Quantcast
Channel: PAMOJA BLOG
Viewing all articles
Browse latest Browse all 16395

POSHO ZAUNDIWA KAMATI DODOMA

$
0
0
 
 Mwenyekiti wa muda wa Bunge la Katiba, Ameir Pandu Kificho.

Wakati  Mwenyekiti wa muda wa Bunge la Katiba, Ameir Pandu Kificho, akiunda timu ya wajumbe sita kushughulikia malalamiko ya wabunge wa Bunge hilo kuhusu kulipwa posho ndogo, watu wa kada mbalimbali nchini wamepinga madai hayo.

 Kificho jana aliunda kamati ya uongozi ya wajumbe sita itakayoshughulikia malalamiko ya posho ya wajumbe na kuliwasilisha suala hilo serikalini lifanyiwe kazi haraka.

Kificho alisema iwapo suala hilo litashughulikiwa litasaidia wajumbe wa bunge hilo waishi vizuri ili kazi nzito waliyonayo ifanyike vema.

“Jana (juzi), nilisema kwamba hili ni jambo ambalo tunalichukua kulifanyia kazi…sasa na bado halina majibu ila nina majibu ya kufanya kazi pamoja na timu ambayo tutakaa pamoja kama kamati ya uongozi ili tuzingatie kwa makini suala hili na kuiomba serikali ione uwezekano wa kuweka jambo hili vizuri ili tufanye kazi kwa umakini.

ENDELEA KUSOMA HABARI HII KWA KUBOFYA HAPA CHINI
“Sasa niombe waheshimiwa wajumbe…nimeshauriwa niteue kamati ya uongozi kuzingatia jambo hili kiundani na kama kutakuwa na jambo lingine kamati hiyo hiyo ya uongozi ndiyo itakayosaidia kutoa mashauri na hatimaye kuomba serikali tupate majibu yatakayosaidia,” alisema.  

WAJUMBE WA KAMATI

Aliwataja wabunge watakaounda kamati hiyo kuwa ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge) William Lukuvi; Waziri Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais (Zanzibar), Mohammed Aboud Mohamed na Freeman Mbowe.

Wengine ni Paul Kimiti, Asha Bakari Makame na Naibu Waziri Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Jenista Mhagama.

Juzi wakati wa semina ya kukabidhiwa rasimu ya kanuni za Bunge Maalum la Katiba na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, baadhi ya wajumbe waliibua hoja ya kutaka nyongeza ya posho kwa kuwa kiasi cha Sh. 300,000 wanacholipwa hakitoshelezi mahitaji.

Walisema wamepata taarifa kuwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, wanalipwa Sh. 420,000 kwa siku na kuwashangaza kuwa Bunge moja posho tofauti.

WANANCHI WAPINGA
Makundi mbalimbali ya jamii yamelalamikia hatua ya wajumbe wa Bunge hilo kulalamkia posho ya Sh. 300,000 kwa siku kuwa haitoshi.

DK. SLAA: WABINAFSI
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, alisema wajumbe hao kudai posho ni ubinafsi, kwa sababu kiasi wanachopewa kwa siku moja ni zaidi ya kiwango cha chini cha mshahara wa mtu mmoja. 

Pia alisema ni jambo la kushangaza wabunge hao kuacha kujadili Katiba iliyowapeleka ambayo ni mstakabali wa taifa wanakimbilia kudai posho.

“Nimepata mshtuko kuona eti mtu badala ya kujadili kilichompeleka,  suala nyeti la mstakabali wa nchi, eti anadai posho, hivi wananchi waliwatuma kudai posho au kuwapatia Katiba,” alihoji Dk. Slaa na kuongeza:

“Tunajua wanahitaji kupewa fedha kwa ajili ya kujikimu katika mahitaji yao muhimu, lakini ni vema wakaweka maslahi ya taifa na wananchi waliowatuma mbele na wakiendelea kufanya hivyo wananchi wao waliowatuma watawadai.”

Pia, alivitaka vyombo vya habari kupuuza kuripoti mambo ambayo hayana mantiki katika bunge hilo, badala yake waripoti hoja za msingi zenye manufaa kwa taifa.

Dk. BANA: ANENA
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Benson Bana, alisema wajumbe hao wameonyesha picha ambayo haikutarajiwa na Watanzania, kwamba wangejikita zaidi kujadili hoja nzito za kuwapatia Katiba bora na si kwa ajili ya maslahi yao binafsi ya kupunguza wimbi la umaskini katika maisha yao.

Alisema suala la wajumbe kudai posho haliingii akilini na kama walitarajia Bunge la Katiba wajikwamue na wimbi la umaskini ni bora wangejiengua mapema ili kuwapa nafasi watu wengine wenye nia njema na nchi yao.

“Jambo nyeti ambalo liliwapeleka wajumbe Bungeni ni Katiba ya Watanzania, fedha wanayolipwa ni nyingi sana, ambayo huwezi kulinganisha na mshahara wa Mtanzania wa kawaida.  Ina maana  Mwanajeshi akitumwa vitani atasema siendi bila posho, hii siyo hulka ya Watanzania,” alisema.

SHIVJI AWASHANGAA
Mhadhiri mstaafu wa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Issa Shivji, alisema kiasi wanachopewa wajumbe ndicho hicho kilichotengwa na hakiingiliani na mshahara wa mtu.

“Bunge hili ni maalum na kila mjumbe anapewa kile kilichotengwa, posho ni posho na mshahara ni mshahara haviingiliani,” alisema.

TGNP YASIKITIKA
Kaimu Mkurugenzi wa Mtandao wa Kijinsia Tanzania (TGNP), Lilian Liundi,  alisema wamepokea kwa masikitiko kitendo hicho cha wabunge kudai posho badala ya kusimamia kile kilichowapeleka.

Alisema wapo Watanzania ambao mishahara yao kwa mwezi haifikii hata nusu ya kiwango cha fedha wanachopata wajumbe hao kwa siku, lakini wanaendelea kufanya kazi bila kulalamika.

Aliongeza kuwa wabunge hao wameonyesha dhahiri kwamba lengo lao lilikuwa ni kwa maslahi yao na si ya wale waliowatuma katika Bunge hilo.

ZITTO, KESSY, NATSE WAPINGA

Baadhi ya ya wajumbe wa Bunge hilo wamemtaka Rais Jakaya Kikwete, kutokubali kuidhinisha malalamiko ya posho ya wajumbe hao.

Zitto Kabwe alisema kuwa posho ambazo zinatolewa sasa hivi zinatosha kwani hali ya wananchi kwa sasa ni mbaya.

“Hatuwezi sisi kutumia fursa zetu za ushawishi wa kisiasa kutaka kufaidika zaidi kwa sababu gharama za posho na nyongeza ambazo wajumbe wanataka katika hali ya uchumi wa sasa na ukiangalia hali ya kima cha chini cha mwananchi haielezeki kabisa,” alisema.

“Hiki kiwango kinatosha, kwanza ni kikubwa kwa sababu posho ya kikao sasa hivi imefika 220,000 ilikuwa 70,000…kwa hiyo kwa siku mjumbe anachukua 300,000 mimi naona inatosha,” aliongeza.

Ally Kessy, alisema anashangaa kuona wajumbe wa Bunge hilo wanapolilia kuongezwa posho wakati wananchi wao vijijini wanakufa njaa.

“Kwani kima cha chini kwa wafanyakazi wetu ni kiasi gani hadi sisi tulilie kupewa fedha zaidi…mbona wao wanaishi kwa kiasi hicho hicho cha fedha wanacholipwa na wanaendelea kuishi… kwa nini sisi hatuna huruma?,” Alihoji.

Naye Mbunge wa Karatu, Mchungaji Israel Natse, alisema: “Hatuwezi kutanguliza posho kwa kazi ambayo tunawafanyia wananchi wetu na taifa kwa ujumla.

“Hata wananchi wanataka kuona viongozi wao wanaishi maisha kama wanayoishi wenyewe na wala si ya kujilimbikizia fedha,” alisema.

Paulina Mziray, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mwenge (Mwuce), alisema ni fedheha kwa wajumbe wabunge hilo kutanguliza ubinafsi kwa kutaka kiasi kikubwa cha posho na fedha za kujikimu wakati kuna wananchi wanapoteza maisha kila siku kwa kukosa dawa katika vituo vya afya, zahanati na hospitali zilizopo katika maeneo wanayotoka.

Genoveva Mkala, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Tiba na Afya  cha KCMC, alisema jamii ya Watanzania bila ya kujali maeneo wanayotoka, itakuwa tayari kuruhusu serikali kuongeza stahili

wanazotaka wajumbe hao iwapo tu kila mbunge ataorodhesha ni wanafunzi wangapi katika eneo lake wamekosa ada na nafasi ya kujiunga na vyuo vya elimu ya juu, lakini pia ni wangapi ambao wanakaa chini kwa kukosa madawati.

Abdallah Issa Jumaa, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Biashara na Ushirika (Muccobs), alisema wajumbe wanaolalamika wakitaka nyongeza hiyo wawakumbuke wananchi wao ambao hivi sasa katika maeneo mbalimbali wanaripotiwa kukosa makazi na chakula kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha kuharibu vibaya nyumba zao na mazao ya chakula.

Mwalimu wa Shule ya Msingi Meru mkoani Arusha, ambaye jina lake hakutaka litajwe, alisema kama wao wanapokea Sh. 240,000 tena kwa mwezi , anawashangaa wanaokataa Sh. 300,000 kwa siku.

Anthony John, alisema haoni sababu ya kupinga fedha hiyo wakati ni nyingi sana. “Tena wanapata kwa siku Sh. 300,000 ambazo sisi hatuzipati hata tukifanya kwa mwezi,,” alisema.

Rubungira Rumagiliza kutoka Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), alisema wajumbe badala ya kuwakilisha wananchi, wanajiwakilisha wao wenyewe kwa maslahi yao na familia zao.

Alisema kuwa ni vyema ingewekwa sheria katika Katiba mpya kuwa ubunge siyo biashara bali ni uwakilishi wa wananchi kwa kupigania maslahi yao.

Paul Loisulie wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), alisema  anapinga wajumbe hao kuongezwa posho kwa madai kuwa hawatendi haki na hawapo sahihi.

“Hiyo laki tatu inawatosha kwa sababu hoteli kubwa kwa hapa Dodoma ni laki moja hata ukila namna gani haiwezi kuzidi laki moja, nawaomba wawe wazalendo na nchi yao hata hivyo, wamezoea kila wakitaja chochote wanakipata na Watanzania hawalalamiki, wametuona ni wapole,” alisema Loisulie.

 Kwa upande wake, Eva Mpagama, alisema ikiwa posho hizo wanaziona ni ndogo na hazitoshelezi kujikimu kulingana na maisha, wanaweza kuachia ngazi na wakabaki wale wenye wito wa kuwakilisha mapendekezo waliyotumwa na wananchi.

Naye John Ntandu, alisema wajumbe hao kitendo cha kutaka wapatiwe Ipad ni muhimu wafahamu kuwa ndani yao kuna kundi la wajumbe wenye ulemavu wa kutoona ambao hata kama watapatiwa anaamini kuwa haitawasaidia chochote.

 Katibu wa Mkuu wa Umoja wa Madhehebu ya Kikristo Dodoma, Dk. Askofu Eliah Mauza, alisema wajumbe wanaolilia posho wapo kimaslahi yao zaidi na wameingia katika Bunge hilo ili wakamilishe miradi yao.

JUKATA YALAANI
Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), limelaani madai ya baadhi ya wabunge kutaka nyongeza.

Mwenyekiti wa Jukata, Deus Kibamba, alisema kitendo wanachoonyesha wabunge hao kwa kutanguliza maslahi yao binafsi, ni kwenda kinyume na kile walichotumwa na wananchi kuwawakilisha.

“Hii si hali ya kawaida ni ubinafsi na tamaa, badala ya wabunge kujadili masuala ya kitaifa kwanza wanataka posho zaidi. Kuna wafanyakazi katika nchi hii ambao wanalipwa mshahara mdogo wa chini ya Sh. 300, 000 kwa mwezi wao wanataka walipwe Sh. 420,000 kwa siku,” alisema Kibamba.

Imeandikwa na Elizabeth Zaya, Christina Mwakangale Dar; Godfrey Mushi, Moshi, Agusta Njoji,  Jacqueline Massano, Peter Mkwavila , Dodoma; Cynthia Mwilolezi, Arusha na Furaha Eliab, Mbeya.
 
CHANZO: NIPASHE

Viewing all articles
Browse latest Browse all 16395

Trending Articles