Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimewadhibiti kwa kuwapa onyo kali viongozi na makada wake sita waliobainika kuanza kufanya kampeni za chini kwa chini kuwania urais katika uchaguzi mkuu ujao utakaofanyika mwakani.
Waliokutwa na hukumu hiyo iliyotolewa na Kamati Kuu ya CCM iliyoketi mwishoni mwa wiki iliyopita ni Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wassira.
Waliokutwa na hukumu hiyo iliyotolewa na Kamati Kuu ya CCM iliyoketi mwishoni mwa wiki iliyopita ni Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wassira.
Wengine ni Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia January Makamba na waziri wa zamani wa Nishati na Madini, William Ngeleja.
Mbali na kupewa onyo kali, makada hao pia wametakiwa kutojihusisha na kampeni au vitendo vyovyote vinavyoashiria kampeni na watakuwa chini ya uangalizi wa mwaka mmoja.
Aidha, CCM imewatangazia makada hao kuwa wakikiuka agizo hilo, watakuwa wamejiondolea sifa ya kushiriki mchakato wa kugombea nafasi yoyote ya uongozi ndani ya chama chao.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, alisema kuwa Kamati Kuu ya chama hicho imefikia hatua ya kuwaonya makada hao baada ya kuwabaini kuwa wameanza kufanya kampeni za kutaka wateuliwe na chama hicho kugombea nafasi za uongozi.
Nape alisema makada hao walihojiwa na kamati ya maadili na kwamba wote walibainika kuanza kampeni kinyume cha maadili na kanuni za chama hicho; hivyo kamati ilipendekeza kuwa wote waadhibiwe.
Nape aliongeza kuwa kazi ya kutoa adhabu ilikuwa ni ya kamati kuu ya CCM ambayo hatimaye ilikaa na kutekeleza wajibu wake wa kutoa adhabu na onyo dhidi ya wahusika.
Nape alisema makada hao walihojiwa na kamati ya maadili na kwamba wote walibainika kuanza kampeni kinyume cha maadili na kanuni za chama hicho; hivyo kamati ilipendekeza kuwa wote waadhibiwe.
Nape aliongeza kuwa kazi ya kutoa adhabu ilikuwa ni ya kamati kuu ya CCM ambayo hatimaye ilikaa na kutekeleza wajibu wake wa kutoa adhabu na onyo dhidi ya wahusika.
“Watakuwa katika hali ya kuchunguzwa kwa kipindi cha miezi 12. Kama wataendelea kujihusisha na vitendo vyovyote vya utovu wa nidhamu watakuwa wanajikosesha haki na sifa ya kugombea nafasi ya uongozi ndani ya chama katika chaguzi zijazo,” alisema Nape.
Alisema makada hao pia walionekana kushiriki kufanya vitendo vinavyokiuka nidhamu ndani ya chama na kwa jamii.
“Hakuna aliye juu au mkubwa ndani ya chama zaidi ya kanuni ambazo zimewekwa. Hawa makada waliohojiwa walibainika wote kwa pamoja kuhusika na makosa haya, hivyo ni vyema kila mwanachama akafuata kanuni na maadili ili kukijenga chama badala ya makundi yanayowagawa wanachama,” alisema Nape.
ENDELEA KUSOMA HABARI HII KWA KUBOFYA HAPA CHINI
Chama hicho kimetangaza pia kuwaita na kuwahoji wapambe na mawakala wanaoshirikiana na makada waliopewa onyo na wengine ambao hawajabainika ili kuwachukulia hatua stahili kulingana na makosa watakayokutwa nayo.
Nape alisema kuwa kamati yao ya maadili inaendelea kuwachunguza na kuwafuatilia kwa karibu na baadaye watawaita ili kuwapatia adhabu kutokana na utovu huo wa nidhamu.
“Chama kinaendeleza kuwashughulikia wale walioanzisha na kuendeleza utamaduni wa kutaka kuvuruga kanuni ili kukibomoa chama. Hatutawafumbia macho hata kidogo, hata hawa waliokuwa wakitumwa au kushirikishwa kwenye harakati hizo wataitwa na adhabu itawafuata,” alisema Nape.
MAKOSA YENYEWE
Akifafanua zaidi kuhusu baadhi ya makosa, Nape alisema kuwa ni pamoja na kukiuka kanuni zisizomruhusu kiongozi kukusanya mchango, kupeleka mchango katika jimbo analotaka kugombea au jimbo lolote na kutumia jina la chama bila kupata kibali kutoka kamati ya siasa ngazi husika.
Alisema vilevile kuwa kiongozi haruhusiwi kutoa msaada au kukusanya michango, zawadi, vifaa au kutumia mwavuli wa dini au kabila bila ridhaa ya chama.
“Ukisoma kanuni za chama utaona haya yote na pia ni namna gani makada hawa wamezikiuka kanuni hizi katika Ibara ya 6(2) i-v na kosa la kufanya kampeni kabla mgombea kutangazwa na chama,” alisema Nape.
NIPASHE iliwatafuta makada wote sita ili kupata maoni yao kuhusiana na karipio lililotolewa na CCM dhidi yao.
Sumaye alisema kuwa hana taarifa kuhusiana na suala hilo.
“Mimi sijapewa karipio lolote, nadhani ni vizuri mkaiuliza ‘centre’ yenyewe (makao makuu ya CCM) wawafafanulie vizuri juu ya karipio hilo,” alisema Sumaye.
Kwa upande wake, Wassira aliiambia NIPASHE kuwa yuko bungeni na hivyo asingeweza kueleza lolote.
“Niko bungeni bwana," alisema Wassira.
Alipotafutwa kwa njia ya simu, Lowassa hakupatikana na simu yake ilipokelewa na wasaidizi wake ambao walisema yuko kwenye vikao vya bunge.
Membe hakupatikana kwa kuwa simu yake ya mkononi ilikuwa ikiita muda wote bila kupokewa, sawa na ilivyokuwa kwa Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia January Makamba. Simu ya Ngeleja haikupatikana kabisa licha ya kupigiwa mara kadhaa.
Kuanzia Alhamisi (Februari 13) hadi jana asubuhi, CCM ilikuwa na vikao kadhaa mjini Dodoma vikiwamo vya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Kamati Kuu na Kamati ya Maadili kujadili masuala mbalimbali likiwamo la viongozi na makada wake waliokuwa wakihusishwa na kampeni za chini chini za kuwania kuteuliwa kuwa wagombea urais wa chama hicho katika katika uchaguzi mkuu wa 2015.
Imeandikwa na Mary Geofrey na Raphael Kibiriti, Dar
CHANZO: NIPASHE