Watu saba wanashikiliwa na Jeshi la kwa tuhuma za mauaji ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mwanza, Clement Mabina (56 - pichani). Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Valentino Mlowola, alithibitisha kukamatwa kwa watuhumiwa hao wakati akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu jana mchana. “Hadi sasa tunawashikilia watu saba kwa tuhuma za kuhusika katika mauaji hayo. Hata hivyo, msako bado unaendelea ili kubaini iwapo kuna watu wengine zaidi waliohusika kwenye mauaji hayo ya kinyama,” alisisitiza Kamanda Mlowola.
Alisema watuhumiwa hao wote ni wakazi wa Kata ya Kisesa wilayani Magu na kwamba hakuwa tayari kuwataja majina kwa maelezo kuwa ni kuepuka kuingilia upelelezi.
Mlowola, alisema taratibu zikikamilika watuhumiwa hao na wengine watakaomatwa watafikishwa mahakamani kujibu mashtaka.
ENDELEA KUSOMA HABARI HII KWA KUBOFYA HAPA CHINI
Alisema bunduki inayodaiwa kutumika kumuua mwanakijiji Temeli Malemi ni Shortgun na siyo bastola na kwamba ilikuwa mapema kutoa ufafanuzi kutokana na mazingira ya tukio hilo huku akikemea wananchi kujichukulia sheria mikononi.
Mabina ambaye alikuwa mwana-CCM maarufu mkoani hapa na Diwani wa Kata ya Kisesa wilayani Magu, aliuawa baada ya kushambuliwa na wakazi wa kijiji cha Kisesa wakati akiwa katika kitongoji cha Kinyama juzi kati ya saa 3 na saa 4 asubuhi kwa kushambuliwa kwa mawe na silaha nyingine za jadi hadi kufa kutokana na mgogoro wa ardhi uliokuwa ukiendelea baina yake na baadhi ya wakazi wa maeneo ya kijiji hicho.
WATU WAKIMBIA MAKAZI
Katika hatua nyingine, wakazi kadha wakiwamo wanaume na vijana, wanadaiwa kukimbilia mafichoni kukwepa mkono wa sheria na msako mkali wa polisi unaiendelea dhidi ya walioshiriki mauaji hayo ya kikatili.
Hatua hiyo inatokana na msako huo ulioanza tangu juzi kuendelea kwa kasi. Mwandishi wa habari hizi aliyetemlea kijijini hapo jana asubuhi alishuhudia askari waliovalia sare za polisi makachero wakiendesha msako huo.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kwenye eneo la tukio, baadhi ya wananchi wamedai kuwa baadhi ya wanaume na vijana wamekimbia makazi yao tangu juzi ili kukwepa kukamatwa na polisi.
Mabina aliuawa wakati akijaribu kujihami kwa kufyatua risasi hewani baada ya kuzungukwa na watu wengi waliokuwa wamebebea silaha yakiwamo mawe na mapanga.Wakati alikajaribu kujihami kwa kufyatua risasi hewani, inadaiwa ilimuua Malemi.
MAZISHI KESHO AU ALHAMISI
Wakati huo huo; Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Magu, Isack Zablon, amesema mwili wa Mabina unatarajiwa kuzikwa kati ya kesho na keshokutwa nyumbani kwake katika kijiji cha Kisesa.
“Hapa nilipo ninajiandaa kwenda kwenye kikao cha mazishi, lakini pia bado tunasubiri mtoto wa marehemu ambaye yuko jijini Dar es Salaam awasili,” alisema.
Mabina alikuwa diwani na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu mwaka 2000 -2005. Mwaka 2007-2012 alikuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza.
Aligombea tena uenyekiti wa mkoa huo katika uchaguzi wa mwaka 2012 na kubwaga na Mwenyekiti wa sasa, Anthony Diallo.
CHANZO: NIPASHE