Jeshi la Polisi linamshikilia Raia wa Vietnam Dong Van(47) kwa kumkamata akiwa na meno 65 na kucha 447 za Simba kinyume cha sheria vyenye thamani ya Shilingi Milioni 189,420,000.
Kamishna Msaidizi wa Polisi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Hamisi Selemani, amesema mtuhumiwa huyo alikamatwa juzi wakati alipotaka kusafirisha nyara hizo kwa kutumia Shirika la Ndege la Qatar Airways kwenda nchini Vietnam kupitia Doha.
Amesema alipopekuliwa alikutwa na nyara hizo ambazo alizihifadhi kwenye pakiti 7 za kahawa na pakiti moja ya mchele na kuzichanganya na pakiti nyingine 15 za vyakula vya aina mbalimbali
Kamanda Selemani amesema pakiti hizo ziliwekwa ndani ya begi la nguo ili kupoteza ushahidi wa aina ya mzigo alioubeba kwa wakaguzi wa uwanjani hapo.
Aidha amesema mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani mara baada ya uchunguzi kukamilika ili aweze kuchukuliwa hatua za kisheria.
CHANZO: TIMES FM