KAMPUNI ya Mwananchi Communication Ltd (MCL), imejitokeza kudhamini Tamasha la Utamaduni wilayani Handeni mkoani Tanga, linalotarajiwa kufanyika Desemba 14 katika Uwanja wa Azimio Handeni Mjini na kuhudhuriwa na watu mbalimbali.
Tamasha hilo linalojulikana pia kwa jina la Handeni Kwetu linafanyika kwa mara ya kwanza likiwa na shauku ya kutangaza utamaduni na fursa nyingine za kimaendeleo wilayani humo, kama sera ya kuwapatia maendeleo.
Akizungumza jana mjini hapa, Mratibu wa Tamasha hilo, Kambi Mbwana, alisema wamekubaliana na wenzao Mwananchi kwa ajili ya kuwezesha tamasha hilo. Alisema kitendo cha Mwananchi kuingia katika tamasha hilo ni kuonyesha ushirikiano mkubwa waliokuwa nao katika jamii ya Kitanzania.
“Wakati naandaa tamasha hili sehemu mbalimbali niliweza kuingia kwa ajili ya kusaidiana na wadau juu ya Tamasha la Handeni linalofanyika kwa mara ya kwanza, huku likijiweka katika nafasi nzuri mno.
Tunashukuru kwa wale walioguswa na kujitokeza kwa namna moja ama nyingine, ukizingatia kuwa Kampuni kama Mwananchi kuingia ni cha kuungwa mkono na Watanzania wote kwa ajili ya kuhakikisha kuwa mambo yanakuwa mazuri,” alisema Mbwana.
Kuelekea kwa tamasha hilo, vikundi mbambali vimeonyesha kuliunga mkono tamasha hilo litakalowaunganisha Watanzania wote, hususan wakazi wa wilaya ya Handeni, mkoani Tanga na Tanzania kwa ujumla.
Wadhamini wengine ni Phed Trans, Clouds Media Group, Grace Products, Screen Masters na mtandao wao wa Saluti5.com, Dullah Tiles & Construction Ltd, Katomu Solar Specialist, PLAN B SOLUTIONS (T) LTD, Country Business Directory (CBD) na Michuzi Media Group duka la mavazi la Chichi Local Ware, Smart Mind & Arters chini ya Anesa Company Ltd, ikidhamini kwa kupitia kitabu chao cha ‘Ni Wakati Wako wa Kung’aa’, Lukaza Blog, Kajunason Blog, Jiachie Blog na Taifa Letu.com, huku likipangwa kuanza saa 2 za asubuhi hadi saa 12 za jioni.