Maelfu ya abiria wamekwama katika barabara kuu ya Morogoro-Dodoma, na kulazimika kusitisha safari zao, baada ya mvua kubwa zilizonyesha usiku wa kuamkia siku ya Jumatano, kusababisha mafuriko makubwa yaliyofanya daraja la Magole, linalokatiza mto kikundi katika eneo la Dumila,kwenye barabara hiyo kukatika.
ITV imeshuhudia maji mengi yakiwa yameziba barabara kuu ya Morogoro-Dodoma, huku visiki vya miti vikiwa vimeziba barabara, na eneo la mto Kikundi unaomwaga maji mto wami, ukiwa umefurika na daraja la magole likiwa limebomoka kabisa na kusababisha watu kutoka upande mmoja kushindwa kuvuka kwenda upande mwingine,huku wananchi wa eneo hilo wakidai hii ni mara ya kwanza kwa mafuriko ya aina hiyo kutokea, yaliyosababisha mashamba na makazi ya watu kuharibika na hata daraja kubomoka.
Wananchi hao wameshauri wakala wa barabara nchini tanroads kuzingatia ubora katika ujenzi wa barabara na madaraja, huku meneja wa wakala huo mkoa wa Morogoro, injinia doroth mtenga, akizungumzia athari za uharibifu uliojitokeza, na naibu waziri wa uchukuzi, dk charles tzeba aliyebainisha vituo 11 vya reli navyo kuharibiwa kwa mvua,akiwashauri wananchi kukaa mbali na eneo hilo kutokana na daraja kuzidi kubomoka kadiri muda ulivyokuwa ukiendelea sambamba na magari kutumia njia nyingine mbadala kuendelea na safari.
ENDELEA KUSOMA HABARI HII KWA KUBOFYA HAPA CHINI
Baadhi ya wananchi wameiomba serikali kufanya jitihada za haraka, kuwanusuru wananchi waliokuwa mashambani na majumbani,walioweza kujiokoa kwa kupanda juu ya miti, na juu ya paa za nyumba,waliokuwa wamezingirwa na maji,ambapo mtendaji wa kijiji cha magole, amesema mafuriko hayo yameathiri zaidi ya nyumba 300, ofisi za serikali,shule na nyumba za ibada katika kijiji hicho, na mkuu wa mkoa wa Morogoro Joel Bendera akibainisha tayari wameomba msaada wa helikopta ya polisi kuwanusuru watu hao.
Kufuatia maafa hayo waziri wa nchi ofisi ya waziri mkuu sera na uratibu Mh. Wiliam Lukuvi amewataka wasafiri wote waliokwama kurudi walikotoka na kutumia njia mbadala kwani daraja hilo la dumila limeondoka kabisa. Amesema mafundi wa wakala wa barabara tanroads wapo eneo la tukio kujaribu kurejesha mawasiliano kazi ambayo inaweza kuchukua siku mbili au zaidi.
Ameshauri wanofanya safari kwenda Dodoma kupitia iringa au Arusha na wale waliokwama kurudi walikotoka.
ITV TANZANIA