UANACHAMA wa aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe umetajwa kuwa ‘kaa la moto’ kwa uongozi wa chama hicho hata kabla ya kiongozi huyo kujibu mashitaka 11 yanayomkabili ili kunusuru uanachama wake.
Duru za siasa ndani ya chama hicho, zinasema Chadema haiko tayari kukabiliana na mtikisiko wa Zitto kuvuliwa uanachama, kwa kuwa hatua ya kuvuliwa madaraka tayari imegharimu umoja na utulivu wa chama hicho.
Taarifa hizo zinasema kwa sasa kuanzia Kamati Kuu mpaka wanachama, kuna mpasuko mkubwa ambao namna pekee ya kuuziba ni kumshawishi Zitto na Mwenyekiti Freeman Mbowe, kupatana.
Hata hivyo, wakati jitihada za kuwapatanisha zikiendelea, duru za siasa zinaeleza kuwa kambi ya Mbowe ina wajumbe wanaoshinikiza kumtosa Zitto na kuwa tayari kukabiliana na gharama zake.
Majimbo
Mtoa habari wetu kutoka ndani ya Chadema anaeleza kuwa hofu kubwa iliyopo kama Zitto atanyang’anywa uanachama, ni ukweli kuwa katika Uchaguzi Mkuu wa 2015, wanaweza kupoteza majimbo mengi na kuipa mwanya CCM kupita kirahisi.
“Ni kweli huu si mgogoro wa kwanza kwa Chadema na mara zote viongozi walipovuliwa madaraka kulitokea mtikisiko, lakini si kama huu wa Zitto… mbaya zaidi, majimbo ya viongozi tuliowavua madaraka leo hii yamepokwa na CCM, hatuko tayari kupoteza zaidi,” alisema mtoa habari huyo ambaye hakuwa tayari kutajwa jina.
Akitoa mfano, alisema mgogoro kati ya Chadema na Katibu Mkuu wa zamani Dk Aman Kabourou, ndio ulisababisha jimbo la Kigoma Mjini lililokuwa moja ya majimbo ya Chadema, leo hii kukaliwa na CCM.
Mbali na Kigoma Mjini, mtoa habari huyo alikumbushia pia jimbo la Tarime, alikokuwa Makamu Mwenyekiti, Chacha Wangwe, ambalo mbali na kushinda katika uchaguzi mdogo baada ya kifo chake, leo linashikiliwa na CCM.
“Unajua hata kwa Zitto (Kigoma Kaskazini) ukiangalia kama kweli tukimtosa, sina hakika kama tutarejesha lile jimbo. Na hata kwa Arfi (Said, Makamu Mwenyekiti aliyejiuzulu, Mbunge wa Mpanda Kati), kama yule mzee tukimchezea hatuna chetu,” alisema.
Alipoulizwa afafanue kuhusu mpasuko huo, alikataa na kuhoji: “Kwani wewe huoni, mbona wenzenu wameandika mpasuko uliotokea katika Kamati Kuu?”
Mbali na mtoa habari huyo, hata katika waraka unaodaiwa kusababisha mtafaruku huo ambao Dk Kitilla Mkumbo alikiri kuuandaa, Chadema imetajwa kuwa na udhaifu wa kushinda majimbo katika uchaguzi mdogo.
“Tangu uongozi huu uingie madarakani, kumefanyika uchaguzi mdogo mara nane, lakini tumeshinda mara mbili tu sawa na asilimia 25,” alisema Dk Mkumbo katika waraka wake.
Usuluhishi
Pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu kutangaza kumwandikia Zitto mashitaka yake na kumpa siku 14 za kujibu, tayari kumeripotiwa kuwa nyuma ya pazia chama hicho kimeamua kumwangukia Zitto yaishe, ikiwa ni pamoja na kumwahidi cheo kikubwa kuliko Naibu Katibu Mkuu.
Kwa mujibu wa taarifa hizo katika uchaguzi mkuu wa Chadema Juni mwakani, Zitto atashawishiwa kugombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti bila mpinzani au na mpinzani dhaifu na Mbowe ataachiwa kugombea uenyekiti bila mpinzani au na mpinzani dhaifu, lengo likiwa kurejesha umoja wakati wakijiandaa na Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Pia inadaiwa Zitto ataahidiwa kupewa fursa ya kugombea urais wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu wa 2020.
Wasira
Akizungumzia mgogoro huo akiwa mkoani Kagera, Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Stephen Wasira, alisema anajivuna kwamba ndani ya chama chake hakuna ubaguzi kama ilivyo katika vyama vingine vya upinzani ambavyo alidai kiongozi wa ngazi ya juu lazima atoke kabila fulani.
Alidai katika baadhi ya vyama, ikitokea mtu ametoka kabila tofauti akataka kugombea uongozi ngazi ya juu, kunazuka vurugu na kufukuzana kwa visingizio vya kuvunja katiba za vyama hivyo.
“Mara nyingi huwa natumia kauli ya Mwalimu Julius Nyerere kuwa ubaguzi ni sawa na kula nyama ya mtu, ukiishaionja huiachi kwa hiyo wameionja inawatafuna. “CCM hatuna sababu ya kushangilia matatizo yao na hatuwaogopi wala hatutaki upinzani ufe, kwa sababu upinzani ni mfumo ulio ndani ya nchi, ila nasi tuache makundi yanayotokana na uchaguzi, ili tuendelee kushika Dola kama ilivyo ada yetu,” alisema Wasira.
Vyuo vikuu
Baadhi ya wanachama wa Chadema, wakiwamo wanafunzi wa vyuo vikuu, walikutana Dar es Salaam jana na kutangaza mgogoro wa kiutawala kati ya wapigania demokrasia ndani ya chama hicho na wahafidhina.
Wanachama hao waasi ambao walisema ni wapigania demokrasia ndani ya chama hicho; lakini kwa tafsiri ya viongozi wa Chadema ni ‘wahaini’, wametangaza kuzunguka nchi nzima kuhamasisha wanachama wa chama hicho wakatae baadhi ya watu waliopandikizwa kwa kukaimishwa nafasi za uenyekiti kwa manufaa ya wahafidhina.
Baadhi ya wanachama hao wakiongozwa na Greyson Nyakarungu, walidai wanatambua kuwa mgogoro ndani ya Chadema umetokana na Mwenyekiti Mbowe kutamani kuendelea kuongoza chama kwa gharama yoyote.
Nyakarungu alidai Mbowe anatamani aendelee kutawala hivyo kuzunguka katika baadhi ya mikoa na kuwaondoa katika nafasi zao viongozi waliochaguliwa kidemokrasia, ambao wanaonekana kutomwunga mkono kwa kisingizio cha kutowajibika.
Nyakarungu ambaye alijiita Brigedia wa Uasi huo, alisema watu wote waliopenyezwa kukaimu nafasi hizo za uongozi mikoani wajiondoe haraka “kabla hatujawaondoa kwa nguvu.
“Sisi tumeamua kama tulivyozunguka nchi nzima na kampeni ya Washa Taa Mchana, tutazunguka nchi nzima kuwaambia wanachama ubovu huu wa wahafidhina. “Tunamwonya Zitto na Dk Mkumbo tabia zao za kusema kuwa wanaheshimu uamuzi wa CC huku wakijua ni nini kitatokea, waache mara moja, kwani unyonge wa aina hii ni kuendelea kuruhusu baadhi ya watu kupora rasilimali za chama,” alidai Nyakarungu.
Nyakarungu, Jeremia Fumbe wa Chuo Kikuu cha Ardhi na Likapo Bakari ambaye alifukuzwa Chuo Kikuu cha Dodoma, walisema wao ni majeruhi wa kufinyangwa kwa demokrasia ndani ya chama hicho, na kila hoja ambayo wanatoa wamekuwa wanaitwa masalia ya Zitto.
Nyakarungu alisema watu wote wanaoitwa wasaliti ndani ya chama hicho au ‘wanaotumwa na CCM’ hoja yao imekuwa moja tu ya matumizi ya fedha za chama hicho, hoja ambayo pia walidai imemgharimu Zitto.
“Tunafikia hatua wahafidhina wanasema wazi kuwa ni bora chama kishuke daraja kuliko kupewa mtu wa nje, mtu wa kuja, mtu wasiyemfahamu,” alisema Nyakarungu na kusisitiza kuwa wanachama wa Chadema kutoka Mara na Kigoma ndio wamekuwa wahanga zaidi.
Nyakarungu, ambaye alidai alijiunga na chama hicho mwaka 2005 na kushiriki kujenga, alisema kilichomponza Zitto ndani ya chama hicho ni kuhoji matumizi ya chama hicho kupitia kamati ya Bunge ya PAC, ndio maana alishambuliwa yeye binafsi wakati huo ulikuwa uamuzi wa Kamati ya Bunge.
“Viongozi wetu wa Chadema wanahoji Serikali na matumizi ya fedha za walipa kodi wakitaka uwazi na usawa, leo wanataka kutonywa mapema ili wafanye marekebisho ya kuficha uovu wa matumizi ya pesa? “Zitto kama kiongozi anayejipambanua asingeweza kuwatonya ili wafiche uchafu katika matumizi ya fedha huku akitengeneza nafasi ya kuumiza vyama vingine, hii ni dalili ya udikteta. Na kwa kuwa aligusa mkia wa mfalme nge ni lazima ang’atwe,” alidai Nyakarungu.
HABARI LEO