Katika Bunge hilo, wajumbe wengi wa CCM walimshambulia Warioba na tume yake wakidai kuwa Rasimu ya Pili ya Katiba haikuzingatia maoni ya wananchi na Mabaraza ya Katiba.PICHA|MAKTABA
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba amewashauri wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na CCM kuacha kuzunguka mikoani kufanya mikutano inayoeleza misimamo yao kuhusu mchakato wa Katiba Mpya kwa kuwa haina tija kwa taifa.
Ameonya kuwa mikutano hiyo inajenga mwelekeo mbaya kwa taifa na kuhatarisha mchakato wa Katiba na kuzitaka pande hizo kumaliza tofauti zao.
Akizungumza katika mahojiano maalumu yaliyofanyika Dar es Salaam jana, Warioba alisema: “Kwa mustakabali mwema wa taifa, ni muhimu makundi haya ‘ya-resolve’ (yamalize), matatizo yaliyopo kabla ya Agosti, ili Bunge Maalumu la Katiba likirejea, wote washiriki na kukamilisha mchakato wa kupata Katiba Mpya. Hili ni kwa masilahi ya taifa.”
ENDELEA KUSOMA HABARI HIII KWA KUBOFYA HAPA CHINI
Kauli ya Waziri Mkuu huyo mstaafu ambaye pia aliwahi kuwa Mwanasheria Mkuu, imekuja huku makundi ya Ukawa linaloundwa na wabunge wengi wa upinzani na viongozi wa CCM wakiendelea kung’ang’ania misimamo yao kuhusu Rasimu ya Katiba Mpya iliyowasilishwa kwenye Bunge Maalumu la Katiba.Wakati CCM ikipinga mapendekezo ya kuwapo kwa mfumo wa serikali tatu uliomo kwenye Rasimu, Ukawa unaunga mkono mapendekezo hayo.
Aprili 16, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba aliiongoza Ukawa kutoka ndani ya Bunge la Katiba baada ya kumaliza kuchangia mjadala huo, kwa madai ya kutokutendewa haki na CCM katika mambo mbalimbali ikiwamo kupinga mapendekezo ya upinzani hata yale ya msingi akisema hawawezi kuwa sehemu ya watu wanaosambaza chuki na kuwa sehemu ya kuibomoa nchi.
Siku chache baadaye, Ukawa ulianza mikutano nchi nzima kwa kile ulichodai kuwaeleza wananchi namna CCM inavyotaka kuchakachua maoni yao yaliyokusanywa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.Kwa upande wake, CCM imekuwa ikifanya mikutano kueleza msimamo na sababu za kutaka kuendelea kwa muundo wa serikali mbili.
Jaji Warioba alisema makundi hayo yana nafasi ya kumaliza tofauti zao kabla ya Bunge Maalumu la Katiba kuanza tena vikao vyake, hivyo kuliwezesha taifa kupata Katiba Mpya.
Alisema makundi hayo yasipopatana yanaweza kuhatarisha mustakabali wa taifa hata amani iliyopo.Alionya kuwa amani iliyopo nchini ikivurugika kwa sababu yoyote ni vigumu kuirejesha na kwamba watakaotaabika ni wananchi.
Jaji Warioba ambaye aliwahi kuongoza Tume ya Rushwa iliyoundwa na Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, alisema amani ya Tanzania ikivurugika kutokana na makundi kupingana katika mchakato wa Katiba wanasiasa ndio watakaonyooshewa vidole.
Awali, Februari mwaka huu baada ya Jaji Warioba kuwasilisha Rasimu ya Pili ya Katiba katika Bunge Maalumu la Katiba wanaCCM wengi, kuanzia Mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete waliichambua huku wakionyesha dhahiri kutokuridhishwa na mapendekezo kadhaa kubwa ikiwa ni muundo wa Muungano.
Katika Bunge hilo, wajumbe wengi wa CCM walimshambulia Warioba na tume yake wakidai kuwa Rasimu ya Pili ya Katiba haikuzingatia maoni ya wananchi na Mabaraza ya Katiba.
Baadaye katika uzinduzi wa ripoti ya Twaweza kuhusu Mchakato wa Katiba, Jaji Warioba alijibu shutuma hizo alipouliza maswali saba ya msingi ambayo aliwataka wawajibu wananchi ili kutuliza kiu yao.
Maswali hayo yalikuwa:
1. Kwa nini mnapinga muundo wa Muungano wakati walioupendekeza ni wananchi?
2. Wapeni majibu wananchi kwa nini Tanganyika imevaa koti la Muungano?
3. Elezeni kwa nini Katiba imevunjwa, madaraka ya Rais kuchukuliwa na marais wawili katika nchi moja?
4. Tume ilitumwa na nani kukusanya maoni ya wananchi na kwa kutumia sheria ipi zaidi ya ile ya Mabadiliko ya Katiba?
5. Kwa nini wanawatuhumu uongo yeye na Joseph Butiku kuwa walikuwa wajumbe wa Tume za Kisanga na Nyalali zilizopendekeza serikali tatu?
6. Kwa nini hawataki kuzungumzia yaliyomo katika rasimu bali wanadai imeandikwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba?
7. Waeleze kwa nini wanadai Tume imeingiza maoni yake, wakati iliyakusanya kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba?
Bunge Maalumu la Katiba litarejea Agosti mwaka huu baada ya kusitisha vikao vyake kupisha Bunge la Bajeti linaloendelea mjini Dodoma.