Dodoma/Dar es Salaam. Wabunge 160 wa CCM wamejiorodhesha kuomba kuitishwa kwa kikao cha Kamati ya Wabunge hao kwa lengo la kuwajadili mawaziri wanaotajwa kuwa mizigo.
Pia wabunge hao wanataka Katibu Mkuu wa CCM, Abdurahaman Kinana naye awepo kwenye kikao hicho.
Mjumbe wa Kamati ya Uongozi wa Kamati ya Wabunge wa CCM, Hussein Mussa Mzee, alimwambia mwandishi wetu kuwa wamepokea barua iliyoambatana na orodha ya majina ya wabunge zaidi ya 160 waliotia saini kutaka kuitishwa kwa kikao hicho.
“Hata kama wangesaini wabunge 10 tu tungeitisha kikao. Bahati nzuri walisaini zaidi ya 160, kwa hiyo kikao kitaitishwa kwa kuwa ni haki yao kikanuni kutaka kukutana,” alisema.
ENDELEA KUSOMA HABARI HII KWA KUBOFYA HAPA CHINI
Alipoulizwa kwa nini kikao hicho hakikuitishwa ndani ya wiki moja ambao ndiyo muda wabunge hao walioutaka kabla ya Kamati Kuu ya CCM kukutana wikiendi iliyopita, Mzee alisema hiyo lilitokana na Mwenyekiti wa Kamati ya Wabunge wa CCM, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, kutokuwapo bungeni.
Mzee alisema pia kikao hicho kilishindwa kufanyika mara ya kwanza kutokana na Kinana kuwa safarini Afrika Kusini ambako alihudhuria mazishi ya Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Nelson Mandela.
Hata hivyo, alisema hawezi kujua ni lini kikao hicho kitafanyika lakini aliahidi kuwa itakuwa mara baada ya Kinana kurejea nchini.
Wiki iliyopita, gazeti hili liliandika kuhusu wabunge wa CCM kujiorodhesha ili kushinikiza kufanyika kwa kikao hicho.
Chanzo kimoja cha kuaminika kilisema kuwa fomu hiyo iliwasilishwa katika Ofisi ya Katibu wa Wabunge wa CCM ikiambatana na barua inayotaka kuitishwa kwa kikao kitakachowakutanisha.
“Tuliwaomba waitishe kikao cha wabunge wa CCM ili mawaziri ambao tunawaona hawatimizi majukumu yao kikamilifu waweze kuhojiwa lakini wakawa wanasuasua,” kilisema chanzo hicho.
Kikao hicho kilitakiwa kufanyika Alhamisi iliyopita ili kuwahoji mawaziri hao kabla ya kikao cha Kamati Kuu.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alikaririwa wikiendi hii akieleza kuwa mawaziri saba walihojiwa katika kikao cha Kamati Kuu na kumuachia Rais Jakaya Kikwete jukumu la kuamua kuwafukuza kazi, kuwahamisha au kuwataka kutekeleza majukumu yao kikamilifu.
Miongoni mwa mawaziri waliohojiwa ni Naibu Waziri wa Fedha, Saada Mkuya na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Hawa Ghasia.
Tayari Bunge limepitisha azimio la kumtaka Ghasia pamoja na Manaibu wake wawili, Aggrey Mwanri na Kassim Majaliwa kupima na kutafakari kama wanatosha kusimamia wizara hiyo.
Kiini cha Bunge kupitisha azimio hilo ni taarifa ya Bunge ya Hesabu za Serikali kubainisha kuwapo wizi, ubadhirifu na mtandao wa ufisadi ndani ya Tamisemi, kwenye halmashauri na Hazina.
Vuguvugu linaloendelea hivi sasa la wabunge wa CCM, liliwahi kujitokeza katika Bunge la Aprili mwaka jana na kumlazimisha Rais Kikwete kupangua Baraza lake Mawaziri Mei 4, 2012 kwa kuondoka mawaziri sita kutokana na taarifa za kamati za kudumu za Bunge na ile ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Sefue aweka msimamo
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue amewataka mawaziri saba wanaotuhumiwa kushindwa kutekeleza majukumu yao kueleza mikakati ya utekelezaji wa majukumu hayo kama ilivyodaiwa, badala ya kuiachia Serikali kufanya hivyo.
Balozi Sefue alitoa wito huo jana alipoulizwa msimamo wa Serikali baada ya Kamati Kuu ya CCM chini ya uenyekiti wa Rais Kikwete, Alhamisi na Ijumaa iliyopita kuwahoji mawaziri hao waliodaiwa kuwa ni mzigo, kueleza upungufu wao huku kamati hiyo ikimshauri Rais Kikwete hatua za kuwachukulia.
“Wanaohusika ni mawaziri kutoka wizara mojamoja hivyo wao ndiyo wanaoweza kulizungumzia kwa undani suala hilo, ikiwa ni pamoja na mipango na mikakati yao ya kurekebisha matatizo.”
Ghasia anena
Waziri Ghasia amesema hakuna anayepaswa kunyooshewa kidole kwa matatizo yaliyopo Tamisemi.
Akifungua warsha ya kujadili changamoto za uongozi wa Serikali za Mitaa jana mjini Dodoma, Ghasia alisema kwa sasa kazi kubwa iliyoko ni kurekebisha kasoro baada ya kufanyika utafiti juu ya matatizo ya Tamisemi.
Alisema wizara yake inashughulikia matatizo hayo baada ya kupokea ripoti ya utafiti uliofanywa na Taasisi ya Uongozi (Uongozi Institute).
“Kiongozi anapaswa kuwa mbunifu anayeweza kuongoza wakati kunapokuwa na changamoto, anapaswa aone mbali zaidi ya wengine. Hatutarajii tuwe na kiongozi anayeongoza katika mazingira yasiyokuwa na changamoto kabisa,” alisema Ghasia.
Imeandikwa na Sharon Sauwa, Israel Mgussi na Fidelis Butahe.
MWANANCHI