KUSIMAMISHWA kwa kiungo Athumani Iddi ‘Chuji’ Yanga huenda ndio ukawa mwisho wake kuichezea klabu hiyo yenye maskani yake mtaa wa Twiga na Jangwani Dar es Salaam.
Habari za kuaminika zilizopatikana jijini Dar es Salaam jana, Chuji alipewa barua ya kusimamishwa jana akidaiwa kuwa na nidhamu mbovu.
Mtoa habari wetu ambaye ni mmoja wa viongozi wa Yanga, alikiri Chuji kusimamishwa ingawa hakuwa tayari kuweka hadharani aina ya utovu wa nidhamu aliofanya kiungo huyo.
“Ni kweli kama habari zilivyozagaa kwamba Chuji kasimamishwa, lakini siku itakayozungumzwa rasmi, nadhani tatizo lake litawekwa hadharani kila mmoja alijue,”alisema mtoa habari wetu.
Hata hivyo,taarifa zinadai kuwa, Chuji amekuwa na utovu wa nidhamu ikiwa ni pamoja na kutosikiliza maagizo wanayopewa na viongozi na makocha.
“Kila kwenye tukio la ajabuajabu Chuji hakosekani, na sio kwamba haonywi, uongozi umemuonya mara kadhaa, mpaka kufikia kumsimamisha kwa muda usiojulikana, hata sisi pia tumechoka kumuonya mtu mmoja huyohuyo kila mara,” alisema.
ENDELEA KUSOMA HABARI HII KWA KUBOFYA HAPA CHINI
Habari zinadai kuwa, Chuji pia amekuwa akichagua wachezaji wa kusajiliwa kwenye timu hiyo, na inadaiwa usajili wa hivi karibuni wa kipa Juma Kaseja na mshambuliaji Emmanuel Okwi hakuufurahia.
“Mara kwa mara alikuwa akihoji sababu za kuwasajili Okwi na Kaseja, sasa yeye ni mchezaji tu kama wengine, anawezaje kuamua fulani asajiliwe fulani asisajiliwe?” Alihoji mtoa habari wetu.
Hata hivyo, Chuji amesaini mkataba wa miaka miwili na Yanga hivi karibuni, kitu ambacho pengine kinaweza kumnusuru, ingawa inadaiwa Yanga inaweza kuvunja naye mkataba au kumtoa kwa mkopo.
Chuji aliwahi kuondolewa kwenye timu ya taifa, Taifa Stars na aliyekuwa kocha wa timu hiyo Mbrazil Marcio Maximo akidaiwa kuwa na utovu wa nidhamu pia.
Wengine alioondolewa nao kwenye timu hiyo chini ya Maximo alikuwa Haruna Moshi ‘Boban’ ambaye kwa sasa amesajili na Costal Union na Amir Maftaha.
HABARI LEO