Pamoja ni kiasi kidogo cha pesa alicholipwa ($85) kwa kazi ya kutafsiri (kwa ishara za uongo) hotuba za viongozi wakati wa hafla ya kumbukumbu ya Nelson Mandela jijini Johannesburg, Afrika Kusini Jumanne (Dec 10) wiki hii, jina la mkalimani huyo Thamsanqa Jantjie limeendelea kutajwa katika vyombo vya habari japo ni kwa sifa mbaya.
Baada ya kuandamwa kwa kutoa ishara zisizotengeneza maana yoyote wakati wa hotuba za viongozi akiwemo Rais wa Marekani Barrack Obama katika hafla hiyo, sasa mambo yanazidi kumuendea vibaya, siyo yeye tu Jantjie bali na wote waliohusika kumpa nafasi ya kazi hiyo kitu kinachorudisha sifa mbaya kwa nchi yake pia.
Jana (Dec 13) mtandao wa Afrika Kusini eNCA, umeripoti kuwa bwana Jantjie amewahi kuwa na historia ya kutuhumiwa kubaka (1994), aliwahi kutuhumiwa wizi (1995), kuvamia nyumba (1997) pamoja na kutuhumiwa kuuwa na kuteka (2003).
Taarifa hiyo imeongeza kuwa tuhuma nyingi dhidi yake ikiwemo ile ya kubaka zilifutwa kutokana na kuwa na matatizo ya kiakili kiasi cha kutoweza kuhimili kesi, lakini aliwahi kuhukumiwa miaka mitatu jela kwa kosa la wizi.
ENDELEA KUSOMA HABARI HII KWA KUBOFYA HAPA CHINI
Taarifa za historia ya matukio aliyowahi kuyafanya miaka iliyopita zimekuja baada ya hivi karibuni Mr Jantjie, kujitetea kwa tukio la kutoa tafsiri feki wakati wa hotuba za viongozi katika hafla ya kumuaga Madiba, kwa kudai kuwa aliugua ghafla akiwa jukwaani na kuanza kusikia makelele kichwani, mara aliona malaika wakimjia wakati shughuli ikiendela, na kumfanya achanganyikiwe na kuanza kurusha tu mikono bila ya kuwa na maana yoyote katika lugha ya ishara.
Wengi wanahoji ilikuwaje kwa mtu mwenye sifa zisizokidhi viwango vya kupata nafasi ya kufanya kazi ya ‘high profile’ kama ile na viongozi wakubwa wa dunia, na ndiyo maana haishi kufuatwa na vyombo vya habari kila kukicha.