Walikwenda kuwatoa wenzao waliokamatwa kwa mauaji
Wenzao wachoma kituo, gari la polisi, pikipiki, majadala ya kesi
Watu watatu wameuawa kwa kupigwa risasi na askari wa Jeshi la Polisi wa Kituo cha Malinyi Wilaya ya Ulanga mkoani Morogoro, na wengine kujeruhiwa vibaya.
Tukio hilo lilitokea jana asubuhi baada ya kundi la wakazi wa Kijiji cha Igawa kuvamia kituo hicho wakitaka kuwatoa wenzao waliokamatwa kwa tuhuma za mauaji.
Akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu, Diwani wa Kata ya Malinyi, Said Tilla, alisema tukio hilo lilitokea jana majira ya asubuhi baada ya wakazi hao wakiwamo waliouawa na kujeruhiwa kuvamia kituo hicho.
Tilla, alisema kundi la wakazi hao waliandamana hadi katika kituo hicho wakiwa na matawi ya miti kushinikiza kutolewa kwa wenzao hao walikamatwa siku mbili zilizopita kwa madai ya kumua mfugaji wa jamii ya Kisukuma, Matanji Luhembe (16).
ENDELEA KUSOMA HABARI HII KWA KUBOFYA HAPA CHINI
Alisema kitendo cha wakazi hao kuvamia kituo hicho kinatokana na askari wake kuwakamata wakulima hao watatu peke yao na kuwaacha wafugaji jamii ya Kisukuma wakati wao ndiyo chanzo cha mapigano hayo.
Wafugaji hao wanadaiwa kumuua mjumbe wa kamati ya mazingira ya kijiji hicho, Victory Maleka Desemba 12, mwaka huu.
Alisema wakazi hao walipofika katika kituo hicho, waliwakuta askari saba wakiendelea na kazi baada ya kuzidiwa waliamua kuwapiga risasi za moto na kuua watatu na kujeruhi wengine wanne kisha kukimbilia kusikojulikana.
“Wananchi hawakuwa na siraha zozote bali walikuwa na matawi tu ya miti, walipofika na kutaka wenzao watolewe ndipo askari wakaanza kupiga risasi ovyo na kuwaua watu watatu papo hapo na wengine kujeruhiwa na kisha hao askari wakakimbia na kutelekeza kituo hicho,” alisema Diwani Tilla kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Aliwataja waliouawa kwa kupigwa risasi kuwa ni Leon Chikwale, Andrew Kikonoki na Edson Kidunde, wakazi wa kijiji hicho.
Alisema majeruhi hao walikimbizwa Hospitali ya Misheni ya Lugala kwa ajili ya kupatiwa matibabu zaidi.
Diwani huyo, alisema baada ya mauaji, wakazi hao waliamua kuchoma moto kituo hicho, na gari la polisi na pikipiki za kituo hicho huku baiskeli zilizokamatwa katika matukio mbalimbali wakizichoma pia.
Hata hivyo, alisema katika tukio hilo hakuna askari yoyote aliyejeruhiwa na wakazi hao na kwamba Jeshi la Polisi limeamua kuongeza nguvu ya askari kutoka sehemu mbalimbali ikiwamo wilaya ya Kilombero na mkoa wa Morogoro ili kutuliza ghasia hizo.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga Furaha Lilongeri, alithibitisha kutokea kwa mauaji hayo yaliyosababishwa na askari hao kuwapiga raia watatu waliokuwa miongoni mwa wananchi waliovamia kituo cha polisi.
Kamanda wa polisi mkoani Morogoro, Faustine, Shilogile, alithibitisha kutokea kwa mauaji ya watu hao papo hapo na wengine kujeruhiwa baada ya kutokea mapambano baina yao.
Shilogile alisema watu hao waliouawa ni kati ya zaidi ya wakazi 500 wa kijiji waliovamia kituo hicho wakishinikiza kutolewa kwa wenzao wanne waliokamatwa kwa tuhuma za mauaji ya watu wawili na kuchoma moto nyumba saba.
Alisema polisi walilazimika kutumia nguvu kuwatawanya wakazi hao waliovamia kituo kwa nia ya kutaka kukichoma moto.
Kamanda huyo, alisema wakazi hao walichoma moto gari la askari aina ya Pick up, pikipiki ya polisi, baiskeli tano za vielelezo na majalada ya kesi yaliyokuwamo kituoni hapo .
Alisema wakazi hao walivamia kituo hicho kwa nia ya kuwatoa watuhumiwa wanne waliokamatwa usiku wa Desemba 14, mwaka huu kwa tuhuma za mauaji ya watu hao wawili, lakini wakati tukio hilo likiendelea, walikuwa wameshahamishiwa kituo kingine cha polisi.
Alisema majeruhi wanne wa tukio hilo wamekimbizwa Hospitali ya Lugalo kwa matibabu zaidi huku jeshi hili likiongeza nguvu kutuliza ghasia hizo.
Tukio la kuuawa mfugaji huyo na kusababisha watu wannne kukamatwa lilitokea Desemba 13, mwaka huu baada wafugaji wa jamii ya Kisumuma kumpiga na kumjeruhi vibaya hadi kumuua Victory Maleka (55).
Chanzo cha kifo cha Maleka ni wafugaji wa Kisukuma kumtuhumu marehemu kuwaelekeza askari wa wanyamapori wa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) maeneo wanayoishi wafugaji hao kinyume cha sheria na ndipo walipomvamia na kumpiga na kusababisha kifo chake.
Hata hivyo, baada kifo hicho wakazi hao walishikwa na hasira na kuamua kujikusanya na kulipiza kisasa kwa jamii ya wafugaji hao kwa kwa kumuua mwenzao, Matanji Luhembe.
Luhembe alifariki baada ya kupigwa na wakazi hao waliomvamia ghafla akiwa na wenzake wakati wa harakati za kukimbia.
Luhembe alishindwa kujiokoa na kuanguka chini kutokana na tatizo la ugonjwa wa pumu na kupigwa hadi kufa.
CHANZO: NIPASHE