Meneja wa Manchester United, David Moyes amesema hatofanya mabadiliko yoyote kwenye mbinu zake na kuwaomba mashabiki wa timu hiyo kuwa na imani nazo licha ya kuiacha timu hiyo ikishindwa mara nne mfululizo kwa mara ya kwanza tangu zaidi ya miaka 50 iliyopita.
Meneja huyo jana alipigwa faini na chama cha soka cha England kwa kutoa kauli chafu kwa marefa kufuatia kushindwa na Sunderland kwenye kombe la Capital One Cup.
“Unaendelea kufanya kile ulichokuwa ukikifanya,” alisema Moyes. Kama ukibadilisha, inamaanisha kuwa ulikuwa ukifanya vitu sivyo mwanzoni lakini hatufanyi na vitu tulivyokuwa tukivifanya viko sahihi. Kwenye uongozi, lazima utapoteza michezo. Simjui kocha yeyote ambaye hajawahi kupoteza michezo na lazima upitie hilo katika sehemu ya career yako.”
“Ni wazi, kama haushindi inaweza kuathiri kujiamini kwako na hiyo ni sehemu kubwa ya soka. Lakini kabla ya hiyo, tulishinda michezo sita na tulikuwa hatuongeii kuhusu kujiamini baada ya hapo.”
“Wachezaji wamekuwa vizuri sana. tunahitaji tu vitu vya kwenda navyo, tunahitaji kucheza vizuri na kutumia nafasi. Takwimu zote ni nzuri, lakini kitu pekee chenye maana ni magoli na hatujafunga ya kutosha hivi karibuni.”