Wabunge wawili waliokuwa mawaziri katika Serikali ya Awamu ya Tano, Nape Nnauye (Mtama) na Charles Kitwanga (Misungwi) jana waligeuziwa kibao, wakidaiwa kukiuka maadili ya uongozi baada ya kuzungumza kwa hisia dhidi ya bajeti ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji.
Nape alikuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kabla ya kuachwa katika mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri, wakati uteuzi wa Kitwanga ulitenguliwa baada ya kuingia bungeni akiwa amelewa.
Wawili hao juzi walizungumza kwa hisia kuhusu kiwango kidogo cha fedha kilichowekwa wakisema hakiwezi kutatua tatizo la maji katika maeneo yao; Kitwanga akisema yuko tayari kuhamasisha wananchi wake 10,000 kwenda kufunga bomba la maji linalopita eneo lake.
Nape , ambaye pia alionekana kuwa na hisia kali, alisema sera ya Tanzania ya viwanda haitawezekana kama suala la maji halitapewa kipaumbele na kutengewa fedha za kutosha.
Jana, mbunge wa Geita Vijijini (CCM), Joseph Kasheku, maarufu kwa jina la Msukuma, alisema wakati akichangia hoja ya bajeti hiyo kuwa kauli za wawili hao zinaonyesha kuwa kuna haja ya kazi ya uhakiki kufanyika pia kwa mawaziri.
“Kazi zilizoahidiwa katika Ilani ni nyingi si moja. Hizi hela ni nyingi tuunge mkono na wala tusiwasumbue kwa kuzikataa. Tuwape nafasi ili wakafanye kazi,” alisema Msukuma.
“Lakini suala langu, nataka kuwazungumzia wana-CCM wenzangu ambao jana nilisikiliza mchango wa mmoja, Kitwanga analalamika anasema atawamobilize (atawashawishi) wananchi 10,000 wakazime mashine ya maji Iherere.
“Nataka niwaulize nyinyi mawaziri wa Magufuli hivi vile viapo mnavyokula mnajua maana yake? Kama hamvijui basi sina hakika kama mko sawasawa na kama hamko sawasawa, (Waziri wa Elimu, Joyce) Ndalichako hebu pitisha operesheni ya vyeti feki, huenda hapa penyewe kuna feki za kutosha.”
Alihoji sababu za mtu aliyekuwa waziri kusimama bungeni na kusema kuwa alivyokuwa waziri alibanwa kuzungumza.
“Kwahiyo sisi mambo (ambayo) hatuzungumzi kwa kuwasaidia nyinyi tumebanwa na nani? Mnasimama mnasema sasa nazungumza na nakwenda kuwahamsisha wananchi 10,000 wakazime mtambo?” alihoji.
“Hebu ngoja niwakumbushe tukio la mwaka 2014. Wakati Mheshimiwa Kitwanga akiwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini, alikuja Geita . Mimi kama mwenyekiti wa CCM wa mkoa nikawaambia wananchi wasitoke mpaka walipwe na mzungu, yeye akaja akamwambia mkuu wa mkoa hata kama kuna mwenyekiti wapigwe mabomu na kweli kesho yake tulipigwa mabomu.
“Kwa hiyo nataka nimwambie Waziri wa Mambo ya Ndani siku akienda kuunganisha wananchi palepale Misungwi naye apigwe mabomu aonje joto ya jiwe. Haiwezekani waziri uliyekula kiapo, ukitimuliwa unakuja humu kutuchanganya, wakati hatujui mambo mliyokuwa mnazungumza kwenye cabinet (baraza la mawaziri).”
Baadaye alimgeukia Nape.
“Nape ambaye alikuwa mwenezi wangu wa (CCM) Taifa, jana (juzi) alizungumza mambo mazuri lakini kuna moja alisema ‘tusipowatekelezea suala la maji wananchi hawataturudisha tena madarakani’.”
Alisema hilo haliwezekani kwa sababu wananchi wanawategemea kwa mambo mengi na si maji pekee yake na wamewafanyia vizuri.
Alisema ilani hazijaanza kuandikwa katika Serikali ya Awamu ya Tano na suala si kumaliza ahadi zote.
Awali alimpongeza Rais John Magufuli na wizara hiyo kwa kazi aliyoiita kuwa nzuri, akisema ameona mabadiliko makubwa. “Mimi niko tofauti kidogo na wabunge wenzangu wanaosema tusipitishe bajeti kwa sababu hela ni ndogo. Binafsi naona hizi hela ni nyingi sana, tatizo ni zitoke zote tofauti na bajeti ya mwaka jana.”