Kamishna wa uhamiaji mkoa wa Kilimanjaro Johanes Msumule akizungumza na wanahabari ofisini kwake baada ya kukamatwa kwa wahamiaji haramu 11 wilayani Rombo
Wahamiaji haramu waliokamatwa wilayani Rombo katika moja ya nyumba ya wageni.
Bi. Leokadia Tarimo raia wa Tanzania na Bw. Paulo Endevayesu raia wa Burundi ambao wanatuhumiwa kujihusisha na biashara ya kusafirisha wahamiaji haramu hao
Afisa wa uhamiaji wilaya ya Rombo akiwasindikiza watu wawili ambao wanatuhumiwa kuwa ndio wahusika wa usafirishaji wa wahamiaji haramu hao.
Askari wakiwa katika gari lililopeba wahamiaji haramu hao waliokamatwa wilayani Rombo katika moja ya nyumba ya wageni.
Na Dixon Busagaga wa Globu ya Jamii, Moshi.
WIMBI la wahamiaji haramu kuingia nchini limeendelea kushika kasi katika siku za karibuni kufuatia kukamatwa kwa wahamiaji haramu wengine 11 raia wa Ethiopia katika kijiji cha Mlele kata ya Mashati wilayani Rombo wakiwa wamehifadhiwa katika nyumba ya kulala wageni.
Tukio la kukamatwa kwa wahamiaji hao linakuja ikiwa ni wiki moja imepita baada ya kukamatwa kwa kundi jingine kubwa la wahamiaji haramu wapatao 56 katika kijiji cha Jiungeni wilayani Same wakiwa katika harakati za kufanya safari kuelekea nchini Afrika Kusini kwa lengo la kutafuta kazi. Kamanda wa polisi mkoa wa Kilimanjaro Robert Boaz amesema kuwa wahamiaji hao walikamatwa juzi majira ya saa 7 mchana baada ya askari polisi waliokuwa doria kupata taarifa ya kuwepo kwa wahamiaji hao haramu katika moja ya nyumba za wageni.
“Jana(Juzi) saa 7 mchana askari wakiwa doria walipata taarifa kuwa kuna wahamiaji haramu na kwamba kwamba wamefichwa kwenye nyumba moja katika kijiji cha mlele kata ya Mashati na askari baada ya kufika katika nyumba hiyo waliwakuta”alisema Kamanda Boaz.
Alisema baada ya kukamatwa kwa wahamiaji hao polisi ilianza ufuatiliaji juu ya wahusika waliowaingiza nchini na kuwahifadhi ndipo wakafanikiwa kumkamata mwanamke mmoja aliyefahamika kwa jina la Leocadia Gapiti ambaye anadaiwa kuwa ndiye mmiliki wa nyumba hiyo. “Tumemkamata mwanamke mmoja anaitwa Leokadia Gapiti ambaye alikuwa amewahifadhi kwenye nyumba hiyo na mwingine Paulo Endevayesu ambaye ndiye wakala halisi ambaye alikuwa anawasafirisha watu hao.”alisema.
Kamanda Boaz alisema uchunguzi zaidi unafanyika ili kujua watu hao walikuwa wanatoka wapi wanaenda wapi na kwamba pindi utakapo kamilika watafikishwa mbele ya vyombo vya sheria. Kwa upande wake kamishna msaidizi wa uhamiaji mkoa wa Kilimanjaro Bw. Johanes Msumule alisema wamebaini kuwepo kwa mtandao mkubwa katika suala hilo na kwamba tayari wanaendelea kuwahoji watu wawili waliokamatwa ambao ni Leokadia na Paulo Endevayesu raia wa Burundi. Alisema katika kipindi cha wiki tatu kilichopita tayari wamesafirishwa zaidi ya wahamiaji haramu 74 kurudi nchini mwao Ethiopia ambapo kundi la kwanza lilikuwa la wahamiaji haramu 18 ambao walikabidhiwa kwa askari wa Kenya .
Alisema kundi la pili lilikuwa la wahamiaji haramu 56 lililokamatwa hivi karibuni lilisafirshwa hivi karibuni kupitia mpaka wa Namanga hadi katika kijiji cha Moyale kilichopo mpakani ma nchi za Kenya na Ethiopia.
Tukio la karibuni lilihusisha kukamatwa kwa wahabeshi 56 katika kijiji cha Jiungeni –Same wakiwa katika Lori aina ya Fuso, yenye namba za usajili, T188 AYU,linalotajwa kama mali ya kampuni ya ELyimo Trans ya Mjini Moshi likiwa na jina la Godbless Mbasha wa mkoani Manyara.