Jeneza lililobeba mwili wa aliyekuwa Rais wa Kwanza Mzalendo wa Afrika Kusini, Nelson Mandela lilipofikishwa Uwanja wa Ndege wa Mthatha jana. Maziko yanafanyika leo kijijini kwao, Qunu kwa taratibu za kimila. PICHA | AFP
Qunu. Huzuni na simanzi viliyateka maeneo ya Mthatha na Qunu katika Jimbo la Eastern Cape, Afrika Kusini baada ya kuwasili kwa mwili wa rais wa kwanza mzalendo wa nchi, Nelson Mandela.
Mwili wa Mandela uliwasili jana katika Uwanja wa Ndege wa Mthatha saa 7:40 mchana (kwa saa za huku) dakika 20 kabla ya muda uliotarajiwa, ukiwa umesafirishwa kutoka Uwanja wa Ndege wa Jeshi wa Waterkloof, Pretoria.
Ulisindikizwa na maofisa waandamizi wa Jeshi la Afrika Kusini (SANDF), maofisa kutoka Serikali, wawakilishi wa familia yake na viongozi wa mila kutoka kabila la abaThembu.
ENDELEA KUSOMA HABARI HII KWA KUBOFYA HAPA CHINI
Mandela anazikwa leo katika makaburi ya familia yaliyopo katika Kijiji cha Qunu ambako alikulia, katika mazishi ambayo yatakuwa mchanganyiko wa mila na desturi, dini yake ya Kikristo ikifuata taratibu za kimethodisti na kijeshi kwa maana ya Serikali,
Alizaliwa katika Kijiji cha Mvezo, Julai 18, 1918 na alifariki dunia Desemba 5, mwaka huu nyumbani kwake, Houghton, Johannesburg akiwa na umri wa miaka 95 baada ya kuugua magonjwa ya figo kwa zaidi ya mwaka mmoja.
Maziko yake yanamaanisha kuhitimishwa kwa siku 10 za maombolezo ya kitaifa, ambayo yalishuhudia mamia ya viongozi kutoka pande zote za dunia, waliofika Afrika Kusini kushiriki Ibada ya Kitaifa iliyofanyika katika Uwanja wa FNB, Soweto Jumanne iliyopita.
Kadhalika mwili wa kiongozi huyo kwa siku tatu mfululizo; Jumatano hadi Ijumaa wiki hii ulikuwa ukiwekwa katika Ikulu ya Pretoria iliyopo Majengo ya Umoja (Union Buildings) ambako waombolezaji zaidi ya 100,000 walipata nafasi ya kutoa heshima zao za mwisho.
Serikali ya Afrika Kusini imetaganza kuwa leo ni siku ya mapumziko huku wamiliki wa maduka makubwa nao wakitangaza kwamba hawatafungua biashara zao kama hatua ya kuienzi siku ya mwisho ya Mandela.
Rais Jakaya Kikwete na Rais wa Malawi, Joyce Banda ni wakuu wa nchi pekee ambao watahudhuria mazishi ya Mandela na wote wamepangiwa kutoa salaamu za rambirambi wakati wa mazishi. Watawaongoza viongozi wengine kadhaa wakiwamo wale wanaowakilisha mashirika ya kimataifa.
Simanzi uwanjani
Uwanja wa Ndege wa Mthatha ulikuwa kimya hasa baada ya ndugu wa karibu wa Mandela, wakiongoza na mjane Graca Machel kuwasili saa 6:44 mchana na kulakiwa na viogozi mbalimbali wakiongozwa na Waziri wa Ulinzi, Nosiviwe Mapisa Nqakula.
Mara baada ya jeneza kushushwa kutoka kwenye ndege ya jeshi Namba C-130, wimbo wa taifa ulipigwa, pia kupokea heshima kutoka kwa askari wa SANDF ambao walikuwa uwanjani hapo mapema.
Kabla ya safari ya Mthatha, mtalaka wa Mandela, Winnie Medekileza alikuwa akimsaidia Graca kwa kumshika na wakitembea pamoja taratibu, ambaye alikuwa katika majonzi makubwa.
Safari ya kwenda Qunu ilianza saa 8:15 kwa msafara uliokuwa na magari yapatayo 100. Vijana wa ANC walikuwa wamejipanga pembezoni mwa barabara wakiwa wametengeneza uzio wa kuwazuia watu wasiingie barabarani wakati msafara huo ukiwa unapita.
Inakadiriwa kuwa vijana hao ni zaidi ya 6,500 na walijipanga umbali wa kilometa 35 kutoka Uwanja wa Ndege, Mthatha hadi Qunu nyumbani kwa Mandela ambako mwili wake ulikabidhiwa kwa viongozi wa kimila.
Kama ilivyokuwa Pretoria, wananchi waliokuwa wamejipanga pembezoni mwa barabara walikuwa wakipunga mikono na wengine walisikika wakiangua vilio na kuomboleza.
Mapema jana asubuhi katika Uwanja wa Waterkloof, mwili wa Mandela uliagwa na viongozi waandamizi wa Chama Tawala cha Afrika Kusini, African National Congress (ANC) na ilipotimu saa 3:00 walikabidhi mwili huo kwa uongozi wa SANDF.
Kabla ya kupandishwa kwenye ndege, wimbo wa Taifa ulipigwa na gwaride la heshima lililokuwa limeandaliwa. Mamia ya wakazi wa Pretoria wakionekana wenye simanzi, walipunga mikono wakati ndege hiyo ikiondoka, na wengine walitokwa na machozi.
Ulinzi mkali
Uwanja wa Qunu ambao umekabidhiwa kwa SANDF hivi sasa, umetengwa kwa ajili ya wageni mashuhuri wakiwamo wakuu wa nchi na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa hivyo hakuna ndege za kiraia zinazoruhusiwa kuutumia.
Waziri wa Usafirishaji, Dipuo Peters alisisitiza kwamba ndege nyingine zitumie viwanja vya East London na Port Elizabeth ili kuondoa uwezekano wa kusababisha msongamano.
Mkuu wa Jimbo la Eastern Cape, Noxolo Kiviet alisema watu mashuhuri watakaotua Mthatha watachukuliwa katika mabasi maalumu, hivyo hakutakuwa na usafiri binafsi hata kwa wakuu wa nchi.
Ulinzi umeimarishwa katika eneo lote la Eastern Cape ambako askari polisi na wale wa SANDF walikuwa wakiendesha doria katika maeneo mbalimbali. Helikopta za jeshi na polisi pia zilikuwa zikizunguka eneo lote la Mthatha tangu juzi.
Msemaji wa Polisi, Kanali Mzukisi Fatyela alisema polisi na wanajeshi wamejiandaa kuhakikisha kuwa mambo yote yanakwenda sawa kwa maana ya usalama na mchakato wa mazishi.
Kanali Fatyela alisema baadhi ya barabara zimefungwa kwa sababu za kiusalama na kwamba askari watatoa maelekezo jinsi ya kutumia zile zilizopo kwa lengo la kuepusha msongamano.
Taratibu za kimila
Katika kutekeleza mila na desturi, jana asubuhi ng’ombe dume (fahali) alichinjwa na WaXosa wanaamini kwamba roho yake inasindikiza roho ya Mandela katika Ulimwengu wa mizimu. Ng’ombe huyo alichinjwa kabla ya mwili kuwasili.
Bila kuwekwa viungo vyovyote, nyama ya ng’ombe huyo ilichemshwa katika chungu cheusi cha chuma, kwenye moto ambao uliwashwa nje, hadharani.
Juzi mmoja wa viongozi wa kimila, Chifu Mfundo Mtirara alisema: “Baada ya mwili kuwasili, viongozi wetu wa mila watafanya matambiko na mwili huo utalala hapa ndani mpaka asubuhi”.
Mapema leo asubuhi, ng’ombe mwingine alitarajiwa kuchinjwa kabla ya taratibu za maziko kuanza kama sehemu ya taratibu za kimila za kusema buriani kwa Mandela.
Baada ya taratibu hizo, mwili unatarajajiwa kukabidhiwa kwa viongozi wa Kanisa na baada ya ibada ya kidini na baada ya taratibu hizo, utakabidhiwa kwa Rais Jacob Zuma kwa ajili ya mazishi ya kitaifa.
Mazishi hayo yatahitimishwa na taratibu nyingine za kimila zitakazoongozwa na Mfalme wa abaThembu, Buyelekhaya Dalindyebo anayetoka katika Ukoo wa Mandela.
Mfalme huyo ataongoza taratibu za kuukabidhi mwili wa Mandela katika Ulimwengu wa mizimu.
Wasaidizi wake wataungana naye katika tukio hilo na baada ya hapo, watatawanyika na kurejesa nyumbani ambako watanawa mikono kisha kupata chakula cha mchana.
Baada ya wiki moja, familia hiyo itakuwa na tambiko jingine la kusafisha beleshi (koleo) na vifaa vingine ambavyo vilitumika katika kuchimba kaburi atakamozikwa Mandela.
Baada ya mwaka mmoja, Desemba 15, 2014 ng’ombe dume mwingine anachinjwa kwa ajili ya hafla ya kuwavua wanafamilia mavazi ya maombolezo.
MWANANCHI