Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.
HISTORIA inaonyesha kwamba tumbaku ilivumbuliwa na mabaharia wa Kihispania kwenye fukwe za Marekani mwaka 1500 (BK). Kuanzia hapo, wafanyabiashara wa Kizungu waliichukua tumbaku hiyo kutoka Marekani na kuisambaza sehemu mbalimbali duniani walikokuwa wakifanya biashara zao.
Iliaminika kwamba tumbaku ni zawadi kutoka kwa Mungu. Moshi wa tumbaku uliotolewa nje baada ya kuvuta, ulidaiwa kuwa na uwezo wa kubeba mawazo/matakwa ya mvutaji pamoja na sala kwenda mbinguni. Aidha, tumbaku ilitumiwa kama dawa ya masikio, meno na mafua yatokanayo na baridi.
Aina za Tumbaku
Kwa sasa inaaminika kuwepo kwa aina sita za tumbaku.
1. BIDIS: Hizi ni aina ndogo ya sigara zilizotengenezwa kwa mkono, na hutumiwa sana katika nchi za Bara la Asia. Mtu anapovuta aina hii ya sigara hupata lami, nikotini na kaboni monoksidi nyingi zaidi kuliko sigara za kawaida.
2. BIRI: Hii ni aina ya sigara inayosokotwa kwa majani ya tumbaku au kwa kutumia karatasi iliyotengenezwa kwa tumbaku. Kwa kulinganisha na asidi ya tumbaku iliyo kwenye sigara, tumbaku iliyo kwenye biri hufanya nikotini iingie kupitia mdomo hata ikiwa biri haijawashwa.
3. KRETEKS. Hii ni sigara inayotengenezwa kwa mchanganyiko wa tumbaku na karafuu. Kwa kawaida asilimia 60 inakuwa ni tumbaku na asilimia 40 inakuwa ni karafuu. Mtu anapovuta aina hii ya tumbaku hupata lami, nikotini na kaboni monoksidi nyingi zaidi kuliko sigara za kawaida.
4. VIKO: Hii ni tumbaku aina ya kiko. Tumbaku husagwa na kuwekwa kwenye kiko kinachotengenezwa maalum kwa ajili ya kuvuta tumbaku na mara nyingi hupendelewa kutumiwa na watu wenye umri mkubwa na ina athari zilezile za sigara za kawaida.
ENDELEA KUSOMA MAKALA HII KWA KUBOFYA HAPA CHINI
5. UGORO. Hii ni tumbaku inayotumiwa moja kwa moja bila kutoa moshi. Aina hii hutumika kwa ama kwa kutafuna au kwa kunusa. Kwa hiyo nikotini yake huingia kwenye damu kupitia mdomoni. Ni hatari kutumia tumbaku hizo zisizokuwa na moshi kama tu tumbaku nyingine.
6. SHISHA. Hii ni tumbaku inayovutwa kupitia mvuke wa maji maji. Moshi wa Shisha unaovutwa, hupitishwa kwenye maji kabla ya kuvutwa. Hata hivyo, mbinu hiyo haipunguzi kiasi cha nikotini kilichomo ndani ya tumbaku na zaidi huweza kusababisha kansa mapafu.
Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), linazungumzia matumizi ya tumbaku kwa kusema: "Tumbaku inatumiwa katika njia nyingi tofauti-tofauti. Tumbaku huuzwa katika maduka yanayouza dawa na bidhaa za vyakula vya kuboresha afya. Hata hivyo, tumbaku ni hatari hata itumiwe kwa njia yoyote ya gani."
Uvutaji wa tumbaku una kemikali za sumu, kama vile nikotini, lami (tar), kaboni monoksidi, arsenic, benzopyrene na nyinginezo. Mvutaji anameza sumu hizi angalau kwa kiwango kidogo. Madhara yake yanajumuisha kufika wakati ambapo athari yake ni kuua kidogo kidogo viungo vya mwanadamu na nyama nyama (tissues) za mwanadamu. Mtu anaweza kufa kutokana na magonjwa yanayosababishwa na tumbaku kama vile kansa na magonjwa ya moyo.
Kwa mujibu wa ripoti za WHO, kwa kila sekunde nane, mtu mmoja hufariki dunia ulimwenguni kutokana na matumizi ya tumbaku. Inaaminika pia kwamba watu saba kati ya wavutaji tumbaku 10, huanza matumizi hayo wakiwa watoto.
Ripoti za shirika hilo zinasema kadri mtu anavyoendelea kuvuta tumbaku kwa muda mrefu, hufupisha urefu wa maisha yake kwa takruban miaka 20 hadi 25. Hiyo inatokana na sababu kwamba tumbaku ina aina za kemikali zipatazo 4,000 ambazo zina uwezo wa kudhuru afya ya binadamu. Uchunguzi unaonyesha kwamba zaidi ya asilimia 80 ya chembe za moshi unaovutwa hubakia mwilini.
Inaelezwa kwamba katika karne moja tu iliyopita, watu milioni zaidi ya milioni 100 walifariki dunia kutokana na uvutaji wa sigara.
Inaelezwa kwamba katika karne moja tu iliyopita, watu milioni zaidi ya milioni 100 walifariki dunia kutokana na uvutaji wa sigara.
Aidha, takwimu zilizopo zinaonyesha kwamba watu zaidi ya milioni sita hufariki dunia kila mwaka kwa sababu ya kuvuta sigara.
Wataalamu wanaonya kwamba ikiwa mambo hayatobadilika, kufikia mwaka 2030, uvutaji wa sigara utasababisha vifo vya watu zaidi ya milioni nane kila mwaka. Aidha, wanatabiri kwamba uvutaji wa sigara utasababisha vifo vya watu bilioni moja hivi kufikia mwisho mwa karne ya 21.
Wataalamu wanaonya kwamba ikiwa mambo hayatobadilika, kufikia mwaka 2030, uvutaji wa sigara utasababisha vifo vya watu zaidi ya milioni nane kila mwaka. Aidha, wanatabiri kwamba uvutaji wa sigara utasababisha vifo vya watu bilioni moja hivi kufikia mwisho mwa karne ya 21.
Athari za tumbaku zinaanzia kwa mkulima wa zao hilo, familia yake na hatimaye mvutaji na watu wanaokaa karibu na wavutaji nao. Upo ushahidi wa kutosha wa kisayansi kwamba moshi wa sigara usiokuwa wa moja kwa moja, husababisha magonjwa sawa kama sigara inayovutwa moja kwa moja, ikiwa ni pamoja na ugonjwa wa moyo na mishipa, mapafu na upumuaji (COPD).
Kutokana na hali hiyo, maelfu ya watu wasiovuta sigara nao hufariki dunia kila mwaka kutokana na kuishi au kukaa karibu na watumiaji wa tumbaku. Ndiyo maana WHO wanasema: "Moshi wa sigara unaweza kumdhuru mtu asiyevuta bila kujali kiwango cha moshi anachopumua."
Hivi sasa, hatari za kiafya za moshi wa tumbaku ni suala la makubaliano ya kisayansi, na hatari hizo zimekuwa moja ya motisha kubwa kwa ajili ya kupiga marufuku sigara katika maeneo ya kazi na ndani ya maeneo ya umma, ikiwa ni pamoja na mikahawa, baa na klabu za usiku.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Chama cha Wazuiaji Tumbaku Tanzania (CTCA), hakuna mkulima wa zao la tumbaku ambaye amenufaika na kilimo hicho. Badala yake, utafiti huo unabainisha kwamba wakulima wengi wa zao hilo wamechoka kiafya kutokana na maradhi ya ngozi, kansa na magonjwa ya kifua kikuu.
CTCA wanaamini kwamba kuendelea kuwepo kwa matangazo, promosheni na ufadhili wa bidhaa za tumbaku nchini kumesababisha ongezeko kubwa la matumizi ya tumbaku miongoni mwa vijana. Kwa mfano, utafiti uliofanywa mwaka 2008 na taasisi binafsi ya Global Youth Tobacco Survey, ulionyesha kuwa asilimia 1.06 ya wanafunzi mashuleni na vyuoni wanatumia bidhaa zinazotokana na tumbaku.
Baadhi ya athari za tumbaku katika mwili wa binadamu ambazo zimethibitishwa na wanasayansi ulimwenguni:-
Nywele– Uvutaji wa sigara hudhoofisha kinga ya mwili na kisha kudhuru mizizi ya nywele mapema.
Akili– Uvutaji sigara una madhara kwa akili ya mwanadamu na namna ya kuwasilisha hoja zake. Mtu ambaye ameathirika na sigara anapitia vipindi vibaya vya kuhitaji kuvuta sigara kila wakati na kumfanya kuwa mgumu wa kufikiri, kuwa makini, kusuluhisha tatizo au kufanya jambo lolote muhimu hadi avute sigara. Pale mtu anapovuta sigara, misuli yake inajiachia na anapata kipindi cha mapumziko mafupi ya kutokwa na akili yanayogubika tatizo lililomkumba, lakini baada ya hapo mvutaji anaweza kupatwa na maumivu ya kichwa na kizunguzungu.
Aidha, tumbaku husababisha uraibu (addiction). Kemikali aina ya nikotini katika tumbaku husisimua na vile vile hutuliza hisia. Wanasayansi wamegundua kwamba nikotini hiyo huongeza kiwango cha homoni za mkazo. Lakini pia, kemikali hiyo humfanya mvutaji ajisikie vizuri wakati anavuta sigara, na zaidi humpa mvutaji msongo wa mawazo na kushuka moyo pindi anapomaliza kuvuta sigara.
Kuvuta sigara hupeleka nikotini haraka kwenye ubongo tena na tena. Inaelezwa kwamba pafu (mvuto) moja la sigara, ni sawa na dozi moja, hivyo mvutaji wa kawaida anaweza kuvuta dozi 200 kwa siku, ambacho ni kiwango cha juu kuliko dawa yoyote ile. Ndiyo maana nikotini husababisha uraibu mkubwa zaidi. Mtu aliyezoea kuvuta sigara hujihisi vibaya anapokawia kuvuta.
Macho– Wavutaji wa sigara hupata magonjwa ya macho mara nyingi kuliko wasiovuta. Sehemu ya macho inayopitisha mwangaza inaweza kufichwa kama vile wingu linavyoficha jua na kusababisha upofu. Ugonjwa huu husababishwa kwa njia mbili. Kwanza moshi wa sigara huwasha macho, na pili; kemikali zilizo ndani ya sigara hupita kwenye mishipa ya damu na hatimaye kudhuru macho. Sigara pia husababisha kudhoofika kwa sehemu ya kati ya macho (retina) na hivyo kupunguza uwezo wa macho kuona vizuri na hata kutofautisha rangi (macular degeneration).
Ngozi– Uvutaji tumbaku husababisha kukauka kwa ngozi, kubadilika rangi ya ngozi na kuwa njano pamoja na kukunjamana kwa ngozi. Sigara huleta magonjwa mengi ya ngozi kama vile uvimbe, kuwashwawashwa na kudhoofisha hali ya ungaavu wa ngozi. Kemikali zinazopatikana ndani ya sigara hupunguza uwezo wa ngozi kujirekebisha, hivyo ngozi huzeeka haraka na kupoteza uwezo wa kulainika. Mvutaji wa sigara huonekana mzee zaidi kuliko umri wake.
Aidha, harufu mbaya ya moshi huganda katika ngozi. Uvutaji sigara unasababisha saratani ya ngozi. Kemikali za sigara husababisha vidonda kwenye ngozi na ambavyo haviponi kwa urahisi, ma wakati mwingine huweza kugeuka na kuwa saratani.
Masikio– Uvutaji sigara huweza kusababisha magonjwa ya masikio. Sababu ni kwamba uvutaji wa sigara husababisha uchafu kuganda kwenye mishipa ya damu, na hivyo kupunguza mwendo wa damu hadi kwenye sehemu za ndani za masikio. Moshi na kemikali za tumbaku pia hujeruhi sehemu za ndani za masikio na majeraha hayo yanaweza kuambukiza hata ubongo (meningitis) na hatimaye kusababisha uziwi.
Kinywa– Tumbaku hutatiza mdomo na kuongeza uchafu unaoganda kwenye meno, hivyo kusababisha kuoza kwa meno na harufu mbaya mdomoni. Tumbaku huathiri chembechembe za kinywa zinazotumika kuonja ladha ya chakula, hali inayowasababishia watumiaji wa tumbaku kushindwa kufurahia vizuri ladha ya vyakula.
Aidha, tumbaku husababisha fizi za kinywa kutokwa na damu, na wakati mwingine husababisha kushindwa kupona kwa vidonda mdomoni, hasa baada ya kung'olewa kwa jino. Saratani za mdomo, ulimi na koo zinapatikana zaidi kwa wavutaji sigara na watumiaji wa tumbaku za aina nyingine.
Mapavu– Wavutaji wa tumbaku hupata taabu ya kupumua kwa kuwa uvutaji huharibu mapafu. Uvutaji husababisha kukohoa na kutoa malenda-lenda pamoja na magonjwa ya mapafu (emphysema & chronic bronchitis). Endapo mvutaji ana ugonjwa wa pumu, anaweza kuongeza hatari zaidi ya kubanwa kifua na kuishiwa pumzi.
Uvutaji wa sigara ndiyo sababu kubwa zaidi ya saratani ya mapafu, na pia husababisha kupasuka kwa vibifu vya hewa safi na kutoa harufu mbaya mwilini. Wavutaji pia hupata saratani ya koromeo na kuziba njia ya hewa, na hivyo inabidi kutobolewa kwa kishimo kwenye shingo ili kuwezesha mgonjwa kupumua.
Nyama za mwili na mifupa– Tumbaku husababisha mzunguko wa damu na hewa safi, kwa maana ya oksijeni kupungua kwenye nyama za mwili na hivyo kusababisha maumivu ya nyama na viungo pale mvutaji anapofanya mazoezi au anapokuwa michezoni.
Sigara inasababisha mifupa kuwa mnyepesi na kupunguza nguvu. Sababu ni kwamba kemikali zilizoko ndani ya sigara, hupunguza uwezo wa mwili kujenga mifupa iliyo na nguvu. Mifupa kama hii huvunjika kwa urahisi na kuchukua muda mrefu kupona, hivyo kusababisha magonjwa ya mifupa kama vile ‘Rhematoid Arthritis.’
Sigara inasababisha mifupa kuwa mnyepesi na kupunguza nguvu. Sababu ni kwamba kemikali zilizoko ndani ya sigara, hupunguza uwezo wa mwili kujenga mifupa iliyo na nguvu. Mifupa kama hii huvunjika kwa urahisi na kuchukua muda mrefu kupona, hivyo kusababisha magonjwa ya mifupa kama vile ‘Rhematoid Arthritis.’
Moyo– Tumbaku ni chanzo kikuu cha magonjwa ya moyo. Uvutaji wa tumbaku huharibu mishipa ya damu, hufanya mishipa kuvimba na kufanya upenyo wa damu kuwa mdogo. Hali hii husababisha moyo kusukuma damu kwa nguvu na kasi kubwa kuliko kawaida na hivyo kusababisha shinikizo la damu kupanda (High Blood Pressure). Hata kwa wale wanaovuta sigara chini ya tano kwa siku, wako katika hatarini pia kupata magonjwa ya moyo.
Aidha, uvutaji tumbaku husababisha damu kuganda kwenye mishipa ya damu na kuzuia mzunguko wa damu hadi kupelekea mshtuko wa moyo(Heart attack) tatizo linaloweza sababisha kifo cha ghafla. Moja kati ya kila vifo vitatu ulimwenguni hutokana na magonjwa ya moyo na huua zaidi ya watu milioni moja kwenye nchi za Afrika. Kiharusi/Kupooza(Stroke) kinaweza tokea endapo damu itaganda kwenye mishipa ya damu ya kichwa na kuzuiia mzunguko wa damu kichwani au pale mishipa inapozidiwa na kupasuka.
Tumbo – Sigara hupunguza uwezo wa mwili kujikinga dhidi ya viini vinavyosababisha vidonda tumboni. Pia hupunguza uwezo wa tumbo kustahimili nguvu ya asidi baada ya kula. Vidonda vya mvutaji huwa ni vigumu kutibu na mara nyingi hutokea tena baada ya kupona.
Vifole na Kucha– Tumbaku husababisha kutu inayokusanyika na kuganda kwenye kucha na vidole vya mvutaji, na hivyo kusababisha kubadilika kwa rangi ya vidole na kucha kuwa manjano au maji ya kunde. Ngozi ya vidole pia hukauka na kuwa ngumu kwa sababu ya joto na kemikali za sigara.
Mishipa ya Damu– Uvutaji tumbaku husababisha ugonjwa ambao kitaalam unajulikana kama ‘Buerger's Disease.’ Huu ni ugonjwa wa uvimbe kwenye mishipa ya damu ya miguuni na mikononi. Mishipa hii huzibwa na kuzuia mwendo wa damu kwenye sehemu zilizoathirika. Isipotibiwa kwa haraka, mvutaji anaweza kukatwa miguu au mikono.
Afya ya uzazi kwa mwanamke– Uvutaji tumbaku hupunguza nafasi za mwanamke kushika mimba na kuharibu DNA kwenye shahawa za mwanaume. Ni vigumu zaidi kwa mwanamke mvutaji sigara kutunga mimba na ni rahisi sana kwake kumpoteza mtoto wakati wa kulea mimba (Miscarriage). Uvutaji wa sigara pia hufanya mwanamke kuzaa mtoto iyekufa (Stillbirth) au aliye na kasoro kama uzito usiotimia wa kawaida. Watoto hawa huwa na afya duni baadaye kwa sababu ya kemikali za sigara ambazo hupunguza mwendo wa mtoto kukua akiwa angali mimbani.
Aidha, sigara husababisha ugumba (menopause) kabla ya wakati wake. Sigara inaweza kumfanya mwanamke kuwa tasa. Na pia sigara huongeza hatari ya kupata saratani ya fuko la uzazi (Cancer of the uterus).
Afya ya uzazi kwa mwanaume– Uvutaji wa tumbaku unapunguza msukumo wa damu kwenye sehemu za uume. Sigara pia huharibu mbegu za kiume, na kwa hiyo watoto wanaozalishwa huwa na uwezekano mkubwa wa kuwa na kasoro za maumbile na kupata magonjwa ya saratani. Sigara pia huweza kuwasababishia wanaume wawe tasa.
Saratani– Zaidi ya kemikali 40 zinazopatikana kwenye tumbaku zimethibitishwa kusababisha magonjwa ya saratani kwa mvutaji, ikilinganishwa na asiyevuta sigara. Utafiti uliofanywa na Taasisi ya Saratani ya Ocean Road mwaka 2010/2011, umebainisha kwamba zaidi ya asilimia 30 ya saratani zote, zinahusishwa moja kwa moja na matumizi ya tumbaku na hivyo kuigharimu Serikali zaidi ya dola za Marekani milioni 40 kuhudumia wagonjwa wa saratani.
Kisukari– Uvutaji sigara husababisha aina ya pili ya kisukari (Type 2 Diabetes Mellitus), na hufanya kuwa vigumu kudhibitiwa. Hatari ya kupata kisukari ni asilimia 30-40 kwa wavutaji, ikilinganishwa na wasiovuta. Endapo mvutaji ana ugonjwa wa kisukari, anaongeza mara mbili hadi tatu hatari ya kupata ugonjwa wa figo. Pia wavutaji wenye kisukari wana hatari zaidi ya magonjwa ya moyo, macho na mfumo wa fahamu.