Quantcast
Channel: PAMOJA BLOG
Viewing all articles
Browse latest Browse all 16395

WATANZANIA WAWILI WANASWA NA KILO 55 ZA DAWA ZA KULEVYA AFRIKA KUSINI

$
0
0
Kamanda wa Kikosi cha Kuzuia Dawa za Kulevya, Godfrey Nzowa (katikati) akiangalia dawa za kulevya aina ya heroine zilizokamatwa nchini, zikifunguliwa na afisa wa jeshi la polisi Neema Mwakagendi kabla ya kuteketezwa jana, katika tanuri la Kiwanda cha Saruji wazo jijini Dar es Salaam.Dawa aina mbalimbali zilizokamatwa ziliteketezwa. Picha na Juliana Malondo 
Johannesburg/Dar. Watanzania wawili wanahojiwa na Polisi wa Afrika Kusini baada ya kukamatwa jana na kilo 55 za dawa za kulevya.
Watu hao wawili wanatazamiwa kufikishwa mahakamani kesho kujibu tuhuma za kukamatwa na dawa hizo zenye thamani ya Rand75 milioni (Sh11.7 bilioni).
Maofisa wa Kikosi Maalumu cha Kupambana na Makosa ya Jinai na Rushwa cha Afrika Kusini (The Hawks), kiliwakamata watu hao katika Kitongoji cha Kempton Park, Ekurhuleni, Jimbo la Gauteng.
Msemaji wa Hawks, Paul Ramaloko alisema jana kuwa maofisa hao walivamia nyumba waliyokuwa wanaishi Watanzania hao na kukuta mzigo huo.
Hata hivyo, alikataa kutaja majina ya watu hao kwa kuhofia kuharibu uchunguzi akisema bado walikuwa wanawasaka watuhumiwa zaidi wakiwamo raia wa Afrika Kusini.
Alisema kikosi chao kimepata mafanikio makubwa kwa kukamata dawa nyingi kiasi hicho... “Tunakaribia kuwakamata vinara wa biashara hiyo, maana tumeelezwa kuna kundi kubwa la watu wazito,” alisema Ramaloko. Hii inakuwa mara ya pili katika kipindi cha miezi minne kwa Watanzania kutuhumiwa kubeba dawa hizo.
Julai mwaka huu, wasanii wawili Agness Gerald `Masogange’ na Melissa Edward walikamatwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Oliver Tambo, Johannesburg wakiwa na kilo 180 za kemikali aina ya ephedrine zenye thamani ya Sh7 bilioni.
Baada ya kukaa miezi miwili jela, Masogange alipatikana na hatia ya kuingiza kemikali hiyo, ambayo hutumika kutengeneza dawa za kulevya na kutozwa faini ya Rand 15,000 (Sh2.3 milioni).
Melissa aliachiwa huru baada ya kuonekana hana hatia.
Wasafirishaji sasa watumia samaki
Katika hatua nyingine, wasafirishaji wa dawa za kulevya inasemekana wamebuni mbinu mpya ya kutumia samaki kusafirisha bidhaa hiyo haramu.


Akizungumza jana wakati wa uteketezaji wa dawa za kulevya, Mkuu wa Kitengo cha Kudhibiti Dawa za Kulevya, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Godfrey Nzowa alisema wanatumia samaki kwa kuwa wana harufu kali.
Alisema harufu hiyo huwafanya mbwa waliopewa mafunzo ya kutambua dawa hizo kushindwa kuzigundua.
“Tumebaini kwamba siku hizi wanaweka dawa hizo chini kwenye mizigo yao na kisha kuweka samaki hao juu hata mbwa akinusa vipi hawezi kuambulia kitu,” alisema Nzowa.
Alisema wengine hutumia mboga aina ya kabichi kwa usafirishaji wa bangi. Alisema hutanguliza bangi kwenye magunia na juu yake kuweka kabichi.
Pia alisema changamoto nyingine katika vita hiyo ni baadhi ya wasafirishaji wa dawa hizo kusafirisha malighafi (vibashirifu) ya kutengeneza dawa hizo.
Dawa zilizoteketezwa jana katika tanuri la Kiwanda cha Kutengenezea Saruji cha Twiga, Wazo Hill, Dar es Salaam, zilikuwa kilo 702 za bangi, kilo 12 za heroine, kilo tano za cocaine na kilo 105 za kuberi.
MWANANCHI

Viewing all articles
Browse latest Browse all 16395

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>