“Wengi wetu tunaishi bila kujiuliza maswali kama; “Itakuwaje iwapo siku nitaamka nikiwa sina uwezo wa kuona tena? Hatujiulizi maswali kama haya kwa sababu tunavichukulia vitu muhimu kuwa vya kawaida tu.”
“Hata mimi nilikuwa mmoja kati ya watu hao hadi Januari 2008, nilipopoteza uwezo wa kuona, mama yangu alikuja kuniamsha lakini jibu langu lilikuwa; siwezi kuona, siwezi kuona,” anaanza kusimulia Margareth.
Miaka sita iliyopita Margareth Maganga alikwenda kulala akiwa binti mwenye afya njema na furaha tele, lakini asubuhi ya siku iliyofuata aliamka akiwa na ulemavu wa kutooona. Kwa kijana wa umri wa miaka 19 tu, lilikuwa ni tukio la kutisha, kukatisha tamaa na kutia simanzi.
Ilikuwa Ijumaa ya Januari 11, 2008 mama yake Margareth alipokwenda kumwamsha binti yake kwani alikuwa amelala hata baada ya muda wake wa kawaida kuamka kuwa umepita.
“Mama aliingia chumbani kuniamsha na kuhoji kwa nini nilikuwa nimelala mpaka muda huo, nilimwambia sijaamka kwa kuwa bado ulikuwa usiku, mama aliniambia tayari ilikuwa ni saa mbili asubuhi. Nilifikicha macho kutazama, lakini sikuona kitu...; Nilibaini kuwa nimepoteza uwezo wa kuona,” anasema Margareth.
ENDELEA KUSOMA HABARI HII KWA KUBOFYA HAPA CHINI
Binti huyu ambaye sasa ana umri wa miaka 25 anasema kuwa mwanzoni alipopoteza uwezo wa kuona alihisi dunia imemwelemea kutokana na ukweli kwamba, alianza kuona matarajio yake ya kuwa mwanasheria yamepotea.
“Kilikuwa kipindi cha mateso kwangu na familia yangu, ingawa wao walijaribu kutoonyesha hofu ili kunipa nafuu. Lakini maswali kutoka kwa rafiki na kuishi kwa kutegemea msaada kwa kila ninalotaka kufanya, vilinifanya nikate tamaa,” anasema Margareth.
Anaongeza kuwa alikosa raha kila alipokumbuka kuwa hawezi kutimiza ndoto zake, lakini alipiga moyo konde na kukubali hali yake, ingawa haikuwa rahisi kwake ukilinganisha na ndoto alizokuwa nazo.
Safari gizani
Pamoja na kuwa katika kipindi kigumu cha maisha yake, Margareth ameandika kitabu kiitwacho A Journey Through Darkness ambacho anaelezea safari yake tangu alipopoteza uwezo wa kuona.
Katika kitabu hicho anasimulia jinsi alivyoanza kupata maumivu makali akiwa nchini Taiwan katika Kongamano la Vijana (World Youth Conference for Adventist Youth), alipoanza kupata homa kali na maumivu ya misuli.
“Sikutaka kuonekana mgonjwa, nilijikaza. Hata hivyo, nilizidiwa na wenzangu walinipeleka hospitali. Majibu yalionyesha kuwa nina upungufu wa damu hivyo niliambiwa kuna aina mbili za matitabu ya haraka; moja ilikuwa kuongezewa damu au kupewa vidonge ambavyo vingetuliza maumivu kwa muda,” anasema
Ilimchukua siku mbili kufika kwao Musoma na huko alianza kupatiwa matibabu, mpaka ilipofika Januari 11 alipoamka akiwa amepoteza uwezo wa kuona.
“Baada ya vipimo katika Hospitali za Muhimbili na CCBRT, daktari alishauri nipelekwe nje ya nchi kufanyiwa matibabu kwani hapa uwezo wao ulikuwa umefikia mwisho. Wazazi wangu walifanya mpango nikapelekwa Marekani, baada ya kufanyiwa operesheni nilianza kuona kwa mbali,” anasema na kuongeza:
“Nilipoteza uwezo wa kuona kwa zaidi ya mwezi mmoja, hivyo kuziona tena sura za familia yangu na ndugu zangu wengine, ilikuwa furaha ingawa siyo uono mzuri kama ule wa zamani.”
Margareth anasema kuwa anaamini kupoteza uwezo wa kuona siyo mwisho wa maisha, kwani ungekuwa ndiyo ukweli wenyewe, asingeweza kusoma Shahada ya Sheria na kuandika kitabu kwani vyote amevifanya.
“Kupoteza uwezo wa kufanya jambo lolote inaweza kuwa mwanzo mpya katika maisha yako. Nimemaliza shahada yangu ya sheria nchini Uingereza, nimeandika kitabu na kuanzisha Shirika lisilo la kiserikali la kusaidia wenye uono hafifu na wasioona liitwalo; Hope For The Blind ,” anasema na kuongeza:
Misaada kwa wengine
“Ninasaidia wenye matatizo kama yangu kwa kutoa Sh2,500 katika kila pesa ya kitabu kimoja ninachouza na kuiingiza katika mfuko. Ninasaidia kwenye elimu na matibabu kwa kutumia pesa za mfuko huo.”
Margareth anasema kuwa anaamini kwamba watu wengi wanapoteza uwezo wa kuona kutokana na kukosa matibabu sahihi.
“Mimi ni mfano mzuri, kwani kama wazazi wangu wasingeweza kunipeleka nje ya nchi, ina maana leo hii nisingekuwa na uwezo wa kuona, ingawa sioni vizuri. Wengi wanakosa matibabu sahihi,” anasema.
Anaongeza kuwa ipo haja kwa Serikali kuangalia tena namna matibabu ya watu wasioona, kwani matatizo yao mengine yanaweza kutatuliwa, lakini hospitali hazina vifaa vya kutosha na wataalamu.
“Ipo haja ya kuwekeza katika huduma za macho. Naamini siyo kila asiyeona yupo hivyo kwa sababu Mungu amempangia, isipokuwa ni kwa kukosa matibabu sahihi. Serikali iweke nguvu katika hili pia,” anasema Margareth.
Kuhusu elimu ya watu wasioona, Margareth anasema kuwa ni muhimu Serikali, wadau na watu binafsi wawekeze katika kuwasaidia kwani wengi bado wanasoma katika mazingira magumu ukilinganisha na mahitaji yao.
“Wasioona wanahitaji kupata elimu sahihi na kwa wakati, ni vyema wote kwa pamoja tukasaidiana kuboresha mazingira yao ya kusomea kwani yaliyopo hivi sasa hayaridhishi hata kidogo, na inavyoonekana hayapewi kipaumbele,” anasema Margareth.
Margareth Maganga alizaliwa mwaka 1988. Elimu yake ya msingi na sekondari alipata nchini Kenya katika Shule za Kajiado na ‘The Kenya High School’, baadaye alipata Shahada ya Sheria katika Chuo Kikuu cha Leeds, Uingereza.
Ni mtoto wa kike pekee katika familia ya Paschal Manganga yenye watoto wengine wa kiume wa watatu, Evarist, Raphael na Luckness.
Mbali na kuwa mwanaharakati wa kusaidia watu wenye matatizo ya kuona, Margareth anasema kuwa ndoto zake ni kuwa Jaji kwa kuwa anataka kutoa haki kwa wanaostahili.
MWANANCHI
MWANANCHI