Vijana wafuasi wa Chadema wakipigana mahakamani kutetea makundi wanayounga mkono. Picha ya Mwaktaba.
Dar es Salaam. Mwamko wa vijana katika siasa ulianza kujitokeza katika kipindi cha uchaguzi wa mwaka 1995. Chama Cha Mapinduzi (CCM) mbali na mwamko wa vijana ulioibuka ndani yake, pia kilianza kupata upinzani mkali na kutupiwa lawama na kila aina ya kejeli kwa madai ya viongozi wake kukosa sifa za kuongoza nchi.
Mwamko huo kwa vijana umeendelea kukua kwa kasi mpaka sasa kupitia uhamasishaji wa makundi mbalimbali ya wanaharakati, wasomi na huo ukawa ni mwanzo wa baadhi ya vyama vya siasa kuona umuhimu wao, hivyo kila chama kuwavuta upande ke kwa maslahi yake.
Idadi kubwa kati ya vijana hao ni wahitimu wa vyuo mbalimbali na walioko vyuo vikuu ambao ni rahisi kupokea agenda za vyama husika na kuziendeleza, hivyo kutimiza malengo ya vyama husika.
ENDELEA KUSOMA HABARI HII KWA KUBOFYA HAPA CHINI
Pamoja na hao, wapo vijana wenye elimu ya wastani, na wengine walioikosa kabisa, ambao ni rahisi kufanya lolote bila kujali matokeo yake, kwa kuwa wao ni ‘bendera fuata upepo’.Kwa hali ya siasa ilivyo nchini, baadhi ya vijana wameanza kujikuta njiapanda, wakishindwa kuchagua ni chama gani, mwanasiasa yupi au kundi lipi linaweza kuwa tumaini jipya kwao.
Hatua hiyo inatokana na udhaifu unaoendelea kuonekana ndani ya vyama vya siasa, hususani vile vyenye ushindani mkubwa katika kipindi fulani – kama ilivyokuwa kwa NCCR na CCM mwaka 1995; CCM vs CUF mwaka 2000; na CCM vs Chadema mwaka 2010 na sasa tunapoelekea 2015.
Sote ni mashuhuda wa mivutano iliyopo, vurugu na tuhuma mbalimbali za mara kwa mara zisizokuwa na majibu.
Vuguvu hilo la vijana limeanza kuingia hata ndani ya vyama vyewenye, mfano ni katika uchaguzi wa Umoja wa Vijana wa CCM mwaka juzi, na hivi karibuni katika sakata la Chadema dhidi ya Zitto Kabwe.
Katika matukio hayo, tumeshuhudia jinsi vijana walivyoamua kupigana wao kwa wao, kila upande ukitaka kutimiza malengo yake.
Kutokana na mazingira hayo, wachambuzi wa masuala ya kisiasa nchini wanaeleza mitazamo mbalimbali inayosababisha vijana kuathiriwa na mapenzi ya vyama, au watu binafsi ndani ya vyama hivyo mpaka kufikia hatua ya kukosa uvumilivu, wakiamini kuwa chama hicho au watu hao ndio suluhisho la matatizo yao.
Vijana wanapotoka?
Tofauti na fikra za vijana hao, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Slaam (UDSM), Bashiru Ali anasema mpaka sasa haamini kama kuna chama chochote cha siasa duniani kilichowahi kuwa na historia ya kuleta mabadiliko ya kuikomboa jamii kuondokana na changamoto zinazoikabili.
Bashiru anasema kila chama kimekuwa na ajenda ya kuhakikisha kinashika dola pasipo kuangalia au kupigania mabadiliko katika huduma za kijamii.
“Vyama huwa na ajenda ambazo vinaona zitafaa kuwatengenezea mazingira ya kufanikisha itikadi zao. Mfano kodi za nyumba zimekuwa zikiongezeka kila wakati na hatujasikia chama hata kimoja kimesimama kulisemea, ni changamoto inayowagusa wananchi na maisha yao, kwani wanasiasa hawaoni?”
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya kiraia inayofuatilia mwenendo wa Bunge nchini (CPW), Marcossy Albanie anasema hatua ya vijana kupigana inatokana na hali tofauti na matumaini waliyokuwa nayo ndani ya chama.
“Wamewekeza kwa muda mrefu wakiamini ndiyo sehemu ya kuleta mapinduzi mapya ya kiutawala, sasa inapotokea mivutano kama tukio la Chadema, matokea yake wanakosa uvumilivu,” anasema na kuongeza;
Kina nani hawajitambui?
Katibu wa Hamasa na Chpikizi katika Umoja wa Vijana wa VCCM, Paul Makonda anasema bila kuangalia itikadi za vyama vya siasa, tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi mpaka sasa asilimia 75 ya vijana hawajatambua itikadi za kisiasa.
Anasema mbaya zaidi miongoni wasiojitambua ni wasomi wengi waliohitimu elimu za vyuo vikuu.
“Hawajui siasa, hawajui itikadi ni nini na hawajui hata wanachokitaka kupitia vyama vya siasa, ila picha iliyopo kwa sasa wamekuwa wakifuata ushabiki tu wa kisiasa na kuangalia mwanasiasa gani, kundi au chama gani kinachozungumzia hisia zao,” anasema Makonda.
Kiongozi huyo aongeza kuwa kundi jingine la vijana sawa na asilimia 25 ni lenye ujasiri lakini linaishi kwa hofu na woga, linakosa nguvu ya kuhoji udhaifu uliopo katika mfumo wa vyama kutokana na nguvu za wanasiasa wachache wanaotaka kulinda maslahi yao.
Anasema kutokana na mazingira hayo, mwasiasa amekuwa akitumia fimbo hiyo kama udhaifu wa kuendelea kumtumia kijana katika jambo lolote analohitaji kupenyeza maslahi yake kwa wakati fulani.
Makonda anasema mbaya zaidi mpaka sasa taifa halina mfumo wa kuwaandaa vijana katika uelewa wa itikadi za kisiasa ndani ya vyama.
“Kutokana na hali hiyo ukijumlisha na uvivu wa kufikiri hoja na maazimio ya wanasiasa, matokeo yake vijana wanapigana ovyo wao kwa wao au kuwa watumwa wa wanasiasa,” anasema Makonda.
Nini Kifanyike?
Bashiru anasema hatua ya kwanza katika kuwakomboa vijana hapa nchini ni pomoja na kuwasaidia waweze kufikiri na kuchambua kwa makini kila hoja inayotolewa na mwanasiasa yeyote.
Anasema uwezo wa vijana ujengeke mpaka kufikia hatua ya kutengeneza msimamo na ajenda zao kama vijana.
“Tunataka tuone vyama vya siasa ndiyo vinafuata ajenda za vijana, siyo vijana wanafuata ajenda za wanasiasa, matokeo yake wanajikuta kwenye mpasuko wa makundi,” anasema.
Bashiru anasema uelewa mdogo wa vijana katika kuchambua itikadi za kisiasa hapa nchini utaendelea kuwa changamoto mpaka pale vijana wanakapokuwa tayari kufanya mabadiliko.
“Vijana watengeneze vyama vyao kwa ajili ya kupigania maslahi yao, waunde vyama ambavyo vitakuwa na ajenda ambazo zitakuwa na ushawishi wa kutumiwa hata na hao wanasiasa, kama ambavyo tuliwahi kuwa na vyama vya wakulima, wafanyakazi, wafanyabiashara,” anasema Bashiru.
MWANANCHI