Mnamo mwezi Julai, 2013, Serikali kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ilikamisheni jopo la wataalamu wa Chuo Kikuu kufanya tathmini ya mchakato mzima wa uhamaji toka mfumo wa utangazaji wa analojia kwenda mfumo wa kidijiti pamoja na uzimaji wa mitambo hiyo kwenye miji saba ambayo ni Dar e salaam, Tanga, Moshi, Mwanza, Dodoma, Arusha na Mbeya. Uzimaji wa mitambo ya analojia ilikuwa ni kwa mujibu wa sheria, ambayo iko kwenye kanuni zinazojulikana kama “Digital Broadcasting and Other Networks 2011”
Jopo hilo lilijumuisha wataalamu wafuatao:-
1. Prof. Nerey Mvungi - Mtaalamu wa Mawasiliano ya ki electronic
2. Dr.Francis Sichona - Mtaalamu wa Takwimu
3. Mr.F.M Ishengoma - Mtaalamu wa Habari na Mawasiliano
Wote hawa ni wafanayakazi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
1.1 MADHUMUNI YA TATHMINI
Madhumuni ya tahmini hii ilikuwa imejengwa kwenye maeneo Makuu manne kama ifuatavyo;
(a) Tathmini ya utendaji na utoaji huduma za utangazaji kwenye mfumo wa kidijiti ikiwa ni pamoja na usimikaji wa miundo mbinu ya kidijiti.
(b)Tathmini ya kuangalia jinsi Mamlaka ya Mawasiliano ilivyokuwa imejizatiti kuandaa na kusimamia zoezi zima la uhamaji toka mfumo wa utangazaji wa analojia kwenda kidijiti
(c) Tathmini ya jinsi watumiaji wa huduma za utangazaji walivyopokea mabadiliko hayo na changamoto zilizopo na
(d)Tathmini ya jinsi zoezi zima la uzimaji mitambo lilivyoendeshwa.
Katika uendeshaji wa tathmini hiyo wataalamu walizingatia mambo muhimu yafuatayo ikiwa ni pamoja na hoja zilizotolewa na taasisi na watu mbalimbali kutoka kwenye jamii kama ifuatavyo:-
(i) Idadi ya visimbuzi vilivyokuwepo kwenye soko kabla ya uzimaji mitambo kama vinatosheleza mahitaji,
(ii) Idadi ya watu walioweza kununua visimbuzi ilikuwa ndogo hivyo watu wengi kushindwa kununua na kukosa habari zinazopatikana kwa njia ya luninga,
(iii) Ushirikishaji wa wadau kwenye mchakato mzima wa uhamaji toka mfumo wa analojia kwenda kidijiti kabla ya uzimaji mitambo hiyo,
(iv) Kiwango cha Elimu kwa Umma (Public Awareness Campaign) kilichotolewa kabla na baada ya uzimaji mitambo,
(v) Bei za visimbuzi kama zilikuwa juu kwa watu wa hali ya kawaida na kusababisha kushindwa kuvinunua,
(vi) Ubora wa visimbuzi na upokeaji wa matangazo usioridhisha kama vile kuganda kwa picha.
1.2 NJIA ILIYOTUMIKA KUFANYA TATHMINI
Njia iliyotumika kufanya tathmini hii ni ile inayotumika kimataifa (International Best Practise) kuendesha mazoezi kama haya ijulikanayo kama “Sampling Approach” ambapo takwimu hukusanywa kwa kuzingatia uwiano wa kaya zilizopo kwenye eneo husika, jinsia, umri, elimu na kazi za kumuingizia kipato mtu anayehojiwa.
Makundi mabalimbali yanayohusika kwenye mchakato huu wa uhamaji kutoka mfumo wa analojia kwenda dijitali yalihojiwa kwa kupitia dodoso maalumu lililoandaliwa na maoni yao yalikusanywa. Makundi hayo ni kama ifuatavyo:-
(i) Watumiaji wa huduma ya matangazo kwa mfumo wa kidijiti (Consumers)
(ii) Watengenezaji na wasambazaji wa maudhui kwa njia ya Luninga (Content Service Providers)
(iii) Wasimikaji wa miundo mbinu ya kidijiti (Multiplex Operators) na
(iv) Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania.
2.0 MATOKEO YA TATHMINI
Yafuatayo ni matokeo ya zoezi zima la tathmini hiyo kama ilivyoendeshwa kwenye maeneo tajwa hapo juu.
2.1 TATHMINI YA UTENDAJI NA UTOAJI HUDUMA ZA UTANGAZAJI KWENYE MFUMO WA KIDIJITI IKIWA NI PAMOJA NA USIMIKAJI WA MIUNDO MBINU YA KIDIJTI.
Tathmini iliyoendeshwa na jopo la wataalam kuhusu utendaji na huduma kwa walaji kwa ujumla wake zimeonyesha yafuatayo;
(a) Asilimia 89% ya kaya za watumiaji (consumers) walikuwa wakitumia huduma ya matangazo kwa mfumo wa kidijiti mara baada ya uzimaji wa mitambo ya analojia kwenye miji saba ambayo tathmini ilikuwa ikifanyika
(b) Asilimia 11% ya kaya za watumiaji hawakuweza kupokea matangazo ya kidijiti kwa sababu mbalimbali kama ifuatavyo:-
- 5.5% hawakununua visimbuizi
- 0.1% ya Kaya, walisema visimbuzi vilikuwa havipatikani
- 3.2% ya Kaya, walishindwa kunua visimbuzi sababu ya bei kuwa juu
- 0.2% ya Kaya visimbuzi vyao vilikuwa vibovu
- 0.3% ya Kaya, visimbuzi havikuweza kupokea matangazo ya kidijiti kwa sababu ya mawimbi hayapatikani kwa ubora zaidi (Poor signal reception)
- 0.9% ya Kaya Luninga (TV screen) zilikuwa mbovu
- 0.7% ya Kaya hawakuwa na umeme
2.2 UTAYARI WA MAMLAKA YA MAWASILIANO KUANDAA NA KUSIMAMIA ZOEZI ZIMA LA UHAMAJI TOKA UTANGAZAJI WA MFUMO WA ANALOJIA KWENDA KIDIJITI
Jopo la wataalamu lililokuwa likiendesha tathmini hii liliweza kuthibitisha kuwepo kwa mambo yafuatayo pamoja na baadhi ya nyaraka kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA):-
- Kuwepo kwa kamati ya Kiufundi inayoundwa na wadau mbalimbali ikiwa na kazi ya kutoa ushauri wa kiufundi kwa maswala yote yanayohusu uhamaji toka utangazaji wa analojia kweda kidijiti,
- Kuwepo kwa dira madhubuti inayoonyesha mambo muhimu ya kutekelezwa kuelekea uzimaji wa mitambo ya analojia,
- Kuwepo kwa sheria na kanuni zinazosimamia zoezi la uhamaji toka analoja kwenda kidijiti,
- Kuwepo kwa nyaraka mbalimbali zinazoonyesha muhtasari wa vikao mbalimbali vilivyofanywa kati ya wadau na Mamlaka ya Mawasiliano.
Vilevile Jopo la wataalamu liliweza kuthibitisha mambo yafuatayo:-
- Muundo bora wa leseni unaozingatia utoaji huduma za matangazo ya kidijiti,
- Utaratibu mzuri wa ushindani kwa njia ya wazi uliotumika kuwapata “Multiplex Operators” (wajenga Miundombinu na Wsambazaji wa matangazo),
- Waraka unaonyesha mchakato wa namna ya kupata malipo yananayotakiwa kulipwa na watengenezaji na wasambazaji wa maudhui (Transmission fee) kwa wenye leseni ya miundo mbinu ya kidijiti (Multiplex Operators),
- Mfano wa nyaraka itakayotumika kufikia makubaliano ya utoaji huduma na mahusiano yao kibiashara (SLA) kati ya wasimikaji wa miundo mbinu ya kidijiti na watengenezaji na wasambazaji maudhui.
Kutokana na vielelezo na nyaraka ambazo jopo la wataalamu iliweza kuzipata, jopo limeridhika kabisa kuwa Mamlaka ya Mawasiliano ilikuwa imejizatiti vizuri kuandaa na kusimamia utekelezaji wa uhamaji toka mfumo wa zamani wa analojia kwenda utangazaji wa mfumo mpya wa kidijiti.
2.3 MATOKEO YA TATHMINI KUHUSU UPATIKANAJI WA VISIMBUZI NA ELIMU KWA UMMA
Tathmini imeonyesha kuwa kati ya kaya zote zilizohojiwa kwenye miji saba, ni 0.1% ya kaya zilizodai uhaba wa visimbuzi wakati wa zoezi zima la uzimaji mitambo ya analojia. Matokeo mingine ni kama ifuatavyo:-
- 35.4% ya kaya zilizohojiwa walinunua visimbuzi kabla ya uzimaji mitambo ya analojia na kabla ya kuanza utoaji wa elimu kwa umma kuhusu mfumo mpya wa uatangazaji wa kidijiti
- 29.5% ya kaya walinunua visimbuzi kabla ya uzimaji mitambo ya analojia lakini baada ya utoaji elimu kwa umma
- 35.1% walinunua visimbuzi baada ya uzimaji mitambo
Takwimu hizi zinaonyesha kuwa upatikanaji wa visimbuzi na bei halikuwa tatizo kubwa lililoathiri mchakato mzima wa uhamaji kutoka mfumo wa analojia kwenda kidijiti kwenye miji hii saba. Vilevile elimu kwa umma ilisaidia sana kuhamasisha walaji kuhamia kwenye mfumo huu mpya wa utangazaji
2.4 ZOEZI LA UZIMAJI MITAMBO YA ANALOJIA
Ilifahamika kuwa zoezi la uzimaji mitambo ya analojia lilifanyika kwenye awamu nne ambapo kila awamu ilitoa nafasi ya mwezi mmoja. Jopo la wataalam limeridhika na utaratibu huu, ambao unatoa nafasi kubwa ya kutathmini matatizo yanayojitokeza kwenye awamu ya kwanza kabla ya kwenda kwenye awamu nyingine. Vilevile ulitoa fursa ya kuhakikisha kuwa eneo linalofuata linakuwa na visimbuzi vya kutosha na elimu kwa umma inatolewa kikamilifu kwa kutumia Radio na Televissheni za eneo husika.
2.5 WATENGENEZAJI NA WASAMBAZAJI MAUDHUI (CONTENT SERVICE PROVIDERS)
65% ya watengenezaji na wasambazaji wa maudhui walikuwa wamejiunga na mfumo wa kidijiti kabla ya uzimaji wa mitambo ya analojia.
Sababu kubwa ya vituo vingine kutojiunga na mfumo huu kwa wakati ilikuwa ni sababu za kimazoea kwamba huenda mitambo isingezimwa kwa wakati uliopangwa.
Mpaka sasa vituo vyote vilivyopo Dar es Salaam vimeshajiunga na mfumo huu kasoro kituo kimoja.
3.0 MAJUMUISHO
3.1 Jopo la wataalam limeridhika kuwa watazamaji wengi waliokuwa kwenye mfumo wa analojia walijiunga kwenye mfumo wa kidijiti. 11% tu ndio ambao hawakuweza kujiunga kwa sababu mbalimbali kama nilizoelezea mwanzoni. Idadi hiyo inaweza kuwa imepungua kwa vile watu wamekua wakiendelea kununua visimbuzi,
3.2 Zoezi hili halijawanyima watanzania haki ya kupata habari kwani wengi tayari wameshajiunga na mfumo huu mpya. Jopo liliona kuwa sababu ya malalamiko mengi yalitokana na tabia halisi ya wanadamu kuogopa mabadiliko,
3.3 Kutokana na takwimu zilizokusanywa, jopo limeridhika kabisa kuwa elimu kwa umma ilitolewa kwa kiwango kikubwa kwani 90% ya kaya zilizotembelewa walikuwa na habari kuhusu mfumo huu mpya wa utangazaji kwa njia ya kidijiti,
3.4 Hatua madhubuti zilichukuliwa kuhakikisha kuwa kabla eneo husika kuzimwa mitambo ya analojia kulikuwa na visimbuzi vya kutosha,
3.5 Mfumo huu mpya wa kidijiti utatoa fursa nzuri kwa watengenezaji na wasambazaji wa maudhui kutumia muda wote kutengeneza vipindi vizuri badala ya kujihusisha na usimikaji miundo mbinu ya utangazaji,
3.6 Mfumo huu mpya wa utanagazaji kwa njia ya kidijiti umeongeza ubora wa picha na channel nyingi. Juhudi zifanyike kuwa na channel nyingi za nyumbani badala ya nje ya nchi.
3.7 Jopo limeridhika kuwa mfumo huu mpya haujapunguza idadi ya watazamaji wa luninga ila watazamaji wamegawanyika kutazama channel mbalimbali na hivyo kujenga hisia kuwa watazamaji wamepungua.
3.8 Maeneo mengi yaliyokuwa yanapokea channel moja mpaka tatu sasa wanaweza kuona channel za kinyumbani zaidi ya tano.
3.9 Uhamaji kutoka DVB-T kwenda DVB-T2 uende kwa nguvu ya soko kwani dhana nzima ilikuwa kuhama mfumo wa analojia kwenda kidijiti, na viwango vyote hivi viwili vinatoa matanagazo ya kidjiti
4.0 HITIMISHO
Kutokana na matokeo ya tathmini iliyofanyika serikali inashauriwa iendelee na zoezi la uzimaji mitambo ya analojia sehemu zilizobakia. Jopo limeridhika na uandaaaji na usimamizi wa zoezi hili na kwamba kasoro zilizojitokeza ni sababu ya hofu ya mabadiliko na uzoefu wa walaji kwenye matumizi ya visimbuzi. Vilevile kuna faida nyingi za mfumo wa kidijiti ambazo watoa huduma wanatakiwa kuzitumia ili kuchochea ukuaji wa uchumi nchini.
Serikali inashauriwa kutoa punguzo la kodi kwa visimbuzi ili kuwawezesha watanzania wengi zaidi kununua visimbuzi na kupata habari kwa njia ya Luninga
Naomba niwakabidhi ripoti hii ambayo ina maelezo na taarifa za kina kuhusu zoezi tathmini hii.
Imetolewa na:
Prof. Nerey Mvungi Mtaalamu wa Mawasiliano ya ki electronic
Dr.Francis Sichona Mtaalamu wa Takwimu
Mr.F.M Ishengoma Mtaalamu wa Habari na Mawasiliano
JOPO LA WATAALAMU TOKA CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM
19 FEBRUARI 2014