Septemba mwaka jana, mfanyakazi wa Wakala wa Ndege za Serikali, Dominic Bomani alimwambia Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe alipotembelea uwanjani hapo kuwa wapo wahamiaji haramu ambao wamepewa nafasi nyeti za ajira katika uwanja huo. Dk Mwakyembe aliahidi kufuatilia suala hilo.
Uchunguzi wa Mwananchi umebaini kuwa polisi katika baadhi ya viwanja vya ndege wamejenga mtandao na watumishi wengine, wakiwamo wa Idara ya Uhamiaji ambao huwawezesha raia wa kigeni hasa kutoka nchi za Ethiopia, Somalia na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC), kuingia nchini bila ya kuwa na nyaraka zinazokubalika kisheria.
ENDELEA KUSOMA HABARI HII KWA KUBOFYA HAPA CHINI
Tukio la karibuni zaidi ni lile la kuingizwa nchini kwa raia watatu wa Pakistani ambao licha ya kukamatwa katika Uwanja wa Ndege wa zamani (Terminal – I) kutokana na kutokuwa na hati za kusafiria, wala nyaraka zozote zinazowaruhusu kuingia nchini, baadaye waliachiwa na kuingia nchini katika mazingira ya kutatanisha.
Chanzo chetu uwanjani hapo kilisema: “Hawakuja na hati za kusafiria wala nyaraka zozote na waliachiwa huru katika mazingira ya kutatanisha.”
Chanzo hicho kiliwataja Wapakistani hao kuwa ni Hussein Amir, Ahmad Tahmir na Shakeel Muhamadadi ambao walifika nchini, Oktoba Mosi, 2013 saa kumi na moja jioni kwa ndege ndogo ya kukodi ambayo ilikuwa ikitokea Zanzibar.
Baada ya kufika, walishukia Terminal 1 na baadaye kwenda kuswali katika msikiti wa karibu, lakini kabla ya kutimiza azma yao hiyo, walikamatwa na polisi kisha kufunguliwa hati ya kukamatwa (RB) namba JNIA/1005/2013.
Mapema baada ya kuwasili kwao, wageni hao walipokewa na Dereva Teksi, Shami Maringo ambaye alikiri kwamba aliagizwa kuwapokea, lakini kabla ya kuanza safari waliomba kwenda msikitini kuswali kwa sababu ilikuwa tayari ni saa 12:00 jioni.
Maringo alisema aliwapokea raia hao watatu baada ya kupewa majina yao na Mtanzania mwenye asili ya Asia ambaye alimwambia baada ya kuwapokea awapeleke Kariakoo.
“Nilipewa majina matatu kwenye karatasi na mhindi mmoja, nikaambiwa hao watu watafika saa 10 jioni. Walipofika nikawatambua lakini tulikamatwa,” alisema Maringo.
Maringo pia alikamatwa na kuambiwa kuwa ataachiwa baada ya mtu aliyemwagiza kuwapokea raia hao atakapofika.
Alisema siku ya pili asubuhi, mtu huyo ambaye hata hivyo, alisema hamfahamu kwa jina, alifika polisi na Maringo pamoja na raia hao waliachiwa huru. Maringo anasema hakuweza tena kuwapeleka kwa sababu gari lake lilipata pancha.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa tukio la kukamatwa hadi kuachiwa kwa raia hao wa Pakistani lilimhusisha Ofisa Upelelezi Kituo cha Polisi cha JNIA, Denis Moyo.
Chanzo chetu cha habari kinaeleza kuwa ili kufuta ushahidi wa tukio hilo, taarifa za wahamiaji hao haramu hazikuandikwa katika kitabu cha rekodi za polisi kama inavyotakiwa.
Kauli za wahusika
Kamanda wa Polisi wa Viwanja vya Ndege, Seleman Hamis anasema taarifa hizo ni za kushtua kwani hakudhani kama mambo kama hayo yanaweza kutendeka kwani ulinzi mkali umewekwa uwanjani hapo.
“Nashukuru kwa taarifa hizi, unajua nyinyi waandishi wa habari ni wa muhimu sana katika habari za uchunguzi na mnaweza kutusaidia katika kazi zetu,” alisema.
Kamanda Hamis alisema inawezekana kabisa kuwa watu wanafanya vitendo vya uhalifu huo pasipo polisi kufahamu. Hivyo wananchi hawana budi kutoa ushirikiano ili kuutokomeza.
Moyo ambaye pia ni Msaidizi wa Mkuu wa Makosa ya Jinai wa JNIA alipoulizwa kuhusu madai hayo badala ya kujibu, aliuliza maswali mengi, huku akitaka apewe majina ya baadhi ya wahamiaji hao.
Baada ya kupewa, aliomba apewe dakika chache kisha apigiwe tena na alipopigiwa simu baada ya dakika 20 alisema: “Nashukuru kwa taarifa nitazifanyia kazi, ilimradi umenipa taarifa basi nitazifanyia kazi.”
Kabla ya kutoa majibu hayo, ilisikika sauti ya mwanamke ambaye hakufahamika ikimwelekeza: “Mwambie kwamba suala hilo litashughulikiwa.”
Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa JNIA, Felisia Mtenga alikanusha kuwapo kwa taarifa hizo na kusema hakuna suala kama hilo katika uwanja huo ingawa alimtaka mwandishi kuzungumza na Moyo.
Kwa upande wake, Meneja wa Usalama wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Clemence Jingu alisema hafahamu suala hilo na haliwezekani kufanyika katika uwanja huo akisema ni lazima mgeni yeyote anayefika awe na hati ya kusafiria, tiketi ya kurudi na viza.
Hata hivyo, alisema hakuna tatizo iwapo wageni wanafika na ndege ya kukodi wakitokea Zanzibar kwani uwanja wa huko unatakiwa kuhakikisha kuwa wana nakala zote za kusafiria na wanapofika Dar es Salaam hufika kama watu wa kawaida hivyo, hakuna haja ya kuangaliwa upya.
“Kila uwanja wa kimataifa una sheria zake, akitua Zanzibar halafu akakodi ndege kuingia Dar es Salaam, hana haja tena ya kuonyesha documents (nyaraka) zake, anaingia kama mwenyeji tu,” anasema Jingu.
Alipoelezwa kuwa wapo wahamiaji haramu wanaoingia kupitia JNIA moja kwa moja kutoka nje alisema ni vigumu mno... “Haiwezekani wakawahonga, uhamiaji, polisi wa uwanja wa ndege na kila mtu, ni vigumu. Lakini kama kuna suala kama hilo sijalisikia na silifahamu. Zungumza na watu wa Uhamiaji.”
Msemaji Mkuu wa Idara ya Uhamiaji, Naibu Kamishna wa Uhamiaji, Abbas Irovya alipoulizwa alisema: “Tunashukuru kwa taarifa, lakini nafikiri tukipata ushahidi kamili kama muda wa tukio, waliohusika na jinsi matukio hayo yanavyofanyika, tutashukuru zaidi kwa sababu mtakuwa mmetusaidia.”
Mamlaka za Zanzibar
Kamishna wa Polisi Zanzibar, Hamdani Makame alisema ingawa ameishika nafasi hiyo Zanzibar kwa muda mfupi lakini anafahamu kuwa kuna tatizo la wahamiaji haramu.
“Ni pana, linahitaji mshikamano wa kila kitengo. Kama wahamiaji wametokea Pakistani lazima watakuwa wameanza kufanya mchezo huo tangu huko walipotoka kwa hiyo ni tatizo mtambuka,” alisema Kamishna Makame.
Alisema Uwanja wa Ndege Abeid Amani Karume unakabiliwa na uhaba wa watenda kazi jambo ambalo alikwishapelekewa malalamiko na RPC wake.
Mkurugenzi wa Uwanja huo, Juma Salehe alisema hajapata taarifa hizo... “Zipo tuhuma za hapa na pale ambazo huwa tunazifanyia kazi na iwapo zinatushinda tunazipeleka ngazi za juu, ingawa kwa tukio la hao raia wa Pakistani, sijalisikia.”
Alisema suala la wahamiaji haramu limesambaa kwani hata uhamiaji nao huenda wanahusika kwani ndiyo wanaohakiki hati za kusafiria na visa.
MWANANCHI