Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, imesema itatoa hukumu ya kesi ya ujenzi wa jengo la ghorofa 18 lililojengwa jirani na Ikulu lililopo mtaa wa Chimala Kitalu cha 45 na 46, jijini Dar es Salaam inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Makumba Kimweri na mwenzake Januari 15, mwaka 2014.
Uamuzi huo ulitolewa jana na Hakimu Mkazi Sundi Fimbo, baada ya upande wa utetezi kufunga ushahidi wao.
Hakimu Fimbo alisema baada ya upande wa utetezi kufunga ushahidi wao, mahakama hiyo itatoa hukumu Januari, mwakani.
Kabla ya uamuzi huo, mshtakiwa wa pili aliyekuwa Msanifu Mkuu wake, Richard Maliyaga (55), alidai kuwa alipitisha kibali cha jengo baada ya kupata maelekezo ya serikali.
Alidai kuwa alishiriki mchakato wa ujenzi wa jengo hilo kama Mwenyekiti wa kamati ya kutoa vibali vya ujenzi iliyokuwa na watu sita akiwamo yeye.
“Kamati ilinitaka nitoe kibali cha ujenzi huo baada ya kupokea maelekezo ya serikali …kabla ya kutoa vibali kamati yetu ilikuwa inapitia michoro na kama haina mapungufu tulikuwa tunaridhia kibali kutolewa kwa ajili ya ujenzi kufanyika,” alidai Maliyaga.
Alidai kuwa watu wote waliohusika kwenye mchakato wa ujenzi wa jengo hilo, hawajaburuzwa mahakamani na kwamba kesi hiyo inawakabili watu wawili huku wenzao wakipeta mtaani.
“Mimi naona nimeonewa tu kwenye kesi hii, sijanufaika na chochote katika mradi wa ujenzi wa jengo hilo na kwamba sikutumia madaraka yangu vibaya,” alidai mshtakiwa huyo wakati akifunga utetezi wake.
Katika kesi ya msingi, Kimweri na Maliyaga wanakabiliwa na mashitaka matano ya matumizi mabaya ya ofisi katika utoaji kibali cha ujenzi wa jengo la ghorofa 15 kiwanja namba 45 mtaa wa Chimara.
Ilidaiwa kuwa Kimweri alikuwa na wadhifa huo TBA kuanzia mwaka 2002 hadi 2010 na Maliyaga aliajiriwa mwaka 2002 akiwa Msanifu Mkuu.
Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai, alidai kiwanja hicho kilikuwa kinamilikiwa na TBA, ambako hadi mwaka 2006 kilikuwa hakijaendelezwa.
Aidha,TBA kwa mujibu wa Sheria ya Ununuzi wa Umma, iliwaalika wanaotaka kuwekeza kuwasilisha andiko la awali kwa ajili ya uendelezaji.
CHANZO: NIPASHE