Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza kuwepo kwa nafasi wazi ya Mbunge wa Viti Maalum kwa tiketi ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo – CHADEMA, kufuatia kifo cha Mbunge wa Viti Maalum wa chama hicho Mhe. Dr. Elly Marko Macha aliyefariki tarehe 31 Machi 2017.
Akitoa taarifa ya nafasi hiyo kuwa wazi Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji wa Rufaa Mhe. Semistocles Kaijage amesema kuwa kwa mujibu wa Kifungu cha 37 (3) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343, Mhe. Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameijulisha Tume juu ya kuwepo kwa nafasi wazi ya Mbunge huyo.
Amesema taratibu za kujaza nafasi hiyo zinaendelea kwa kuzingatia Ibara ya 78 (4) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ikisomwa pamoja na kifungu cha 86A (8) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343.