Meneja Mawasiliano wa TANAPA Pascal Shelutete akiongea na waandishi wa habari jijini Arusha alipokutana nao kutoa ufafanuzi kuhusiana na kutokuwepo kwa mpango wa kuikabidhi Hifadhi ya Taifa ya Katavi kwa wawekezaji kutoka Afrika Kusini kama ilivyoripotiwa na gazeti moja la kila wiki nchini hivi karibuni (Picha kwa hisani ya TANAPA)
…………………………………………………………………………….
Katika gazeti la Jamhuri Toleo Namba 129 Machi 25-31, 2014 kulikuwa na habari iliyoandikwa chini ya kichwa cha habari “Nyalandu ‘auza’ Hifadhi” ambapo maelezo ya habari hiyo yaliitaja Hifadhi ya Taifa ya Katavi kuwa inatarajiwa kukabidhiwa kwa wawekezaji kutoka nchini Afrika Kusini ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Lazaro Nyalandu.
Shirika la Hifadhi za Taifa linalosimamia Hifadhi ya Taifa ya Katavi pamoja na Hifadhi nyingine 15 nchi nzima linapenda kukanusha habari hiyo iliyoandikwa kwa lengo la kupotosha umma kama ifuatavyo.
ENDELEA KUSOMA HABARI HIII KWA KUBOFYA HAPA CHINI
Mosi, hakuna mpango wala uamuzi wowote uliopo au uliokwisha kufanywa wa kuingia Mkataba wa Uendeshaji wa aina yoyote ile baina ya Shirika la Hifadhi za Taifa na Mwekezaji yeyote kutoka nchini Afrika ya Kusini ikiwa ni pamoja na African Parks Network waliotajwa katika habari husika.
Pili, Sheria inayosimamia uanzishwaji wa maeneo ya Hifadhi za Taifa ikiwemo Katavi imelipa dhamana hii pekee shirika kusimamia maeneo haya kwa niaba ya Watanzania na ni kinyume cha sheria kukabidhi kwa wawekezaji kwa ajili ya usimamizi kama ilivyobainishwa katika habari hiyo.
Tatu, Shirika la Hifadhi za Taifa bado linao uwezo thabiti wa kusimamia uendeshaji wa Hifadhi ya Taifa ya Katavi ili kuhakikisha rasilimali za wanyama na mimea zinaendelea kutunzwa kwa miaka mingi ijayo kama ambavyo imekuwa ikifanya tangu kuanzishwa kwa hifadhi hiyo mwaka 1974.
Aidha, kama ambavyo shirika limekuwa likipanga katika mipango yake ya maendeleo mwaka hadi mwaka, katika mwaka mpya wa fedha ujao shirika limepanga kuongeza idadi ya watalii katika Hifadhi za Kusini ikiwemo Katavi Saadani, Mikumi na Ruaha. Mkakati huu utahusisha kuongeza ubora wa utoaji huduma ikiwa ni pamoja na malazi ili kukuza utalii wa ndani.
Shirika litafungua ofisi Jijini Dar es Salaam na kuimarisha ofisi za Mwanza na Iringa ili watalii wapate taarifa za Hifadhi na kuweza kufanya ‘bookings’ kwa urahisi. Aidha, kama ambavyo imekuwa ikifanyika kwa masoko ya nje, Shirika sasa litaanzisha ‘Road shows’ mbalimbali kwa soko la ndani na nchi za jirani. Vilevile, Shirika litaongeza kujitangaza kupitia Mitandao ya Jamii, TV, majarida na tovuti ya Shirika itaboreshwa katika kuarifu wadau masuala mbalimbali yanayojiri kwenye Hifadhi zetu.
Tayari Shirika limeanzisha Kurugenzi mpya ya Utalii na Masoko kwa ajili ya kutekeleza mkakati huu wa kuzifanya hifadhi za ukanda wa kusini kuvutia watalii wengi zaidi.
Imetolewa na Idara ya Mawasiliano
Hifadhi za Taifa Tanzania
30.03.2014