Bahati (katikati) akiwa hospitalini na baadhi ya wajeruhiwa wa mgogoro baina ya wakulima na wafugaji katika Wilaya ya Kiteto.Picha na Musa Juma.
Kiteto:Bahati ni kweli ana bahati kama jina lake lilivyo Bahati. Katika mapigano, yaliyotokea hivi Karibuni, mtoto, Bahati Juma alikuwa ni mmoja wa watu waliojikuta wako katikati ya mapigano hayo.
Mtoto huyu anasema alikamatwa na kundi la wafugaji wa Kimasai, akiwa ndani ya nyumba yao iliyochomwa moto. Katika tukio hilo, Bahati alinusurika kufa ingawa tayari sime ilikuwa imeanza kukata shingo yake.
Hivi sasa Bahati amelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kiteto, Mkoa wa Manyara, akiuguza jeraha la kukatwa na sime na ameshonwa nyuzi nane huku akiwa na majeraha ya fimbo mgongoni na mikononi.
Ndugu zake watatu ambao ni wakulima wote kutoka mkoani Dodoma, wameuawa ambao ni Juma Mlangwa (47) na Yohana Hivo (33) waliuawa papohapo na Mussa Juma alifariki akiwa hospitali.
ENDELEA KUSOMA HABARI HII KWA KUBOFYA HAPA CHINI
Katika mapigano hayo yaliyotokea Desemba 21 Kijiji cha Olpopong, wakulima wengine wanane walijeruhiwa, mmoja alikuwa mahututi. Mussa Juma ambaye alichomwa mkuki wa mbavu, alihamishiwa hospitali ya Mkoa ya Dodoma, alifariki baadaye.
Wengine waliolazwa hospitali ya wilaya ya Kiteto ni Emanuel Mathias (26), Hoti Damas (38), Mwajuma Hamis (20), Habiba Ally(16 ) na Mwajuma Martin(33).
Daktari azungumza
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya wilaya ya Kiteto, Thomas Ndalio anasema, hali za majeruhi hao saba zinaendelea vizuri.
“Mussa ndio hali yake ilikuwa mbaya sana na ndio sababu alihamishiwa Hospitali ya Mkoa wa Dodoma kwa matibabu zaidi, kwa bahati mbaya alifariki,”anasema Dk Ndalio.
Bahati asimulia alivyonusurika kifo
Anasema, anakumbuka Desemba 21 alikuwa nyumbani na ndugu zake, wakiwa wamepumzika baada ya kutoka shamba kulima.
Siku hiyo anakumbuka kulikuwa kumezuka mgogoro katika eneo la malisho kati ya wakulima na wafugaji wa jamii ya Kimasai. Wafugaji hao walikuwa wameingiza katika mashamba yao, mifugo na walifanikiwa kuwafukuza.
Hata hivyo, anasema ilionekana wafugaji hao, walikasirishwa na kufukuzwa lakini waliondoka na hasira.
“Sasa mimi nikiwa ndani ghafla nilisikia nje watu wakisema kuna vita! kuna vita!. Nilipotaka kutoka, tayari nyumba yetu ilikuwa imeshika moto,” anasema Bahati.
Anasema aliamua kutoka mbio ili kujiokoa, lakini alijikuta yuko mikononi mwa wafugaji wa kimasai, walimkamata na kuanza kumkata na sime huku wengine wakimchapa.
“Wakati wanaendelea kutaka kunichinja ndugu zangu wengine walijitokeza, ugomvi ulikuwa mkubwa na hapo niliona wenzangu wawili wakiuawa kwa kuchomwa mikuki na kukatwa sime”anasema Bahati.
Anasema baada ya tukio hilo, wafugaji waliendelea kuchoma nyumba zao, baadaye wakaondoka huku wakionya wasisumbuliwe.
“Wakati huo mimi nilikuwa chini nalia, damu zilikuwa zinanivuja, baadaye nilichukuliwa na kuletwa hapa hospitalini,”anasema Bahati huku akisisitiza kuwa Serikali ikomeshe haraka mgogoro huo.
Aomba Serikali kumaliza mgogoro
Bahati anaomba Serikali, kutatua mgogoro wa ardhi katika wilaya hiyo, kwani hali ya usalama sio nzuri katika kijiji cha Olpopong wanachoishi.
“Tunaomba tu watusaidie tukae kwa amani na hawa wafugaji,“anasema Bahati kwa uchungu.
Anasema kama amani ikipatikana katika eneo lao, atarejea kuishi, lakini kwa sasa bado ana hofu kwani bado hajui ndugu zake wengine wamekimbilia wapi.
Chanzo cha mapigano
Saitoti Kalanga, ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Olpopong kilichotokea mapigano baina ya wakulima na wafugaji na kusababisha vifo vya watu wawili, anasema chanzo cha mapigano hayo ni watu kuvamia ardhi ya kijiji bila kufuata mpango wa matumizi bora ya ardhi na kila wanapotakiwa kuondoka wamegoma.
Anasema watu hao wakiwemo wakulima wamejianzishia vitongoji batili ndani ya kijiji. Katika maeneo wanayolima wamekuwa wakikamata mifugo inayopita na kuikatakata kwa mapanga jambo ambalo limekuwa kero kubwa kwa zaidi ya miaka miwili sasa.
“Wakulima ni wavamizi, hawatambui Serikali ya kijiji, wameingia tu kwa nguvu na wanalima kwa kukata miti ovyo jambo ambalo limewaudhi wafugaji,”anasema Kalanga.
Kalanga anasema kijiji hicho, kilichosajiliwa mwaka 1993, kina mpango wa matumizi ya ardhi, uliopitishwa na halmashauri tangu mwaka 2010, lakini umekuwa haufuatwi baada ya wakulima kuvamia.
Mwenyekiti huyo anaonyesha ramani ya mpango wa matumizi ya ardhi katika kijiji hicho; ekari 2880 zilitengwa kwa kilimo, hekari 1, 450 kwa makazi, ekari 9184 kwa malisho na ekari 9805 hifadhi ya jamii.
“Hivi sasa ardhi ya malisho na hifadhi imevamiwa na wakulima kutoka Mkoa wa Dodoma, ndiyo sababu kumeibuka mapigano,”anasema Kalanga.
Naye Mwenyekiti wa Kitongoji cha Eseriani, ambacho mapigano yametokea, Mariam Ijumaa, anasema kumekuwepo na uvamizi wa wakulima katika kitongoji chake, anaamini suluhu ni kuwagawia ardhi.
“Uvamizi unaongezeka na hawa wanaokuja hawataki hata kutambua Serikali ya kijiji, wameanzisha vitongoji vyao porini,”anasema Ijumaa.
Waeleza suluhu ya mgogoro huo
Saitoti Kalanga, Mariam Ijumaa na Alaisi Nangoro, wakazi wa eneo hilo wanasema suluhu ya mgogoro ulioibuka katika kijiji hicho ni kufuatwa mpango wa matumizi bora ya ardhi.
Nangoro anasema kwa kuwa tayari kijiji hicho kilipimwa, ni busara Serikali ikasaidia kufuatwa mpango halali; kama kuna wakazi wasio na ardhi wapewe.
“Tunapaswa kuishi kwa amani, mapigano yaliyozuka hapa yasitokee tena, ni muhimu kuheshimu mamlaka za vijiji kwa wale wanaotaka ardhi,”anasema Nangoro. na mkazi wa kijiji hicho,
Kauli ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Elaston Mbwilo, anaeleza Serikali kusikitishwa na hali ya mapigano ya ardhi katika wilaya ya Kiteto na hadi kufikia watu watatu kufariki ndani ya wiki moja na wengine wanane kujeruhiwa.
Mbwilo anaagiza Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto kusaidia vijiji kuondokana na mapigano ikiwamo kupanga matumizi bora ya ardhi na kuwaondoa wavamizi. “Haiwezekani watu wavamie tu ardhi kama hakuna viongozi, ni lazima tufuate sheria,” anasema.
MWANANCHI