TAARIFA KWA UMMA
KUKOMA KUWA KIONGOZI KWA MWENYEKITI WA WILAYA YA MONDULI MCHUNGAJI AMANI SILANGA MOLLEL
Kwa niaba ya baraza la uongozi la mkoa wa Arusha, napenda kuujulisha umma wote kwa ujumla kuwa mwenyekiti wa wilaya ya monduli Mchungaji Amani Silanga Mollel amekoma/amesimamishwa kuwa Mwenyekiti wa CHADEMA wilaya ya monduli kuanzia tarehe 29 Novemba 2013 kufuatia tuhuma nzito za uvunjifu wa kanuni za maadili ya chama.
Hatua hii imefikiwa baada ya kuthibitika na yeyé mwenyewe kukiri mbele ya kikao cha kamati tendaji ya wilaya ya monduli kilichoketi tarehe 29 Novemba 2913 saa NNE asubuhi kuwa alitoa tamko batili akitumia wadhifa wa mwenyekiti wa wilaya bila ridhaa ya kamati tendaji na huku akidanganya kuwa ni tamko kwa niaba ya wilaya ya Monduli.
Katika tamko lake ametoa tuhuma dhidi ya wajumbe wa kamati kuu na viongozi wakuu wa kitaifa kwa maamuzi halali ya kikao cha kamati kuu huku akijua kuwa anavunja kanuni za chama kwa mujibu wa katiba ya chama toleo la mwaka 2006 ya Kanuni za uendeshaji kazi za chama, sura ya KUMI, ibara ya 10 (X) “Kiongozi asitoe tuhuma zozote juu ya viongozi wenzake pasipo kupitia vikao halali na kuzingatia taratibu na ngazi zilizoelezwa kwenye kanuni za chama”.
Sambamba na hilo, Mchungaji Amani Silanga ametoa tuhuma za uzushi, uongo na upotoshaji na kutaka kuaminisha jamii kuwa chadema ina makundi ya CHADEMA Asili na CHADEMA Family kitu ambacho ni upotoshaji mkubwa na wa hatari kwa ustawi na umoja wa chama na kinyume na kanuni za uendeshaji kazi za chama, sura ya KUMI, ibara ya 10 (VII), “Kiongozi anatakiwa kuwa mkweli na muwazi wakati wote hususani katika vikao halali na aachane na vikundi vya majungu, wadanganyifu (Rumour Mongers). Ni mwiko kwa kiongozi kujihusisha na upotoshaji wa maamuzi wa vikao halali”.
Kamati tendaji ya wilaya ilipomtaka aonyeshe CHADEMA asili ni kina nani na CHADEMA family ni kina nani alishindwa kutoa maelezo yoyote ya maana na kufikia hatua ya kutaka kuvuruga kikao kwa kuleta vijana wahuni wapatao 17 ndani ya kikao ambao wengi walijulikana kuwa sio WANACHADEMA. Katika utambulisho wake wa majigambo Mchungaji Amani SIlanga kwa kiburi na kejeli amejitambulisha na kukiri kuwa yeye yupo kambi ya Zito Kabwe na hakuna wa kumfanya kitu maana ni mjumbe wa baraza kuu la chama. Maneno yake yalidhihirisha kuwa Mchungaji Amani Silanga anashiriki mpango wa kuunda makundi yasiyo na tija ndani ya chama na hivyo kuwa kinyume na sura hiyo hiyo ya kumi ya kanuni za uendeshaji kazi za chama ibara ya 10 (IX), “Kiongozi asijihusishe au kushiriki na vikundi au vitendo vya kuchonganisha au kuzua migogoro ndani ya uongozi wa chama au wanachama wake”.
AZIMIO LA BARAZA LA UONGOZI LA MKOA WA ARUSHA:
Baraza la uongozi la mkoa lililoketi tarehe 29 Novemba 2013, limepokea mapendekezo ya kamati tendaji ya wilaya na kuzingatia hofu kubwa iliyoainishwa na kamati tendaji kufuatia matendo mengi yanayotia shaka ya uadilifu na uwezo wa kiuongozi wa Mchungaji Amani Silanga na hivyo baraza la uongozi la mkoa limeridhia kuwa amevunja kanuni za maadili ya chama sura ya KUMI ibara ya (VII) hadi (XII) na hivyo kupelekea ukomo wa yeye kuwa Mwenyekiti wa wilaya kuanzia tarehe 29 Novemba 2013. Baraza la mkoa likiwa mamlaka ya nidhamu kwa mujibu wa katiba ibara ya 6.3.6 (a) (iv) limemjulisha tuhuma zake na hatua hii stahiki iliyochukuliwa. Kwa vile Mchungaji Amani Silanga alikiri kosa hili mbele ya kamati tendaji ya wilaya bila kulijutia au kuomba msamaha, baraza la mkoa limechukua hatua hii stahiki kwa maslahi ya chama na kuwa uchunguzi zaidi utafanyika ili kufikia maamuzi makubwa zaidi ya tuhuma nyingi kwa mujibu wa kanuni za hatua za kinidhamu.
Baraza la uongozi la mkoa wa Arusha, linatoa onyo kwa wote ambao wapo katika mtandao huu mchafu, ama watoke wenyewe mapema maana hawatavumiliwa kamwe. Baraza la uongozi wa mkoa liliona kuwa Mchungaji Silanga amepotoka na hivyo yeyé kuendelea kuwepo ndani ya chama wakati wa uchunguzi wa tuhuma hizi nzito dhidi yake ni hatari zaidi kwa ustawi wa chama na hivyo baraza likaridhia kwa kuzingatia tafsiri ya katiba ya chama ibara ya 6.3.4 (c) wa yeyé kukoma uongozi na hivyo akae nje kwa muda na waliopotoka wenzake.
Amani Golugwa
Katibu wa CHADEMA – Mkoa wa Arusha.
(Kwa niaba ya Baraza la Uongozi la Mkoa wa Arusha)
Tarehe 30 Novemba 2013