Mtoto Samir mkazi wa mtaa wa Langoni kata ya Miembeni,akiwa amefungwa kamba katika mguu wake wa kushoto huku upande mwingine ukiwa umefungwa katika chuma kizito kilichopo jirani na mlango.
Na Dixon Busagaga
MTOTO Samir anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka minne hadi mitano mkazi wa mtaa wa Langoni katika manispaa ya Moshi, amejikuta katika wakati mgumu kutokana na tabia ya bibi yake kumfunga kamba katika mguu wake kwa lengo la kumzuia asiende kucheza mbali na nyumbani kwao.
Tukio hilo limetokea hivi karibuni katika eneo hilo ambapo bibi huyo ambaye jina lake halikufahamika mara moja alikutwa akiwa amemfunga kamba ya kudu mjukuu wake huyo katika mguu wa kushoto huku sehemu nyingine ikiwa imefungwa katika chuma kizito.
ENDELEA KUSOMA HABARI HII KWA KUBOFYA HAPA CHINI
Kwa mujibu wa majirani walisema bibi huyo amekuwa akimfunga mtoto huyo mara kwa mara kwa zaidi ya nusu saa hasa nyakati ambazo bibi huyo amekuwa akifanya shughuli zake za usafi wa ndani pamoja na kufua.
Wakizungumza kwa sharti la kutotajwa majina,majirani hao wamesema imekuwa ni kawaida kwa bibi huyo ambaye anaishi na wajukuu zake kumfanyia kitendo hicho mtoto huyo huku akimzuia kucheza na wenzake wa nyumba za jirani.
“Sisi hiyo hali mbona tumeizoea mara kwa mara Samir akienda kucheza na wenzake huko mtaani,bibi yake akimkuta huko anamkamata na kisha kumfunga kwenye hilo chuma lililoko hapo mlangoni kwa zaidi hata ya nusu saa”alisema mmoja wa majirani.
Akizungumza tukio hilo Bibi huyo ambaye anakadiriwa kuwa na miaka zaidi ya 60 alikiri kumfunga mtotot huyo kwa madai kuwa amekuwa mtundu kupita kiasi na kwamba ametumia mbinu hiyo ili kumdhibiti asitoroke nyumbani.
“Hapa nyumbani naishi na wajukuu zangu ,wengine wako mashuleni na wengine wako kazini ambao ni wazazi wa huyu Samir,mmoja anafanya kazi Arusha,mwingine yuko hapo mjini(Moshi)sasa sina mtu wa kunisadia kumwangalia huyu mtoto”alisema Bibi huyo.
Alisema analazimika kumfunga kamba mtoto Samir kutokana na kuwa na tabia ya kwenda kuzurura katika nyumba za watu huku wakati mwingine huenda kucheza mbali na nyumbani jambo ambalo humpa shida kumpata kwa urahisi.
“Wakati mwingine nashikwa na hasira kumpiga siwezi hivyo naamua kumfunga kamba hapa mlangoni…watu wote si wazuri kumruhusu kuingia kila nyumba huko atafundishwa mambo mabaya ndio sababu nafanya hivi.”alisema Bibi huyo.
Mmoja wa wazazi walioshuhudia tukio hilo walisema wazazi wengi wamekuwa wakikosea kuwaacha watoto wao walelewe na bibi zao hali inayochangia kuwepo kwa vitendo vya ukiukaji wa hali ya watoto na kibinadamu kama ilivyotokea kwa mtoto huyo.
“Wazazi tumekuwa bize sana na shughuli za utafutaji ,hali hii inapelekea majukumu ya kulea watoto kuiacha kwa wasichana wa kazi na hata mama zetu kama ilivyo kwa familia hii ,sasa suala hili pia wakati mwingine linachangia makuzi mabovu kwa watoto”alisema Juma Nzota.