Shirika la fedha duniani limeonya jumuiya ya Afrika Mashariki dhidi ya kuharakisha mpango wake wa kutaka kuwa na sarafu moja.Mataifa ya jumuiya hiyo yalianzisha mkakati wao wa kutaka kubuni sarafu moja inayoweza kutumika katika nchi wanachama ili kurahisisha biashara katika kanda hiyo.
Mataifa matano ya wanchama wa jumuiya hiyo mwishoni mwa mwezi Novemba mwaka jana, yalitia saini mkataba wa kuanza mkakati wa kutafuta sarafu moja katika kipindi cha miaka kumi ijayo , mpango wanaotumai utapanua biashara katika kanda hiyo nzima.
Mpango huu utashuhudia nchi hizo zikiwianisha sera zao za kifedha na kuchumi na kuweza kubuni benki kuu moja.
Kenya, Uganda, Tanzania na Rwanda tayari husoma bajeti zao kila mwezi Juni.
Ushauri huu kutoka kwa shirika la fedha duniani, unakuja wakati kanda ya Ulaya ingali inakumbwa na matatizo ya kiuchumi kutokana na viwango vikubwa vya madeni yao huku mataifa wanachama wakikabiliwa na ukosefu wa ajira.
ENDELEA KUSOMA HABARI HII KWA KUBOFYA HAPA CHINI
Mkuu wa shirika hilo ambalo yuko ziarani Kenya, Christine Lagarde amesema kuwa kuwianisha sera za kifedha ni wazo zuri lakini pia ni changamoto kubwa.
Bi Lagarde alisema itakuwa muhimu kwa Kenya kutoa funzo kutoka katika mataifa ya Euro ambayo yanatumia sarafu moja na kusoma aina ya changamoto zinazokabiliwa nazo.
Ziara ya Bi Lagarde nchini Kenya ni kama jambo la kawaida kwa shirika la fedha duniani kuhakikisha kuna uthabiti wa kiuchumi katika sehemu mbali mbali duniani.
Kenya ni nchi ya pili kwa ukubwa kwa uwekezaji katika kanda ya Afrika Mashariki.
Kuweka wazi soko la pamoja la biashara kwa mataifa wanachama wa mataifa ya Afrika Mashariki itakolesha biashara na kuinua maisha ya watu wa kipato cha kadri ambao wanastawisha zaidi uchumi.
BBC SWAHILI