Polisi imewakamata wasichana wawili wa Kitanzania katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere Dar es Salaam, wakiwa na zaidi ya pipi 187 walizokuwa wamezimeza za madawa ya kulevya kwa ajili ya kusafirisha nchini China.
Aidha, polisi imemtia mbaroni, raia wa China Guoyn Shen (44), kwa kukutwa na madini aina ya quates kilo 19 aliyokuwa akiyasafirisha kwa njia ya ndege kuelekea China.
Wasichana waliokamatwa Jumatano ya wiki hii saa 11:00 jioni. uwanjani hapo walikuwa kwenye harakati za kupanda ndege ya kampuni ya ndege ya Qatar kuelekea China kupitia Hong Kong.
Kwa mujibu wa Mkuu wa kitengo cha kupambana na dawa za kulevya, nchini Kamanda Godfrey Nzoa, wasichana hao ni Mariam Makuhani (29) mkazi wa Tabata Kimanga na Khadija Shomari (30), mkazi wa Magomeni Mapipa ambao hadi jana asubuhi walikuwa wanaendelea kuzitoa pipi hizo kwa njia ya haja kubwa.
Alisema Mariam kwa wakati huo (saa 5:00) alikuwa ametoa pipi 65 wakati Khadija alifanikiwa kutoa pipi 122 ambazo zitapelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa ajili ya kubaini ni za aina gani na thamani yake.
ENDELEA KUSOMA HABARI HII KWA KUBOFYA HAPA CHINI
Alisema wasichana hao bado wapo chini ya uangalizi ambapo baada ya kumaliza zoezi hilo wataandaliwa mashitaka yao na kufikishwa mahakamani kujibu makosa yanayowakabili.
Kaimu wa Viwanja vya Ndege nchini, Mratibu wa polisi, Renatus Chalya, alisema awali baada ya wasichana hao kukamatwa, Mariam alikiri kumeza pipi 72 huku Khadija akidai alimsindikiza Mariam.
Akizungumzia changamoto za kupambana na madawa ya kulevya, Kamanda Nzoa alisema wasafirishaji wamekuwa wakiibuka na mbinu tofauti na wengine wakisafirisha viatilifu vya kutengenezea dawa hizo badala ya dawa zenyewe.
Alisema mbinu hizo zimekuwa zikifanywa kwa msimu na kutaja njia ambazo hutumiwa kuwa ni majini, viwanja vya ndege na nchi kavu.
Kufuatia changamoto hiyo, Tanzania na nchi nyingine duniani zilishiriki mikutano mbalimbali ambapo wa mwisho ulifanyika mwezi Oktoba mwaka huu nchini Afrika Kusini.
Alisema katika mkutano huo washiriki pamoja na mambo mengine walipata fursa ya kueleza changamoto wanazokabiliana nazo kwenye mapambano dhidi ya dawa hizo ambapo lililojitokeza ni usafirishaji wa viatilifu.
"Tuliliongelea kwa upana wake suala hili na kuafikiana kuwepo kwa sheria kali kwa kuwa tunayoitumia kwa mfano Tanzania haiwabani sana," alisema na kuongeza:
Alisema nchi zilizoshiriki mkutano huo zilibaini hiyo ni moja ya changamoto hivyo wakakubaliana kutungwe sheria itakayokuwa na makali zaidi.
Kamanda Nzoa aliwataja Watanzania wawili waliokamatwa kwa nyakati tofauti na viatilifu Agnes Masogange, Afrika Kusini na mwingine aliyemtaja kwa jina moja la Sada aliyekamatwa Tanzania ambao kutokana na sheria hiyo walilipa faini ndogo na kuachiwa huru.
Alisema sheria iliyopo inatoa nguvu kwa mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) ambapo mtu akikamatwa na viatilifu hivyo bila kibali atachukuliwa hatua za kisheria.
Kamanda Nzoa alisema kuanzia mwezi Machi hadi Julai mwaka huu, wamefanikiwa kukamata kilo 1482 ambazo tayari zilishaharibiwa.
Alisema dawa hizo zilikamatwa kwa nyakati tofauti kwenye meli ambapo moja ilikutwa na kilo 500, nyingine kilo 300.
"Ipo iliyokutwa na kilo 200 meli nyingine ilikutwa na kilo 182 ambapo hata hivyo kutokana na eneo walilokutwa walishindwa kuwafikisha mahakamani badala yake waliharibu mzigo huo," alisema.
Kwa upande wa njia ya anga, alisema kwa mwaka huu wamefanikiwa kukamata kilo 50 bila kuzijumlisha zinazoendelea kutolewa na wasichana hao wawili waliokamatwa Jumatano.
"Ipo kesi ambayo ukija hapa ofisi kwangu nitakuonyesha mlolongo mzima, huwezi amini tulikamata watu tena wakazitoa dawa hizo kwa njia ya haja kubwa lakini mahakama iliwaachilia, kama nilivyosema tunapoenda mahakamani tunatakiwa kuthibitisha pasipo kuacha shaka," alisema.
Kamanda Nzoa alisema kutokana na changamoto hizo, tayari wameshawapeleka vijana wao nchi mbalimbali na kutaja baadhi kuwa ni Afrika Kusini, Ghana, India, Iran, Ivory Cost kwa ajili ya mafunzo maalum.
Kuhusu Mchina aliyekamatwana madini alisema kuwa Shen alikamatwa Jumatano wiki hii uwanjani hapo akiwa kwenye harakati za kusafirisha mzigo huo kuelekea nchini humo.
Alisema mtuhumiwa huyo alikuwa akisafiri na ndege ya kampuni ya ndege ya Ethiopia iliyokuwa iondoke jioni ya siku hiyo.
Alisema mtuhumiwa huyo alipokamatwa alipotakiwa kutoa kibali cha kusafirisha mzigo huo hakuwa nacho na alipoulizwa ameyapata wapi alidai ameyanunua kwa wananchi.
Alitaja namba za hati ya kusafiria ya mtuhumiwa huyo kuwa ni 00609687.Alisema upelelezi wa tukio hilo unaendelea ikiwa ni pamoja na kubaini thamani ya madini hayo.
CHANZO: NIPASHE