Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue
Ikulu yafanya uteuzi, kuhamisha Makatibu Tawala
Wamo Chambo, Dk. Ndunguru
Wamo Chambo, Dk. Ndunguru
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, leo anakutana na vyombo vya habari Ikulu jijini Dar es Salaam kwa kile kinachotarajiwa kutangazwa kwa mawaziri wapya.
Uwezekano huo unatokana na taarifa ya Ikulu iliyotolewa jana ikieleza kuwa Balozi Sefue ambaye pia ni Katibu wa Baraza la Mawaziri atazungumza na wanahabari katika kikao hicho kinachotarajiwa kufanyika wakati wowote leo.
“Katibu Mkuu Kiongozi na Mkuu wa Utumishi wa Umma, Balozi Ombeni Sefue ambaye ni Katibu wa Baraza la Mawaziri, leo, Jumapili, Januari 19, 2014, atazungumza na waandishi wa habari katika mkutano utakaofanyika Ikulu, Dar es Salaam.” Ilisema taarifa hiyo, iliyosainiwa na Mwandishi wa Rais, Salva Rweyemamu.
Matarajio ya wengi yalikuwa Rais Jakaya Kikwete angetangaza baraza la mawaziri wiki hii ili kuziba nafasi zilizoachwa wazi na mawaziri wanne walioshinikizwa na Bunge kujiuzulu, kufuatia kushindwa kusimamia majukumu yao kwenye Operesheni Tokomeza Ujangili iliyosababisha vifo na uharibifu wa mali za watu.
ENDELEA KUSOMA HABARI HII KWA KUBOFYA HAPA CHINI
Waliojiuzulu ni Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Mathayo David, Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki , Waziri wa Mambo ya Ndani Dk John Nchini, na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Shamsi Vuai Nahodha. Pia alitarajiwa kutangaza Waziri wa Fedha kuchukua nafasi ya marehemu Dk William Mgimwa, aliyeaga dunia Januari mosi mwaka huu.
Mwanzoni mwa mwezi huu kumekuwa na taarifa kwenye vyombo vya habari zikipendekeza baadhi ya sura zinazotarajiwa kuingia katika baraza hilo.
Hata hivyo, ukweli utajulikana leo baada ya Katibu Mkuu Kiongoza kutangaza rasmi.
Kuna wasiwasi kuwa huenda Rais akawabadilisha baadhi ya mawaziri wanaodaiwa kuwa mizigo, baada ya Chama cha Mapinduzi (CCM), kuwataja na kupendekeza wahojiwe na Kamati Kuu (CC) ya chama.
Wizara zinazolalamikiwa ni ya Maji, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika.
Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa zamani wa Wizara ya Miundombinu Omari Chambo, ameteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara.
Aidha aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Dk. John Ndunguru, anakwenda kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma.
Taarifa ya Ikulu iliyotolewa Dar es Salaam jana ilisema uteuzi huo pia umemhamisha Mkurugenzi wa Jiji la Arusha Sipora Liana kwenda Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za MItaa (Tamisemi) na nafasi yake kuchukuliwa na Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya Juma Iddi.
MAKATIBU WAPYA
Makatibu Tawala wapya wa mikoa mitano ni Wamoja Dickolangwa (Iringa) Abdallah Chikota (Lindi), Symthies Pangisa (Rukwa), Alfred Luanda (Mtwara) na Jackson Saitabau ( Njombe).
WALIOHAMISHWA
Beatha Swai aliyekuwa Pwani amehamia Tamisemi, Benedict Ole Kuyan zamani Tanga sasa Mara, Salum Chima wa Rukwa anayekwenda Tanga, Mgeni Baruani zamani Njombe na sasa anakwenda Pwani. Uteuzi na uhamisho huo ulianza rasmi jana kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI