“Ni kwamba abiria wengi na mabasi ni machache, lakini hakuna mgomo baridi,” PICHA|MAKTABA
Dar es Salaam. Hali ya usafiri kwenye kituo kikuu cha mabasi yaendayo mikoani na nchi jirani cha Ubungo (UBT) ni mbaya hasa kwa mabasi yanayokwenda Kilimanjaro na Arusha.
Hali hiyo imesababisha Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), kuruhusu mabasi madogo aina ya ‘Coaster’ kusafirisha abiria wanaokwenda mikoa hiyo.
Pamoja Sumatra kuruhusu magari hayo kusafirisha abiria kwenda mikoa hiyo, kumeibuka malalamiko kutoka kwa baadhi ya abiria wakidai kutozwa nauli kubwa kuliko iliyoelekezwa.
Abiria wanadai kutozwa kati ya Sh35,000 hadi 40,000 badala ya Sh20,000 hadi 25,000 kwa mtu mmoja.
ENDELEA KUSOMA HABARI HII KWA KUBOFYA HAPA CHINI
Mwananchi ilishuhudia umati wa abiria kituoni hapo asubuhi ya jana, huku kukiwa na habari zisizo rasmi kuwa kuna mgomo baridi kwa baadhi ya mabasi baada ya kubanwa kutopandisha nauli.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti abiria hao walidai kuwa hali ya usafiri UBT ni mbaya kutokana na uhaba wa mabasi.
Moja ya abiria Joseph Masawe, aliyepanga kusafiri kwenda Kilimanjaro alisema: “Bora waandishi mmefika mjionee wenyewe hali mbaya ya hapa Ubungo. Abiria ni wengi na mabasi hakuna.”
Aliongeza: “Pamoja na shida hii ya usafiri, bado tunapandishiwa nauli kupita kiasi. Ukitaka kuigusa Coaster lazima uwe na Sh35,000 au Sh40,000.”
Abiria mwingine Emmanuel Musa alisema: “Tunahisi huenda kukawa na mgomo baridi baada ya wenye mabasi kutakiwa kutopandisha nauli, kwani tunashangaa hakuna mabasi ya Arusha na Kilimanjaro.” Akizungumzia suala hilo Ofisa Leseni anayeshughulika na ukaguzi wa mabasi kituoni hapo, Sebastian Lohay alisema kutokana na wingi wa abiria wametoa vibali kwa wenye ‘Coaster’ kusafirisha abiria kwenda Mikoa ya Kaskazini.
“Ni kwamba abiria wengi na mabasi ni machache, lakini hakuna mgomo baridi,” alisema Lohay alipoulizwa kama kukosekana mabasi hayo ni kutokana na kuwepo kwa mgomo baridi.
Kuhusu kupandishwa kwa nauli, alisema: “Ni kweli kuna baadhi ya mabasi madogo Coaster yamekuwa yakitoza nauli tofauti na iliyoelekezwa, na wanaofanya hivyo tukiwabaini tunawakamata na kuwatoza faini.”
Naye Ofisa wa Chama Cha Kutetea abiria (Chakua), Gervas Rutaguzinda alisema watu wenye mabasi madogo wamekuwa wakipandisha nauli na kuwataka abiria kutotoa taarifa.
“Hali ni mbaya, nauli zipo juu abiria wamekuwa wakilalamika, lakini cha kusikitisha ni kwamba hawa wenye mabasi wanawatisha abiria kuwa wakitoa taarifa za kupanda kwa nauli watasitisha safari zao,”alisema.
MWANANCHI