Licha ya kuwa ni siku ya huzuni kwa dunia nzima, hotuba ya Rais wa Marekani, Barack Obama imewagusa maelfu ya watu waliokuwa kwenye Uwanja wa FNB katika ibada ya kitaifa kumwaga Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Nelson Mandela.
Obama aliyetumia dakika 20 katika hotuba yake iliyokuwa ikikatizwa na kelele za kumshangilia, aliwataka vijana wa Afrika na dunia nzima kuiga maisha aliyoishi Mandela kama yeye alivyojifunza mambo mengi kutoka kwa mzalendo huyo.
“Miaka 30 iliyopita nikiwa mwanafunzi, nilisoma Kitabu cha Mandela na tangu siku hiyo nilijifunza, nikajenga roho ya uthabiti. Iliamsha uwajibikaji kwa ajili yangu na kwa ajili ya watu wangu... hakika Mandela amenifanya niwe hivi nilivyo leo. Michelle na mimi tumenufaika sana na Mandela,” alisema Obama na kuongeza:
ENDELEA KUSOMA HABARI HII KWA KUBOFYA HAPA CHINI
“Mandela alinifanya niwe mtu ninayesimama mbele yenu leo, alichangia kunifanya kuwa kiongozi bora. Nitaendelea kuiga mfano wake,”
Katika sherehe hizo, Obama alipokewa kwa shangwe na kushangiliwa kila alipopita na kila alipozungumza tofauti na ilivyokuwa kwa Rais wa nchi hiyo, Jacob Zuma ambaye alikuwa akizomewa.
Obama alimtaja Mandela kama kiongozi anayefaa kuigwa kwani pamoja na kukaa gerezani kwa miaka 27 akipigania uhuru, hakutaka kung’ang’ania madaraka na badala yake alistaafu kwa hiari yake, tofauti na viongozi wengi wa Afrika.
“Mandela alionyesha uongozi wa vitendo na kujaribu, alikuwa ni mwanamume, binadamu wa kawaida, mume, baba na kiongozi shupavu,” alisema Obama.
Pia Obama alisema, Mandela aliachiwa huru kama mfungwa, lakini kama mwalimu ambaye alitumika kutuonyesha kuwa, ni lazima kuwaamini wenzako ili nao wakuamini.
“Kufundisha upatanisho, hakuhitaji kudharau historia mbaya ya nyuma bali ni kuikabili kwa umakini, ukweli na uhalisia wake. Mandela alibadili sheria, lakini alibadili mioyo yetu pia,” alisema.
Katika risala hiyo, Obama alimtaja Mandela kama mwanamapinduzi mkubwa wa karne ya 20 aliyeibadilisha mioyo ya watu wake, akaimarisha mapatano na maelewano kwa wazungu na weusi.
“Amezaliwa kipindi cha Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia, kijana aliyekuwa akichunga ng’ombe na kuteswa na wakubwa zake wa kikabila, lakini ameibuka na kuwa mwanamapinduzi mkuu wa karne ya 20,” alisema Obama.
Vilevile, Obama alimfananisha Mandela na Abraham Lincoln, Rais wa zamani wa Marekani kwa kuiunganisha nchi yake pale ilipokuwa inataka kuvurugika.
Rais huyo aliufanya umati katika uwanja huo ulipuke zaidi kwa furaha baada ya kuzungumza neno la Kizulu, ‘ubuntu’ linalomaanisha utu au ubinadamu ambapo alisema Mandela ameimarisha utu na ubinadamu kwa Waafrika Kusini.
“Alidumisha ‘utu’ miongoni mwetu. Utu ambao tunaweza kuupata kwa kushirikiana na kuwajali wanaotuzunguka,” alisema Rais huyo ambaye anatajwa kuwa Rais wa dunia. Obama alionyesha umahiri wake katika risala hiyo na katika sehemu ya risala hiyo alisema ni wajibu wa kila mmoja kuiga maisha aliyoishi Mandela.
“Ni lazima tujifunze kutoka kwake, kwa sababu Waafrika Kusini kwa jumla wao wameonyesha kuwa, tunaweza kubadilika.”
Obama alimtaja Mandela kama mtu asiyependa kujikweza bali aliyeshiriki kuonyesha mawazo yake na hofu na uhalisia wake hasa kwa kusema kuwa yeye si mtakatifu labda kama mtakatifu ni sawa na mwenye dhambi ambaye hachoki kujaribu. Kiongozi huyo alimalizia hotuba hiyo kwa nukuu muhimu za Mandela zinazosema kuwa, ‘Mimi ni kiongozi wa imani, mustakabali wangu, na mimi ni nahodha wa roho yangu’ na kuwataka Waafrika Kusini kuishi katika maneno hayo ya Mandela katika maisha yao.
“Hakika ilikuwa roho ya ajabu, tutamkumbuka sana. Mungu wabariki Waafrika Kusini,” alimaliza Obama. Kabla ya hotuba hiyo, Obama alifanya jambo la kihistoria kwa kupeana mikono na Rais wa Cuba, Raul Castro, kama ishara ya mapatano baada ya migogoro iliyoko baina ya nchi hizo mbili.
Kabla ya Obama kuzungumza, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon katika hotuba yake alisema kuwa, alijitoa muhanga kwa ajili ya usalama, uhuru na demokrasia ya nchi yake.
“Sherehe hizi za kumbukumbu zinadhihirisha upinde wa mvua wa taifa. Ninatumaini tutaweza kuuona upinde huo punde, kupitia mvua ya simanzi,” alisema Ki-Moon. Ki-Moon alimtaja Mandela kuwa ni kiongozi aliyejiandaa kupoteza kila kitu kwa ajili ya uhuru na demokrasia.
“Dunia imepoteza rafiki na mwalimu. Alikuwa ni zaidi ya viongozi wakubwa wa nyakati zetu; mwalimu mkuu aliyetufundisha kwa mifano,” alisema Ki-Moon.
Wakati huo huo, Mkuu wa Majeshi wa nchi hiyo, Jenerali Thanduxolo Mandela kwa niaba ya familia ya Mandela alipata nafasi ya kutoa risala yake kwa Rais huyo na alisema kuwa, familia hiyo ina bahati ya kuwa na mzazi kama Mandela.
“Utakumbukwa daima, hatuwezi kuusahau mchango wako katika familia na katika maisha ya Waafrika Kusini wote,” alisema Thanduxolo.
Baada ya Thanduxolo, walikuja wajukuu na vitukuu wa Mandela kwa niaba ya wajukuu wote, Pumla, Andile na Mbuso Mandela ambao walisema wana mengi waliyojifunza kwa babu yao ambaye walimtaja kuwa kioo cha familia na kuahidi kuwa wataishi na matendo yake.
Mandela atazikwa Jumapili.