Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willbroad Slaa, amelaani kitendo cha Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo cha kukumbatia wawekezaji wa nje katika rasilimali ya gesi na kuwanyima wawekezaji wa ndani.
Amesema waziri huyo anataka kuwagawia wazungu vitalu vya gesi ili wachimbe mabomba kuisafirisha Ulaya badala ya kusambaza nchini itumike kama nishati kuwaletea wananchi maendeleo.
Alisema hayo jana wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Mwangoye jimbo la Bukene wilayani Nzega mkoani Tabora katika ziara yake ya kutembelea mikoa ya Kigoma, Tabora na Singida.
"Waziri Muhongo amekuwa muongo kama jina lake lilivyo, anasema Watanzania hatuwezi kuwekeza kwenye miradi mikubwa kama ya gesi, uwezo wetu ni kutengeneza juisi na maji, mimi nasema kama hatuwezi basi gesi hiyo ikae ardhini hadi tutakapokuwa na uwezo," alisema.
Alisema waziri Muhongo amefikia hatua ya kuwagawa Watanzania katika ardhi yao kwa kutoa rasilimali zao kwa wazungu jambo ambalo ni hatari.
Aliongeza kuwa waziri huyo anapenda waje wazungu kutoa nje wachukue ardhi ya Tanzania ili Watanzania waachwe na kukaa pembeni.
Dk. Slaa ambaye wakati akizungumzia suala hilo alikuwa akishangiliwa na mamia ya wananchi waliohudhuria mkutano huo alisema, Mwalimu Nyerere alishawahi kusema madini yakikaa chini ya ardhi hayawezi kuoza kama ndizi.
Alisema kama Watanzania hawana uwezo na utaalam wa kuchimba gesi iachwe chini ya ardhi ili watoto wasomee na kuichima wenyewe kunufaisha watanzania wote badala ya wazungu anaowang’angania Waziri Muhongo.
Dk. Slaa alisema Waziri Muhongo na serikali yake wanataka kuwagawia wazungu ambao lengo lao la kutengeneza mabomba kutokea Mtwara kupitishia chini ya ardhi ili wauze Ulaya kabla Watanzania hawajanufaika nayo.
Alisema badala ya kutengeneza mabomba kwa ajii ya kuuza gesi Ulaya kuna haja kwa serikali ikajenga mabomba kila kijiji iweze kutumika na Watanzania wote.
Alisema Watanzania kama watachangia hata kama ni shilingi moja na kuunda kampuni wataweza kupata fedha za kuchimba gesi yao na ndiyo maana ya kujenga nchi.
“Mengi amekuwa akitetea rasilimali ya gesi kama mwenyekiti wa PSPF kwa hiyo ametanguliwa na wafanyabiashara wa Tanzania na hivyo hakuzungumza suala hilo kama Mengi mwenyewe,” alisema Dk. Slaa.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI