Mgombea wa kiti cha urais wa shirikisho la mchezo wa soka duniani FIFA, Jerome Champagne, amependekeza kuanzishwa kwa mfumo wa kutoa kadi ya chungwa wakati wa mechi za soka, ili kuruhusu marefa wa mechi kuwaruhusu wachezaji waliofanya madhambi kuondolewa uwanjani kwa muda.
Champagne mwenye umri wa miaka 55 kutoka Ufaransa, aliyasema hayo siku ya Jumatatu wakati alipoanzisha kampeni yake ya kumrithi rais wa FIFA Sepp Blatter, kufuatia uchaguzi wa urais wa FIFA utakaofanyika mjini Zurich Juni mwakani 2015.
Amesema ikiwa atashinda atapendekeza vilabu vya soka kuadhibiwa ikiwa wachezaji wake watahoji maamuzi ya refa na vile vile kuchunguza uwezekano wa kutumia teknolojia kutatua maamuzi muhimu.
Miongoni mwa mapendekezo mengine aliyoyasema ni kuthibiti idadi ya wachezaji wa kigeni wanaosajiliwa na vilabu, kutangazwa kwa mshahara wa rais wa FIFA na maafisa wengine wakuu.
Aidha ameahidi kuwa atafutilia mbali sheria ya sasa inayotoa adhabu tatu kwa mchezaji ambaye atafanya madhambi katika eneo la hatari.
Kwa sheria ya sasa mchezaji yeyote anayefanya kosa katika eneo la hatari, hupewa kadi nyekundu moja kwa moja na pia kupigwa marufuku ya kutocheza mechi mbili zinazofuata.
Source:BBC