Kuna mambo huwa tunajaribu kuyafanya kazini kwa kujaribu kupuuzia au kufikiri kwamba mtu mwingine atafanya. Ni moja ya vitu nilivyokutana navyo leo nilipokuwa nikiongea na mfanyakazi mmoja (Fatuma) ya kampuni fulani hapa mjini.
Fatuma anasimulia kisa chake cha mfanyakazi mwenzake (Joyce) aliyeagizwa kufanya kazi fulani siku moja nyuma. Joyce hakuifanya ile kazi kisa akiamini inawezekana Fatuma ataifanya. Tukio hilo likasababisha kukasirika kwa Fatuma siku inayofuata, Joyce anaposema alidhani na yeye (Fatuma) alipewa maagizo ya kuifanya.
Habari ya Fatuma na Joyce ni moja ya vitu tunavyokutana navyo makazini mwetu kwa namna moja ama nyingine, na chanzo chake ni Uvivu wa watu kutopenda kufanya kazi kisa kwenye idara yao wapo zaidi ya wawili. Jaribu kufikiri nini kitatokea kama hiyo kazi ilikuwa ni ya mteja wa kampuni? Kuna uwezekano wa kupoteza huyo mteja na kampuni kuzorota kimapato kwa uvivu wa namna hiyo.
Kabla ya kufanya kazi au kutokufanya kazi jaribu kuuliza kama kazi hiyo ina uharaka kiasi gani na kama una mambo mengi je yawEzekana kufanya siku inayofuata? Hiyo itapunguza migongano isiyo ya lazima kazini kati ya wafanyakazi wenzako na bosi wako.
ENDELEA KUSOMA HABARI HII KWA KUBOFYA HAPA CHINI
Uvivu hautokani tu na kutokufanya jambo , bali ni hulka ambayo iko katika maisha ya mtu hivyo hukosa fikra endelevu katika kujua madhara ya yeye kutofanya kitu fulani. Uvivu unasababisha biashara nyingi kutokuwa na ubunifu kwa sababu watu wanafanya vitu kama walivyozoea, hawaweki bidii ya utendaji na kufikiri zaidi ili kuboresha wanachokifanya.
Unapokuwa na mtu kama Joyce unatakiwa kuwa na ushahidi wa kimaandishi kama barua pepe, memo endapo kazi aliyopewa na wewe ulikuwa unahusika. Utapunguza na kuboresha utendaji katika kitengo chako. Usiruhusu mtu aharibu taaluma au kazi yako kwa kisa cha uzembe na uvivu.
Zaidi ya yote, “Usichezee kazi ushindani ni mkubwa ” fanya kazi kwa juhudi na bidii. Nakutakia siku njema.
NB: Majina ya Fatuma na Joyce yametumika ili kufikisha ujumbe na sio ukweli kwamba tumemlenga mtu.