Naomba nianze kwa kukujulia hali. Natumaini hujambo na unaendelea vyema na maisha.Najua mihangaiko ni mingi.Vikwazo pia haviishi.Lakini hayo ndio maisha.Isingekuwa hivyo pengine wala usingetamani kuishi.Pamoja na mikwaruzo mbalimbali ya maisha,sote tunapenda kuishi.Hatutaki kuiaga dunia kamwe.Mwenzetu mmoja akiiaga dunia tunamlilia kwa uchungu.Ipo sababu.Niijuayo mimi ni matumaini kwamba kesho itakuwa bora kuliko leo na jana.Maisha yanaendelea.
Yupo mwenzetu mmoja ameniandikia na kuniambia kwamba yeye tayari ana kazi ambayo inamlipa kiasi fulani japo sio cha kutosha.Pamoja na kuwa na kazi,mwenzetu analalama kwamba amefanya kazi kwenye kampuni anayofanyia kwa miaka takribani kumi na hajapandishwa cheo.Anatamani kupandishwa cheo.Afanyeje ili apandishwe cheo?
Kama ilivyo kwa mwenzetu aliyeuliza swali, wengi tunapenda vyeo.Ndio hulka ya binadamu. Kuna kuridhika fulani kunakotokana na kuwa na cheo kikubwa.Wakati mwingine haijalishi hata kama cheo alichonacho mtu hakiendani na kipato anachopata.Anachojali yeye ni kwamba yeye ndio Rais,Mkurugenzi Mkuu,Mkuu wa Mkoa,Mwenyekiti,Meneja nk. Kila mahali pana vyeo…hata jela kuna mfungwa mkuu nk.
Kwa wengi,cheo humaanisha kuongezeka kwa kipato.Cheo humaanisha mazingira mazuri zaidi ya kazi.Kama alikuwa kwenye kajiofisi kadogo basi anajua akipata cheo ina maanisha kuwa na ofisi kubwa na pengine hata kitanda cha kupumzika akichoka achilia mbali kuwa na luninga ofisini na mambo mengine kede.
ENDELEA KUSOMA MAKALA HII KWA KUBOFYA HAPA CHINI
Sasa ufanyeje ili upandishwe cheo.Leo tutaangalia mambo 7 ambayo mtu anaweza kufanya ili kupandishwa cheo.Lakini kabla sijaenda mbali sana,naomba nikutahadharishe kwamba mbinu ninazokupa zisiwe ndio muongozo wako.Lazima ujivike uhalisia(naturality) kwanza. Mbinu hizi ni kukusaidia tu.Ukizifuata kwa kanuni mpaka ukajisahau kwamba wewe ni nani na unatoka wapi,utatumbukia shimoni.
- Fanya Kazi Yako Vizuri: Najua kwa wengi hili linaonekana kuwa wazi.Kama hufanyi kazi vizuri basi huwezi kupandishwa cheo.Au sio? Jibu ni kwamba ingawa huo ndio ukweli wapo watu wengi ambao hawafanyi kazi “vizuri” na badala yake wanafanya tu kazi ili mradi siku iishe aondoke zake akasubiri mwisho wa mwezi apate mshahara.Kwa bahati mbaya,waajiri na watu walio na mamlaka ya kukupandisha cheo huwa wanaona hili kwa urahisi sana.Ipende kazi yako,ipende kampuni unayofanyia kazi. Weka uadilifu na maarifa ya ziada katika kazi zako.Cheo kitakuja.
- Onekana: Kisichopo machoni ni vigumu kuwepo moyoni pia.Huo ni msemo mzuri na unaoweza kukumbusha umuhimu wa kuonekana.Unapokuwa kazini hakikisha kwamba watu(hususani wakuu wako wa kazi) wanakuona na wanaona kazi unayoifanya.Usidanganywe na mtu anayekuambia kwamba ukionekana onekana unakuwa kama unajipendekeza.Hapana.Kama wewe ni mtu wa kujifichaficha,inaonyesha wazi kwamba hujiamini na hivyo hata ukipandishwa cheo kuna ulakini kama utayaweza madaraka yako mapya.Kwa maneno mengine,ondoa soni.Onekana.
- Jitolee: Upo mtazamo fulani kwamba kila unachokifanya kazini(hususani cha ziada au nje ya mkataba wa kazi yako) basi ni lazima kiambatane na ujira fulani.Huo ni mtazamo usiofaa sio tu kwa sababu hautokusaidia kupanda cheo bali hata kwenye maisha ya kawaida nje ya kazi.Kama kuna mtu anahitajika kwenye idara yako kwenye kutoa maelezo fulani,mahali fulani bila hata malipo ya ziada,kuwa wa kwanza kujitolea kufanya.Mwenzako ana tatizo fulani la kikazi,msaidie.Wakati mwingine usingoje kuulizwa au kuombwa.Kuwa wa kwanza kuomba kusaidia.
- Zungumzia Ndoto Zako na Wakuu Wako wa Kazi:Kuna nyakati ambazo ni muhimu kuzungumzia ndoto zako.Kama unataka kupandishwa cheo basi unaweza kabisa kuzungumzia ndoto hizo na wakuu wako wa kazi.Lakini kuwa makini usifanye hivyo kwa vitisho wala majibizano.Kwa weledi kabisa jadili ndoto hizi na wakuu wako.Unaweza kufanya hivyo kwa kuweka swali mezani kwamba nifanyeje ili niweze kupandishwa cheo?Wakuu wengi wa kazi wanaelewa kuhusu ndoto za namna hii kwani hata wao walishapitia huko.Mara nyingi watakusaidia kutimiza ndoto zako.Ila kuwa makini usiongelee kuhusu kuchukua cheo cha mtu ambaye unamwambia ndoto zako.Anaweza akakuhujumu.
- Husiana/Shirikiana Vizuri na Watu: Kushirikiana vizuri na watu kunakwenda sambamba na kuepuka migogoro.Kimsingi kuepuka migogoro ni matokeo ya mahusiano mema miongoni mwa watu(wafanyakazi).Watu wengi wamepitwa na vyeo sio kwa ukosefu wa ujuzi au ufahamu katika kazi zao bali kwa sababu hawaonekani kuwa na uhusiano mzuri na watu au wafanyakazi wenzao.Kumbuka kwamba ninapozungumzia mahusiano mema kazini simaanishi umaarufu.Unaweza kuwa maarufu kazini kwa sababu labda baba yako ni mtu anayefahamika.Lakini kama hauna mawasiliano mema na watu,huaminiki na wala wenzako hawawezi kukutegemea katika kitu fulani,basi cheo nacho kitakupiga chenga.Epuka kujenga maadui,kuwa tegemezi,jenga mbinu nzuri za kuwasilisha kwa wenzako mawazo yako.
- Changia Mawazo: Kila unapopata nafasi,changia mawazo chanya katika vikao au mazungumzo ya kawaida kazini. Jadili kwa uwazi na umakini jinsi ambavyo unadhani mnaweza kufanya ili kuboresha utendaji wenu wa kazi na hivyo kuleta faida zaidi. Wakuu wengi wa kazi(sio wote) hupenda kuona mtu ambaye ana mawazo chanya na ambayo anawaza kwa mapana na marefu. Hiyo sio tu sifa ya uongozi bali pia ishara muhimu kwamba ukipandishwa cheo,itakuwa kwa faida ya kampuni na pia wewe binafsi.
- Jiwekee Malengo: Kama ilivyo katika maeneo mengine ya kimaisha,ni muhimu kuwa na mipango na malengo madhubuti. Kama unataka cheo zaidi au malipo zaidi basi usisite kujiwekea malengo.Unaweza kusema kwamba nitafanya kazi katika kampuni hii kwa miaka mitano ijayo.Ukiona miaka mitano imefika na hakuna hata dalili za mambo kubadilika,kubaliana na matokeo na nenda aidha kutafuta ujuzi zaidi au kubadilisha muajiri.Usijisikie vibaya kushindwa kufikia malengo yako.Kumbuka haijalishi umeshindwa namna gani bali unachokifanya baada ya kushindwa.
Mwisho kumbuka cheo ni dhamana. Unapofikia malengo yako na kupata cheo unachokitaka,kumbuka kutotumia vibaya madaraka uliyopewa.Bila shaka umeshaona jinsi ambavyo watu mbalimbali maarufu duniani wameporomoka kutoka katika ngazi ya vyeo waliyokuwa wameipanda kwa taabu na muda mwingi kutokana na kashfa za matumizi mabaya ya madaraka.
NA JEFF MSANGI
NA JEFF MSANGI