Mwenyekiti wa Chadema,Freeman Mbowe akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana kuhusu Maamuzi ya Kamati Kuu ya Chama hicho ya kuwavua nyazifa Naibu Katibu Mkuu,Zitto Kabwe na Mjumbe wa Kamati Kuu Kitila Mkumbo Katikati ni Mwanasheria wa chama hicho,Tundu Lissu na Katibu Mkuu, Dk Willibrod Slaa. PICHA | FIDELIS FELIX
Dar es Salaam. Mgogoro ndani ya Chadema umezidi kupamba moto baada ya Kamati Kuu kuwavua uongozi Zitto Kabwe na Dk Kitila Mkumbo, huku Makamu Mwenyekiti Taifa, Said Arfi akiandika barua ya kujiuzulu.
Zitto alivuliwa uongozi wa Naibu Katibu Mkuu Taifa na Naibu Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, wakati Dk Mkumbo amevuliwa ujumbe wa Kamati Kuu. Wawili hao wanatuhumiwa kukisaliti chama.
Taarifa zilisema hoja ya kukisaliti chama pia ilimkumba Arfi akidaiwa kumwezesha Waziri Mkuu Mizengo Pinda kupita ubunge bila kupingwa, katika uchaguzi mkuu uliopita na ndiyo sababu ya kuamua kuachia ngazi nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Taifa.
Mbali ya kuwavua uongozi Zitto na Dk Mkumbo, pia Kamati Kuu imewapa siku 14 wajieleze kwa nini wasifukuzwe uanachama. Kwa uamuzi huo Zitto amebaki na wadhifa wa ubunge wake wa Kigoma Kaskazini na wadhifa mwingine kwenye Kamati ya Bunge.
ENDELEA KUSOMA HABARI HII KWA KUBOFYA HAPA CHINI
Zitto azungumza
Mara baada ya kumalizika kwa kikao hicho, Zitto aliliambia gazeti hili, “Sina cha kueleza, kikao kilikwenda vizuri na taarifa rasmi ya chama kuhusu uamuzi wa kikao itatolewa baadaye mchana (jana saa nane mchana), tusubiri Kamanda.”
Arfi ajiuzulu
Makamu Mwenyekiti wa Taifa, Said Arfi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mpanda Mjini, jana aliwasilisha barua ya kujiuzulu nafasi ya uongozi wa chama, akisema; “…kuchoshwa na unafiki unaoendelea ndani ya chama. Napenda ifahamike pia kwangu masilahi ya wapigakura, wakazi na wananchi wa Mpanda Mjini na Wilaya ya Mpanda ni muhimu katika kuwatumikia, hivyo basi sipo tayari kuchaguliwa marafiki.
Katika barua hiyo anasema amechochwa na tuhuma ambazo zimekuwa zikielekezwa kwake kuwa alimsadia Waziri Mkuu Mizengo Pinda kupita bila ya kupingwa katika uchaguzi wa ubunge katika uchaguzi mkuu uliopita.
“Kwa kipindi kirefu zimekuwepo shutuma dhidi yangu na kutiliwa shaka uhusiano wangu na Mhe Pinda Waziri Mkuu. Pamoja na kulijadili katika vikao kadhaa Mpanda na Dar es Salaam bado yapo mashaka kwa nini alipita bila kupingwa. Huo ulikuwa uamuzi wa Wanampanda kwenu imekuwa ni tatizo, lakini hamsemi kwa nini. Majimbo mengine 16 nchini yalipita bila kupingwa mlikuwa wapi na nani alaumiwe? Huu ni unafiki wa kupindukia.
Vilevile, katika barua hiyo, Arfi anasema amechukizwa na kauli ya mwasisi wa chama hicho, aliyemtaja kwa jina moja la Mtei kuwachagulia marafiki.
“Aidha mmechukizwa sana kwa nini nilihoji kauli ya Mwasisi wa chama, Mhe Mtei kutuchagulia viongozi. Naomba ifahamike wazi kwamba huu ni mtazamo wangu na utabakia hivyo siku zote kwa chama cha demokrasia kutoruhusu uongozi wa kiimla kwa kukidhi matakwa ya waasisi ambao huvigeuza vyama kuwa mali binafsi.
MWANANCHI
Kwa kusema ukweli na kusimamia ukweli daima itabakia kuwa lengo langu katika maisha yangu siku zote hata kama itanigharimu maisha yangu.”
Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbroad Slaa alipoulizwa kwa njia ya simu kuhusu barua ya Arfi ya kujiuzulu uongozi, alisema; “Mimi nimekwishaondoka ofisini.”
Taarifa ya chama
Akitangaza uamuzi wa Kamati Kuu jana Mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu alisema, Zitto, Dk Mkumbo na Mwenyekiti wa Chadema mkoani Arusha, Samson Mwigamba walikuwa na mtandao wa kukiua chama hicho, huku wakitengeneza tuhuma za kuwachafua Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe na Katibu wake, Dk Willbroad Slaa.
Alisema kuwa kamati kuu ilibaini kuwapo kwa mkakati mkubwa wa watu hao kutimiza malengo hayo ambao umeandikwa katika waraka unaoitwa ‘Mkakati wa Mabadiliko 2013’, ambao umeandaliwa na kikundi kinachojiita ‘Mtandao wa Ushindi’.
“Kikundi hicho vinara wake wapo wanne, Zitto anajulikana kama Mhusika Mkuu (MM), Mkumbo (M1), Mwigamba (M3) na mtu mwingine wa nne hatujamtambua kwa sasa yeye anatumia jina la M2” alisema Lissu.
Alisema wakati wa kuhojiwa na Kamati Kuu Dk Mkumbo alikiri kuwa mhusika mkuu wa mtandao huo ni Zitto, lakini Zitto alikana kuutambua waraka huo licha ya kueleza unamhusu kwa kuwa umetaja jina lake, kauli ambayo alidai Kamati Kuu haikutaka kuiamini.
Huku akieleza jinsi watu hao walivyokuwa wakiwasiliana na kupanga mikakati ya kuimaliza Chadema kwa siri chini ya ufadhili wa fedha kutoka kwa Zitto, Lissu alisema Naibu Katibu Mkuu huyo wa zamani alikuwa akitumiwa na Chama Tawala (CCM) kuimaliza Chadema.
“Mkakati wa Mabadiliko 2013 ni mpango haramu na ambao unaichanachana katiba ya chama chetu. Ni mkakati wa vita dhidi ya chama chetu na utaratibu wetu wa kikatiba. Hatuwezi kunyamazia mkakati huu wa kutumaliza, uvumilivu umefika kikomo,” alisema.
Uamuzi
Alisema kutokana na hali hiyo kamati kuu iliamuru wahusika wote wavuliwe nyadhifa zao zote za uongozi wa chama, kukubaliana kuunda timu ndogo ya pamoja ya watendaji wa sekretarieti ya makao makuu ya chama hicho ili kumtambua mtu wa nne (M2).
“Kamati ya Bunge imetakiwa kuchukua hatua za haraka kuhakikisha Zitto anavuliwa nafasi zote za Naibu Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, pia wote wanatakiwa kujieleza ndani ya siku 14 kwa nini wasivuliwe uanachama na watapewa fursa ya kujitetea,” alisema.
Alisema Kamati Kuu itakutana kwa dharura kwa ajili ya kufanya uamuzi juu ya hatima ya watuhumiwa hao.
Kauli ya Mbowe
Awali Mbowe alipinga madai kuwa Zitto ameondolewa kwa kuwa alikuwa akitaka kugombea nafasi ya uenyekiti wa chama hicho, akasisitiza kuwa uamuzi huo umefanyika kwa kuwa Chadema ni chama cha watu, siyo mali ya mtu binafsi.
Mvutano Zitto, Lema
Kwa zaidi ya wiki mbili Zitto amekuwa akilumbana na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema kuhusiana na masuala ya posho.
Vita hiyo ilianzishwa na Lema katika kikao cha wabunge wiki iliyopita aliposema kuwa Zitto anafanya unafiki kukataa posho.
Alimtuhumu mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini kwamba anakataa posho za vikao bungeni, lakini anapokea posho nyingi kutoka mashirika mbalimbali ya kijamii nchini.
Lema aliweka tuhuma hizo kwenye Mtandao wa Jamii Forum huku akisema suala hilo halihitaji vikao vya chama kulijadili isipokuwa vyombo vya habari na hususan, mitandao ya kijamii kwani hata Zitto hutumia mitandao hiyo.
Zitto alijibu kuwa tangu siku nyingi alikwishapiga marufuku kwenye Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kupokea posho kutoka taasisi au mashirika yanayosimamiwa na kamati hiyo.
Alisema tangu alipokuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), alipiga marufuku posho na pia aliwahi kuwashtaki Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) wabunge wanaochukua posho kutoka taasisi za Serikali.
Zitto pia alipata msukosuko mwingine baada ya kusambazwa ripoti inayoitwa ‘Taarifa ya Siri ya Chadema’ iliyomtuhumu kuwa alikuwa anashirikiana na CCM na viongozi wa Idara ya Usalama wa Taifa kuihujumu Chadema.
Pia, Zitto aliingia katika malumbano na chama chake baada ya kutuhumu vyama vya siasa kuwa hesabu zake hazikaguliwi na Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG), huku akitaka ruzuku kwenye vyama hivyo isimamishwe.
Chadema ilipinga vikali madai hayo na kueleza kuwa imekuwa inatumia taasisi binafsi kufanya kazi hiyo. Vyama vinavyopata ruzuku ya Serikali ni vile vyenye wabunge Chadema, CCM, UDP, TLP, CUF na NCCR-Mageuzi.
Mvutano kikaoni
Wakati wajumbe wa kikao hicho wakivutana, Zitto alikuwa njiani akirejea kutoka Sudan Kusini, ambapo alienda na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).
Taarifa kutoka ndani ya kikao hicho zinaeleza kuwa, baada ya kuibuka sintofahamu hiyo, Mbowe aliwapoza wajumbe wa kikao hicho, akiwaeleza kuwa haitakuwa busara kumjadili mtu ambaye hayupo.
“Mbowe alipendekeza kuwa ajenda hiyo iwekwe kando na itajadiliwa baadaye kutokana na Zitto kutokuwepo katika kikao hicho,” zilieleza habari hizo.
Baadaye Zitto alituma ujumbe ambao ulitangazwa kwa wajumbe wote, kwamba alikuwa njiani kurejea Tanzania, kwamba akifika moja kwa moja atakwenda katika kikao hicho.
Zitto awasili, mzozo waibuka
Kama vile alikuwa akisubiriwa yeye, mara baada ya kufika katika ukumbi huo saa 2:23 usiku huku akisindikizwa na walinzi wanne, mvutano mkali uliibuka katika ukumbi huo na mara kadhaa walinzi wa chama hicho, Red Brigade walionekana kukaa tayari mlangoni kuzuia vurugu kama ingetokea.
Gazeti hili lilikuwa nje ya ukumbi huo na mara kadhaa lilisikia sauti za malumbano za baadhi ya viongozi wa chama hicho, akiwamo Zitto, Mbowe na Lema.
Wakati wakitoa maelezo kwa nyakati tofauti Lema na Zitto walishutumiana huku kila mmoja akimtaja mwenzake kuwa anatumia vibaya nafasi yake na mitandao ya kijamii.
“Tatizo lake ni kutumia mitandao ya kijamii kueleza mambo ya chama wakati akijua siyo utaratibu, ugomvi wangu naye kwa kiasi kikubwa uko hapo,” alisikika akisema Lema.
Kuna wakati yaliibuka malumbano makali huku sauti za juu zikisikika kutoka ndani ya ukumbi huo, kati ya Zitto, Lema na Mbowe.
Taarifa kutoka ndani ya kikao hicho zinaeleza kuwa Dk Mkumbo alikumbwa na rungu hilo baada ya kubainika kuwa alikuwa ameanda taarifa za siri ambazo zilikutwa katika kompyuta mpakato (laptop) ya Mwigamba ambayo alinyang’anywa baada ya kudaiwa alikuwa anasambaza taarifa za kuhujumu chama hicho.
Kikao hicho kilimalizika saa 10:00 alfajiri huku maamuzi hayo yakifanywa siri na Mbowe alipoulizwa kuhusu kuwepo kwa taarifa za Zitto na Dk Mkumbo kuvuliwa uongozi,” alisema , “Taarifa zitatolewa baadaye mchana.”
Wasomi wazungumza
Akizungumza na gazeti hili jana, Profesa Gaudence Mpangala alisema Chadema ni chama kikubwa kinachoweza kushinda uchaguzi mkuu ujao hivyo kinapaswa kuwa na viongozi walioshikamana na kuwa na nia moja.
Aliongeza kuwa endapo wapo viongozi wanaoonekana kwenda kinyume na viongozi wenzao na kwenda kinyume na misimamo ya Chama, kinayo haki ya kufanya maamuzi ya namna yoyote yenye lengo la kukinusuru.
“Chadema ni chama kikubwa kinachoweza kushika dola…kinahitaji mshikamano mkubwa kwa viongozi wake na kuhakikisha hawatokei wasaliti….kama ni kweli waliosimamishwa ni wasaliti ni halali kabisa” anasema Profesa Mpangala.
Naye aliyekuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha SAUT, Dk Charles Kitima alisema wakati umefika kwa vyama vya siasa kutambua kuwa uwepo wa demokrasia ndani ya vyama vingi vya siasa nchini ni kusahihishana na kujisahihisha.
Dk Kitima alisema kuwa na mitazamo tofauti siyo usaliti ni demokrasia na kusema endapo mtu au kiongozi anafanya kitendo cha kuvunja katika ya nchi huyo moja kwa moja anakuwa mkosaji.
Mbunge wa Jimbo la Wawi (CUF), Hamad Rashid anasema matukio ya kufukuzana na kutuhumiana baina ya viongozi yanayofanywa na watendaji mkuu wa vyama vya upinzani yatasababisha upinzani uzidi kudidimia na kudumaa.
Alisema vyama vya siasa vimekuwa na usultani wa kuonekana kuwa vinapaswa kuongozwa na baadhi ya watu, na wengine wenye uwezo na mawazo mapya na yasiyopendwa na wakubwa anatafutiwa mbinu ya kuondoka.
Rashid alisema hali hiyo inasababishwa na kukosekana kwa mfumo mzuri wa uongozi ndani ya vyama vya siasa, ambapo anasema vyama haviongozwi kama taasisi na badala yake vinaongozwa kama mali za watu.
“Hili linalotokea Chadema sasa ni matokeo ya mfumo mbovu wa uongozi ndani ya vyama vya siasa nchini….vingi haviongozwi kama taasisi.” alisema.
MWANANCHI