Tunasema kitendo cha abiria kuruhusiwa kukaa juu ya boti, eneo ambalo ni hatari kwa usalama wao ni uzembe wa kiutendaji na hivyo wale wote waliokuwa wakisimamia boti hiyo wanapaswa kupelekwa kwenye vyombo vya dola.PICHA|MAKTABA
Matukio ya ajali za Bahari ya Hindi kwa upande wa Zanzibar yamekuwa yakitokea mara kwa mara licha ya ahadi za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kwamba wanafanya kila aina ya juhudi kuhakikisha katu hayatokei.
Matokeo haya ambayo kwa kiasi kikubwa yanayotokea katika eneo la Zanzibar yanachangiwa na uzembe ama wa wamiliki, watendaji, vifaa vya usafiri au viongozi wa Serikali ambao wanapaswa kusimamia usafiri wa majini nchini kwa viwango vinavyokubalika kimataifa.
Tumesukumwa kuandika maoni haya baada ya juzi ajali ya boti ya Mv Kilimanjaro II kupigwa dhoruba ambapo abiria waliokuwa wamekaa juu yake kuzama huku wengine wakipoteza maisha.
Taarifa zilivyoripotiwa kwenye vyombo vya habari jana, zinasema miili ya watu sita ilipatikana ikiwa miongoni mwa waliozama baada ya boti ya Mv Kilimanjaro II kupigwa dhoruba katika mkondo wa Nungwi ikitokea Pemba kwenda Unguja juzi.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, boti ya Mv Kilimanjaro II iliyokuwa imebeba abiria 380 ilipigwa na upepo mkali na kuleta taharuki kwa wasafiri, huku watu waliokuwa wamekaa juu wakidaiwa kuteleza na kutumbukia baharini. Jambo la kusikitisha maofisa wa meli walizembea kutoa taarifa sahihi ili waokoaji waende eneo la tukio mapema.
Tunasema kitendo cha abiria kuruhusiwa kukaa juu ya boti, eneo ambalo ni hatari kwa usalama wao ni uzembe wa kiutendaji na hivyo wale wote waliokuwa wakisimamia boti hiyo wanapaswa kupelekwa kwenye vyombo vya dola.
Tunasema hivyo kwa kuwa eneo la Nugwi limekuwa likikumbwa na majanga ya mara kwa mara kutokana na upepo mkali unaovuma eneo hilo hivyo watendaji wa boti ya Mv Kilimanjaro II walipaswa kulijua hili kwa kukataza abiria kukaa juu ya boti.
Tunasema huu ni uzembe wa hali ya juu usiokubalika kwa utetezi wa aina yoyote ile kwani ni jambo lisiloingia akilini kwamba eneo lenye upepo mkali kama Nungwi wafanyakazi wa boti waliweza kuruhusu hata watoto wadogo kukaa juu ya boti.
Kwa maoni yetu, mamlaka zinazosimamia usafiri wa maji katika Bahari ya Hindi na sehemu nyingine nchini zinapaswa kuwa makini hasa katika maeneo yenye dhoruba za kila wakati. Sote ni mashahidi kwamba Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini ilitoa taarifa Desemba mwaka jana kwamba kutakuwa na upepo usio wa kawaida katika ukanda wa Bahari ya Hindi hivyo watu wachukue tahadhari.
Vilevile, taarifa za kutisha kwamba nahodha wa boti ya Kilimanjaro 11, Khamis Abubakar Khamis alitoa taarifa za uongo dhidi ya ajali hiyo ni jambo ambalo likithibitika ni ukweli basi lazima tutilie shaka uzalendo na utu wa nahodha huyu kwa wananchi.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (ZMA) Mhandisi Abdi Omar Maalim , taarifa iliyotolewa na nahodha katika kituo cha mawasiliano (Signal Station) zilikuwa za uongo na kusababisha kazi ya uokoaji kuchelewa na kutofanyika kwa muda mwafaka.
Tunaambiwa kwamba nahodha katika ripoti yake alisema hakuna abiria waliotumbukia baharini zaidi ya vifaa vya uokoaji na mizigo na hivyo akaamua kuendelea na safari. Ndiyo maana tunasema kwamba sheria lazima ichukue mkondo wake, ili wale wote ambao wamepewa majukumu ya kusimamia vifaa hivi vya usafiri wawe waangalifu . Tusipofanya hivyo, abiria wasio na hatia wataendelea kupata majanga ya aina hii na kuzidi kupoteza maisha.