Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi imepiga marufuku bomoabomoa iliyopangwa kuanza katika jimbo la Kibamba, ili kupisha upanuzi wa barabara ya Morogoro.
Amri ya usitishwaji wa bomoabomoa hiyo imetolewa leo (Jumaatu) na Jaji Leila Mgonya, kufuatia maombi ya zuo la muda yaliyowasilishwa mahakamani hapo na wakazi wa jimbo hilo, kupitia kwa jopo la mawakili wao wanne, likiongozwa na Wakili Aidani Kitare.
Maombi hayo yaliwasilishwa mahakamani hapo na Abdallah Maliki kwa niaba ya wenzake 570, ambao ni wakazi wa maeneo ya Kimara, Mbezi na Kiluvya, dhidi ya Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Katika maombi hayo watoa maombi walikuwa wakiiomba mahakama itoe amri ya kuruhusu hali iendelee kuwa kama ilivyo, kwa maana ya kuwazuaia Tanroads kuendesha operesheni ya bomoabomoa, kusubiri kuisha kwa taarifa yao ya siku 99 kwa Serikali, ili kiufungua kesi ya kupinga bomoabomoa hiyo.