Zaidi ya nyumba 75, zimeezuliwa mabati na nyingine kuta kubomoka baada ya upepo mkali kuvuma kwa takriban dakika kumi katika maeneo ya Wilaya ya Magharibi Mkoa wa Mjini Unguja.
Kamanda wa Polisi Mkoa Mjini Magharibi Unguja, Hassan Nassir Ali amesema tukio hilo limetokea leo (Jumatatu) saa 4.00 asubuhi ambapo upepo huo ulivuma.
Ali amesema miongoni mwa nyumba hizo ni kutoka Shehia tatu zilizomo wilayani humo, ikiwemo shehia ya Pangawe nyumba 30, shehia ya Kwerekwe nyumba moja na shehia ya kinuni nyumba 44.
Amesema kuwa hiyo ni tathmni ya awali iliyokusanywa na kikosi chake ila idadi hiyo huenda ikaongezeka.
“Hadi sasa tumepata nyumba 75, tu lakini tunaona ishara ya kuwepo kwa idadi zaidi kutokana na upepo huu kuonekana kuvuma maeneo mengi,”amesema
Kamanda huyo amesema mbali na athari za nyumba kuna mtu mmoja aliyefahamika kwa jina moja la Zaituni amepata majeraha baada ya kuangukiwa na matofali akiwa nyumbani kwao.
Amesema msichana huyo amepelekwa hospitali kwa ajili ya matibabu zaidi huku jitihada za kuokoa mali za wananchi walioathirika zikiendelea.
Makamo wa Pili wa Rais Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd amewajulia hali wananchi wa maeneo hayo na kutoa matumaini ya kushirikiana nao kwa pamoja katika wakati huo mgumu.