchi hiyo halijatoa taarifa yoyote.
“Tumejaribu kuwasiliana nao mara kwa mara kuhusu kumrudisha nchini lakini hawajajibu lolote. Hivi karibuni tuliwasiliana nao lakini hawajatujibu, kwa hiyo tumebaki na maswali. Kwa kifupi hatujui alipo hadi sasa,” alisema Kamishna Babile.
Alisema awali, baada ya kukamatwa huko Dubai, Tawi la Interpol Tanzania lilikuwa linafanya mchakato wa kumrudisha nchini ikiwamo kutuma ombi la kumrejesha mhalifu nchini, lakini ghafla mawasiliano yakakatika.
“Taarifa zilizopo ni kuwa Masawe ameachiwa huru, kwa vigezo gani hatuelewei,” alisema Babile.
ENDELEA KUSOMA HABARI HII KWA KUBOFYA HAPA CHINI
Babile alisema iwapo atakuwa ameachiwa na polisi wa UAE, basi itakuwa ameachiwa kutokana na sheria za nchi hiyo ingawa bado Tanzania itaendelea kumsaka kwa udi na uvumba.
“Sisi tutaendelea kumsaka kama kawaida, iwapo atakamatwa nchi nyingine au ikitokea akaonekana hapa nchini, tutaendelea na mchakato wa kumfungulia kesi kwa sababu sisi tunajua kuwa ana makosa,” alisema Babile.
Massawe alitajwa mahakamani Aprili 4, mwaka jana katika kesi ya mauaji ya mfanyabiashara, Onesphory Kituly ambaye aliuawa katika mazingira ya kutatanisha Novemba 6, 2011 nyumbani kwake Magomeni, Dar es Salaam.
Katika kesi hiyo, mshtakiwa wa kwanza ni mfanyabiashara Abubakar Marijani, maarufu kama ‘Papaa Msofe’ na mshtakiwa mwingine ni Makongoro Joseph Nyerere.
Nyerere aliwahi kulalamika mbele ya Hakimu Mkazi, Agnes Mchome anayesikiliza kesi hiyo, akidai kwamba kumekuwa na ucheleweshaji wa shauri hilo kutokana na ndugu wa marehemu Kituly kutaka Massawe akamatwe ili ajumuishwe.
Mtuhumiwa huyo aliomba jalada la kesi yao lipelekwe mahakamani hapo kwa ajili ya kulifanyia kazi. Alitoa malalamiko hayo baada ya Wakili wa Serikali, Mwanaisha Kombo kudai upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kuomba tarehe mpya ya kutajwa kwake.
MWANANCHI