*Mahasimu wamvaa ndani na nje ya Chadema
*Atamba kuushangaza mtandao unaomwinda
*Katibu wa Bunge amtetea, ampinga Werema
JINA la Zitto Kabwe, mwanasiasa kijana ambaye mvumo wa sifa zake umechukua mwelekeo tofauti katika siku za hivi karibuni, limeendelea kutawala mwenendo wa siasa za kitaifa kwa wiki ya tatu mfululizo sasa.
Zitto, mmoja wa wabunge vijana ambao wametokea kuwa na ushawishi mkubwa ndani na nje ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambacho yeye ni mwanachama wake amejikuta akikabiliwa na tishio la kuanguka au kuangushwa kisiasa na makundi ya mahasimu wake ambayo yanaonekana kujipanga kummaliza.
Wakati hatma ya kisiasa ya mwanasiasa huyo ikiendelea kubakia kuwa kitendawili tangu Kamati Kuu ya Chadema itangaze kumvua nyadhifa zake zote za kisiasa siku 22 zilizopita, wiki hii Zitto alijikuta akikabiliana na mashambulizi makali ya maneno na misuto ndani ya Bunge.
Kinara wa mashambulizi ya safari hii dhidi ya Zitto alikuwa ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema ambaye mbali ya kumwita Zitto mwongo alikwenda mbele zaidi na kutoa tishio la kuchukuliwa kwa hatua za kisheria dhidi ya mbunge huyo.
ENDELEA KUSOMA HABARI HII KWA KUBOFYA HAPA CHINI
Werema alitoa kauli hizo za mashambulizi na vitisho kutokana na kauli iliyotolewa na Zitto bungeni aliyeituhumu serikali kwa kutokuonyesha kuwa na nia ya dhati katika kuhakikisha kuwa, fedha zilizofichwa nje ya nchi na baadhi ya Watanzania zinarejeshwa.
Akijibu kauli hiyo ya Zitto, Werema alimshambulia mwanasiasa huyo kwa kushindwa kutoa ushirikiano wa kutosha kwa kamati iliyoundwa na serikali kulifuatilia suala hilo.
Werema ambaye misimamo yake ndani ya Bunge katika siku za karibuni imekuwa ikiibua utata mkubwa alifikia hatua ya kumtuhumu Zitto kwa kukiri akiwa chini ya kiapo kwamba, alikuwa hana majina ya watu walioficha mabilioni ya fedha katika akaunti nchini Uswisi, kinyume na kauli ambazo amekuwa akizitoa ndani ya Bunge.
Kwa sababu hiyo basi, Jaji Werema aliliambia Bunge kuwa serikali ilikuwa ikitafakari namna ya kuchukua hatua za kisheria dhidi ya Zitto kwa madai kwamba mbunge huyo alilidanganya Bunge kwa kudai kuwa ana majina ya watu wanaodaiwa kuficha fedha na mali haramu nje ya nchi wakati si kweli.
“Katika hili, nawashukuru wabunge 87 waliofika mbele ya kamati, nawashukuru wananchi wengine waliofika kwani sasa tumefika pazuri ila serikali inaomba iongezewe miezi sita ili ikamilishe jambo hili lakini hili suala la Zitto tutashughulika nalo kisheria kwa sababu huwezi kulidanganya Bunge halafu ukaachwa,” alikaririwa Jaji Werema akiliambia Bunge.
Kama ilivyokuwa kwa Werema, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema) alionekana kutumia fursa hiyo kumshambulia Zitto ndani ya Bunge akimtaka mwanachama huyo mwenzake wa Chadema na Mwanasheria Mkuu wa Serikali “kutochezea akili za Watanzania katika sakata hilo.”
Lema ambaye siku chache tu kabla ya Kamati Kuu ya Chadema haijachukua uamuzi wa kumvua Zitto nafasi zote za uongozi aliingia katika mzozo na mwanasiasa huyo, alikwenda mbele zaidi na kutaka apewe yeye majina ya watu hao walioficha fedha Uswisi ili aweze kuwataja.
Akizungumza na Rai Jumapili jana, Zitto alieleza kushangazwa na kauli hizo akisema zilikuwa zimebeba kile ambacho alipata kukieleza kuhusu kuundwa kwa mtandao wa kuhakikisha unammaliza na kuzima kabisa hoja yake ya ukwapuaji wa mabilioni ya fedha za umma.
“Nilipata kulisema hili la kuundwa kwa mtandao wa kunimaliza. Sasa hivi kila mtu ambaye amepata kuumizwa na Zitto anajitokeza kunishambulia. Katika kundi hilo iko mitandao ya urais wa mwaka 2015 ambayo inaundwa na watu walioficha fedha Uswisi na kwingineko nje ya nchi,” alisema Zitto.
Mbali ya hilo, Zitto alieleza kusikitishwa na kile alichokieleza kuwa ni uongo wa wazi wa Jaji Werema bungeni akisema alikuwa hajawahi hata mara moja kuhojiwa na kamati iliyoundwa na serikali kufuatilia suala hilo akiwa chini ya kiapo.
“Siku zote nimekuwa nikikataa kuhojiwa na kamati nje ya maeneo ya Bunge ili kuwa na kinga kwa kile nitakachosema. Kwanza sijapata kuhojiwa nikiwa chini ya kiapo. Ni kwa sababu hiyo wiki ijayo nitafanya kila niwezalo ili kueleza ukweli kuhusu jambo hili,” alieleza Zitto.
Hakuishia hapo, Zitto alieleza kulipuuza tishio la Jaji Werema kuhusu yeye kuchukuliwa hatua za kisheria kwa kusema uongo, akisema hoja ya mabilioni ya Uswisi si yake ingawa ni yeye aliianzisha kwani tayari ilishachukuliwa na kuwa Azimio la Bunge.
“Mtafuteni Katibu wa Bunge alieleze hili la miye kushitakiwa. Ni Umbumbumbu kushangilia hoja ya Werema. Nawashangaa wanaoshangilia uongo ule. Hoja ya mabilioni ya Uswisi si yangu tena ni ya Bunge.
“Huu ni wakati ambao mwanasiasa anakomazwa, sitetereki hata kidogo. Nitawashangaza wanaoshangilia hoja za uongo za Jaji Werema,” alisema Zitto kwa kujiamini.
Rai Jumapili lilipomtafuta Katibu wa Bunge, Thomas Kashililah na kumuuliza kuhusu sakata hilo na tamko la Werema dhidi ya Zitto alieleza kushangazwa na upotoshwaji unaofanywa.
“Hapa hakuna hoja ya Zitto. Nadhani lipo tatizo la uelewa katika masuala ya Bunge. Suala la mabilioni ya Uswisi ni Azimio Namba 9 la Bunge,” alisema Kashililah.
Gazeti hili lilipotaka aeleze maoni yake basi kuhusu kauli ya Werema kwanza alikataa kusema ilikuwa ni ya ukweli au uongo bali aliifananisha hoja hiyo na ile hoja ya migogoro ya ardhi iliyotolewa na Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema) ambayo nayo ilichukuliwa na kuwa ya Bunge baada ya kuridhiwa na kupitishwa.
Ingawa si rahisi kueleza moja kwa moja kuhusu usahihi au upotoshaji wa hoja ya Werema, ni wazi hoja yake alikuwa akiielekeza katika Kanuni za Kudumu za Bunge, Sehemu ya tano, Kifungu cha 64 (a) ambacho kinakataza mbunge kutoa taarifa ambazo hazina ukweli ndani ya Bunge.
Kwa mujibu wa kitabu cha kanuni za Kudumu za Bunge, sehemu ya sita, kanuni ya 73 (3) inatoa mamlaka kwa spika kumsimamisha mbunge kuhudhuria vikao visivyozidi vitano vya Bunge.
Katika kitabu hicho chicho cha kanuni ya 74 (5) inaipa Bunge mamlaka ya kuchukua hatua nyingine za kinidhamu, ikiwa ni pamoja na kumsimamisha kazi mbunge yeyote aliyetenda kosa chini ya kanuni hii.
Nje ya mwenendo na kanuni za Bunge kauli za Lema na Werema dhidi ya Zitto, zinatoa taswira kwamba mbunge huyo anapita katika nyakati za hatari kisiasa.
Ni wazi kwamba, Werema kwa kujua au kutojua, kwa kukusudia au kwa bahati mbaya alitoa kauli ile huku akijua ilikuwa ikichochea moto dhidi ya Zitto ambaye kwa sasa yuko katika uhusiano mbaya na viongozi wenzake kadhaa wakuu ndani ya Chadema.
Sakata la vigogo wanaodaiwa kuficha mali na fedha haramu nje ya nchi limezua mjadala mkubwa nchini huku serikali ikichukua muda mrefu kuwasilisha ripoti katika mikutano takribani minne ya Bunge kama ilivyoahidi na sasa imeomba miezi sita zaidi kufanyia kazi suala hilo.
Tangu Zitto awasilishe hoja hiyo Novemba mwaka jana, na serikali kuchukua hatua ya kuunda kamati ya kuchunguza, suala hilo limeonekana kuwagusa watu mbalimbali ambapo miongoni mwa watu wanaotajwa kuhojiwa mpaka sasa ni pamoja na wafanyabiashara wakubwa nchini akiwamo Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe na Mbunge wa zamani ya Igunga, Rostam Azizi.