Meneja Udhibiti Ubora wa Makaa ya Mawe wa Kampuni ya Tancoal Energy Tanzania Limited Bw. Bosco Mabena akielezea moja ya majukumu wayafanyayo katika Kitengo cha Udhibiti Ubora wa makaa ya mawe yanayochimbwa kutoka mgodi wa makaa hayo uliopo Ngaka, Wilayani Mbinga Mkoani Ruvuma 10 Mei, 2017.
Baadhi ya Malori katika eneo la Kitai Wilayani Mbinga, Mkoani Ruvuma yakiwa yamepakiwa makaa ya mawe yakifungwa maturubai kwa ajili ya kuzuia makaa ya mawe hayo kunyeshewa na mvua ikiwemo kuchafuliwa na aina yoyote ya uchafu wakati wa kuyasafirisha makaa hayo 10 Mei, 2017.
Lori lililopakia makaa ya mawe katika eneo la Kitai Wilayani Mbinga, Mkoani Ruvuma likipimwa uzito kabla ya kwenda kufungwa turubai tayari kwa kuanza safari ya kupeleka makaa hayo kwa mteja wake, 10 Mei, 2017.
Naibu Meneja wa Mgodi wa Kampuni ya Tancoal Energy Limited (wa pili kulia) Bw. Edward Mwanga, Meneja Udhibiti Ubora wa Makaa ya Mawe wa Kampuni ya Tancoal Energy Tanzania Limited Bw. Bosco Mabena (wa pili kushoto), Afisa Mauzo na Usafirishaji wa Kampuni ya Tancoal Energy Tanzania Limited, Bi. Leahkissa Mwangosi pamoja na Meneja Mawasiliano Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) (kulia) wakielekea katika eneo la mzani wa kupimia malori katika eneo la Kitai Wilayani Mbinga, Mkoani Ruvuma 10 Mei, 2017.
Na Mwandishi Wetu
KAMPUNI ya kuzalisha makaa ya mawe nchini, Tancoal Energy Limited imetekeleza kwa zaidi ya asilimia 100 agizo la Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa ya kuongeza uzalishaji wa makaa ya mawe maradufu.
Taarifa hiyo iliyotolewa jana na Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo, Bw. James Shedd wakati alipokutana na Waandishi wa habari waliotembelea mgodi huo uliopo eneo la Ngaka katika wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma.
Bw. Shedd amesema kwamba, kampuni yake kwa sasa inazalisha kiasi kikubwa cha makaa ya mawe kukidhi mahitaji ya soko la ndani ya tani 60,000 kwa mwezi na ziada ya tani nyingine 20,000 ambazo pia zinauzwa katika nchi za Uganda, Kenya na Rwanda.
“Kampuni yetu imeongeza uzalishaji wa makaa ya mawe kwa zaidi ya asilimia 100 na tayari magari yatumikayo katika ubebaji na uchimbaji wa makaa ya mawe yako njiani kufika huku katika eneo la mgodi ili kuzidi kuongeza uzalishaji na hatimaye tani za uzalishaji wa madini haya zitazidi kuongezeka”, alisema Bw. Shedd.
Kwa upande wake Naibu Meneja wa Mgodi wa Kampuni ya Tancoal Energy Tanzania Bw. Edward Mwanga ameeleza kuwa, kampuni ya Tancoal kwa sasa imeongeza magari yakiyofanya kazi toka 25 hadi 30 ambapo kwa sasa idadi hiyo imeongezeka hadi kufikia gari 67, na sambamba na ongezeko hilo wameongeza mizani ya kupimia magari ili pindi itokeapo ongezeko la magari ya kubeba makaa ya mawe mzani huo utumike kuyapima.
“Kazi yetu huku ni kupakia kutokana na oda ya wateja wetu na idadi ya gari zilizokuja na asubuhi huwa tunapewa taarifa ya gari zilizoko njiani na tunahakikisha kuwa ndani ya saa moja gari hizo ziwe zimepakia makaa yam awe na kuondoka, hivyo tumeongezaidaid ya magari na pia tumeboresha mizani na kupanua eneo”, alisema Mwanga.
Kuhusiana na changamoto zikizoikabili kampuni hiyo amesema kuwa mwanzo wamekuwa wakikabiliana na changamoto za ikiwemo uhaba wa vifaa, barabara, mvua pamoja suala la uagizaji wa makaa ya mawe toka kwa wateja ambapo kwa sasa changamoto hizo zimetatuliwa na hali ya ongezeko la uzalishaji wa madini hayo imeongezeka.
Kwa upande wake Meneja Udhibiti Ubora wa Makaa ya Mawe wa Kampuni ya Tancoal Energy Tanzania Limited Bw. Bosco Mabena amesema kwamba, katika mgodi wao kuna sehemu ya Maabara ya kisasa ambayo hutumika kuchukua sampuli za makaa ya mawe na kuzipeleka katika hatua mbalimbali ikiwemo mkaa ulipochimbwa, katika hatua ya processing na pia mkaa unapokwenda kwa wateja, hivyo maabara yetu hutumika kuchukua sampuli kwa kila gari ili kutunza rekodi.
Ameongeza kuwa mgodi wao una udhibiti mzuri wa makaa ya mawe kwasababu ili kuhakikisha kuwa mkaa wa mawe uko safi magari yote yanayofika katika eneo hilo yanakaguliwa ili kuhakikisha kuwa hayana uchafu wowote na shughuli ya ufungaji hufungwa na wataalam wao maalum ambao ufungaji wao hauwezi kuchafua mkaa huo kwakuwa taarifa za gari ikiwemo dreva wa gari na namba ya gari huchukuliwa ili pindi itakeapo taarifa ya uchafuzi wa mkaa inakuwa rahisi kutambua chanzo.
Naye Afisa Mauzo na Usafirishaji wa Kampuni ya Tancoal Energy Tanzania Limited, Bi. Leahkissa Mwangosi amesema kuwa, kwa sasa wanapokea oda toka Makao Makuu Dar es Salaam kwa Meneja Mauzo na Matangazo na oda hiyo inaeleza taarifa ya mteja hivyo usajili wa gari hufanyika na kisha gari pindi zifikapo zinapakiwa madini hayo.
Kwa kipindi walipokuwa na mzani mmoja waliweza kupakia gari 50 kwa mzani mmoja kwa wakati wa mchana na usiku gari 30 hadi 40 ambapo hiyo ni sawa na wastani wa tani 2,500 kwa siku.
“Kwa sasa pindi mizani ilipoongezeka ongezeko la upakiaji naamini utaongezeka hadi kufikia gari 75 kwa mchana, na kuanzia 40 hadi 50 kwa usiku kwakuwa bado tuna nafasi kubwa ya kufanya hivyo na pindi magari yatakapozidi kuongezeka basi tutatumia mizani yote miwili”, alisema Mwangosi.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Dkt. Binilinith Mahenge ametaja baadhi ya changamoto zilizoikabili Kampuni ya Tancoal na namna jinsi Kampuni hiyo ilivyotekeleza agizo la Serikali ambapo amekiri kuwa kwa sasa kampuni hiyo inafanya vizuri katika kuhakikisha kuwa madini hayo yanazalishwa kufikia malengo yaliyoagizwa na Serikali.
“Tancoal walikua na changamoto ikiwemo ubovu wa barabara, uhaba wa vifaa vya uchimbaji makaa lakini kwa sasa wamejitahidi kuzitatua changamoto hizo na mimi mwenyewe nimekwenda kukagua na kujionea baadhi ya vifaa walivyoongeza na ninaamini zile tani elfu 60 kwa mwezi watazifikia”, alisema Dkt. Mahenge.
Mhandisi Migodi toka Ofisi ya Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Ziwa Nyasa, Godfrey Wandibha anaeleza kuhusu suala la bei ya makaa yam awe na suala la agizo la Mhe. Rais la kumpatia mmiliki wa kampuni ya Dangote eneo la kuchimba madini hayo ambapo amesema kwamba, tayari alishapatiwa leseni kwa ajili ya kuanza kuchimba.
“Dangote yeye kwa sasa anatakiwa kukaa na mtu ambaye alikuwa mwenye lile eneo ili kukubaliana baadhi ya mambo ambayo ni ya kawaida ili akishayakamilisha aanze uchimbaji lakini suala la kupewa eneo tayari lilishakamilika kama Rais alivyokuwa ameagiza”, alisema Wandibha.
Awali agizo la Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa alilitoa mapema Januari 6, 2017 mara baada ya kupokea taarifa na kutembelea katika mgodi wa Ngaka ili kuona shughuli za uzalishaji katika eneo hilo.
Aidha, Waziri Mkuu aliitaka kampuni hiyo ya TANCOAL Energy kutimiza masharti ya mkataba iliouingia na Serikali mwaka 2008.
Kampuni ya TANCOAL iliundwa Aprili 3, 2008 na kampuni tanzu ya Atomic Resources Limited, ambayo wakati huo ilikuwa ikijulikana kama Pacific Corporation East Africa (PCEA) na kwa sasa inaitwa Intra Energy (T) Limited, ambayo hisa zake ni asilimia 70 na Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) lenye asilimia 30 ya hisa.
Mgodi wa Ngaka uko wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma na unamilikiwa na kampuni ya TANCOAL kwa ubia baina ya NDC na kampuni ya Intra Energy Corporation ya Australia.