Delfina akilia machozi ya damu.
Dominica. Waswahili husema; matatizo hayapigi hodi. Ndivyo ilivyo siyo kwa waswahili tu, bali kwa binadamu wote.
Dominica. Waswahili husema; matatizo hayapigi hodi. Ndivyo ilivyo siyo kwa waswahili tu, bali kwa binadamu wote.
Miongoni mwa watu wanaoweza kuelezea vyema kauli hiyo msichana Delfina Cedeno (19), ambaye hutokwa na machozi na jasho la damu.
Ugonjwa huo unaotajwa na madaktari kama siyo wa kawaida, pia umemfanya Cedeno kutoka damu kwenye kucha na kitovu kwa muda wa miaka minne sasa.
Hali ya binti huyo ambaye alianza kupoteza matumaini ya kuishi, ilizidi kuwa mbaya baada ya kuanza kutokwa na damu puani, huku nywele zake zikinyofoka kila siku.
Akizungumza na gazeti la Mirror, Delfina, ambaye ni mkazi wa Veron, Jamuhuri ya Dominica, anasema kuwa wakati Fulani, aliwahi kutokwa na damu kwa muda wa siku 15 mfululizo, hata kulazimika kuongezewa dripu za damu.
Vipimo alivyofanyiwa
Anasema kuwa hadi sasa ameshafanyiwa vipimo zaidi ya mia moja, lakini hakuna daktari hata mmoja aliyeweza kubaini chanzo cha tatizo lake.
“Wakati tatizo hili linaanza kunitokea sikujua nifikiri nini, niliogopa na kubaki na mshituko mkubwa.
ENDELEA KUSOMA HABARI HII KWA KUBOFYA HAPA CHINI
Mwanzoni hakuna mtu aliyetaka kunisaidia, walikuwa wananiangalia kama vile mimi ni kichaa pale nilipojaribu kuwaambia kitu gani kinanitokea,” anasimulia Delfina na kuongeza:
“Hadi pale siku moja nilipoanza kutokwa na damu mbele ya daktari, ndipo walipoanza kulipa umuhimu suala langu.”
Anasema kuwa kutokana na hali yake, anajisikia vibaya hadi kushindwa kuendelea kuishi nyumba moja na mama yake anayejulikana kwa jina la Mariana.
Delfina alilazimika pia kuacha masomo, baada ya rafiki zake wengi kuadhani kuwa huenda angewaambukiza ugonjwa aliokuwa nao.
Chanzo chake
Anasema: “Watu waliniogopa. Walidhani kama wakinishika ningewapaka damu. Watoto wananicheka na kunipigia kelele, muda mwingi ninashinda chumbani kwangu.”
Baada ya kukata tamaa ya kuishi, siku moja binti huyo aliamua kunywa kiwango kikubwa cha dawa ili ajiue, lakini madaktari walifanikiwa kumwokoa.
Anasema: “Nilitaka kufa. Familia yangu ilinikuta nikiwa na hali mbaya chumbani kwangu, huku nikitoka povu mdomoni. Niliishia kukaa chumba cha uangalizi maalumu kwa muda wa wiki nzima hadi nilipozinduka. Ni kama vile nilikuwa nimekufa.”
Anaongeza: “Nilizidiwa, nikawa ninapigwa kwa shoti ya umeme. Kwa kweli kulikuwa na uwezekano ningevunjika mbavu zangu. Lakini inashangaza kwamba sasa ni mzima. Nina furaha kwa sababu maisha yangu yameanza kuimarika.”
Siku moja akiwa hospitali, alitembelewa na mwanaume mmoja aliyetambuliwa kwa jina la Recaris Avila, ambaye baadaye alikuja kuwa rafiki yake wa kiume.
“Aliniambia mimi ni mzuri. Nitaikumbuka hiyo siku zote za maisha yangu,”anasema.
Baada ya miaka minne ya mateso, hatimaye madaktari wameanza kuelekea kupata tiba ya ugonjwa wake.
Wanasema kuwa Delfina unasumbuliwa na ugonjwa unaoitwa Hematidrosis, unaomaanisha kwamba ana kiwango kikubwa cha adrenaline kinachofikia mara 20 ya mtu wa kawaida.
Chanzo chake
Ugonjwa huo humpata mtu anapokuwa na kiwango kikubwa cha hofu, hivyo kufanya shinikizo la damu kuwa juu na kumfanya atoke jasho la damu.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Jarida la India la Dermatology, mishipa mingi ya damu inayozunguka sehemu za kutolea jasho hubana na kuwa na wembamba wakati mtu anapokuwa na shinikizo la damu.
Hofu inapoongezeka, mishipa ya damu hupasuka. Damu huingia hupita kwenye matundu ya jasho na hivyo kutengeneza mchanganyiko wa damu na jashoMadaktari wamempa Delfina dawa ya kudhibiti hofu ambayo imemsaidia kupunguza damu kutoka mwilini.
Akimsifu mchumba wake ambaye wameahidiana kufunga ndoa, Delfina anasema: “Namshukuru Recaris maana ninajisikia nipo huru na sitaki tena kufa. Kukutana naye lilikuwa jambo la furaha sana. Bado ninaweza kuanza kutoka tena damu, lakini sina wasiwasi kwa kuwa najua yupo karibu yangu kunisaidia.”
Kwa upande wake Avila anasema: “Ninauona urafiki wetu ni wa kawaida pamoja na hali aliyonayo, nampenda. Kwangu yeye ni wa kawaida, ingawa wakati mwingine anajisikia vibaya kwa sababu hataki mimi nimwone akitoka damu.
“Mimi namwambia sina wasiwasi, nina furaha.”
Imeandikwa na Goodluck Eliona kwa msaada wa mtandao.
MWANANCHI
MWANANCHI