Ziara ya Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willbroad Slaa, imekumbwa na vurugu wilayani Kibondo baada ya vijana kuingilia mkutano wake wa hadhara wakiwa na mabango.
Vurugu hizo zilisababisha vijana 12 kutiwa mbaroni na polisi.
Mabango hayo yalikuwa yakipinga hatua iliyochukuliwa na Kamati Kuu (CC) ya Chadema kumsimamisha Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe.
Vijana hao wakike na kiume waliingia na mabango katika mkutano huo uliofanyika katika kijiji cha Mabamba jimbo la Muhambwe linaloongozwa na Felix Mkosamali wa NCCR Mageuzi muda mfupi baada ya msafara wa Dk. Slaa kuwasili kijijini hapo.
Vijana hao waliokamatwa na kupandishwa katika gari la polisi PT 1832 na kupelekwa kituo kikuu cha polisi Kibondo ni Yoli James, Fasha Alex, Mohamed Hamis, Laila Hamis, Nuru Yusuph na Mateso Mkwashu.
ENDELEA KUSOMA HABARI HII KWA KUBOFYA HAPA CHINI
Wengine ni Bahati Salum, Shakuru Mahusen, Awadhi Hassan, Muliliye na Bulikoko.
Hii ni mara ya pili kwa vijana kujitokeza na mabango katika mkutano wa Dk. Slaa ambapo juzi ilijitokeza wilaya ya Kakonko na vijana wanne waliingia na mabango yaliyokuwa na ujumbe mbalimbali.
Katika tukio la jana, mabango hayo yalikuwa yameandikwa ujumbe kama "Bila Zitto Chadema ni chama cha wachaga sio makabila mengine", "Tumekuachia chama, Acha ukabila,” "Bila Zitto Chadema hamna jipya ni sawa na nyumba bila msingi itashuka muda wowote kuanzia sasa.”
Mengine yaliandikwa: "Wewe siyo mwema hutufai", "Tunamtaka mtetezi wetu Mhe. Zitto ndiyo kiongozi bora siyo wewe", "Chadema bila Zitto haiwezekani ila Zitto bila Chadema inawezekana, Acha udini.”
Mabango mengine yalikuwa na ujumbe kama "Imedhihirisha kuwa Chadema ni chama cha wachaga siyo makabila mengine na Tumegundua migogoro ya udini imeanzia kwako wewe siyo kiongozi bora hutufai.”
Polisi waliokuwa wakilinda mkutano huo walianza kuwaondoa eneo la mkutano lakini Dk. Slaa aliwataka askari hao kuwaacha na kutaka wasogee mbele na mabango yao karibu na meza kuu.
Kutokana na vurugu hizo Dk. Slaa alilazimika kwenda mbele ya jukwaa na kuanza kueleza kuwa mkutano huo upo kwa mujibu wa sheria, aliagiza polisi wawakamate jambo ambalo lilitekelezwa haraka.
Dk. Slaa alimwagiza Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Kibondo, Clavery Ntidyicha, kufungua kesi dhidi ya vijana hao kwa kufanya vurugu katika mkutano kwa niaba ya chama na kuahidi kufuatilia mwenendo wa kesi hiyo.
Baadaye akizungumza na wananchi katika mkutano huo, Dk.Slaa alisema tabia ya CCM kupandikiza isifikiri kuwa inawajenga bali watambue kuwa inawabomoa.
Alisema ameagiza polisi vijana hao wachukuliwe hatua kwa sababu ndiyo sheria inavyoelekeza na kwamba kama yupo mtu aliwapa pombe ili wafanye vurugu atahukumiwa mbele ya Mungu.
Dk. Slaa alisema katika maeneo (majimbo) atakayotembelea mkoa wa Kigoma watakaokuja na mabango watapaswa kueleza mabango yameandikwa wapi katika katiba ya Chadema.
CHANZO: NIPASHE