Nelson Mandela (kulia) akiwa na Rais mstaafu wa Marekani, Bill Clinton alipotembelea kilichokuwa chumba chake katika jela ya Kisiwa cha Robben, Picha ya Mtandao.
Juni 12, 1964, Nelson Mandela alihukumiwa kifungo cha maisha jela baada ya kupatikana na hatia ya kufanya hujuma dhidi ya Serikali ya kibaguzi ya Makaburu.
Hata hivyo Mandela alitumikia kifungo hicho kwa miaka 27 na kutoka akiwa mtu aliyebadilika kitabia, akiwa mtulivu, akiwa na hekima, mwenye busara na mwenye kuheshimika katika jamii.
Mandela alianza kutumikia kifungo katika jela iliyopo kwenye kisiwa cha Robben kilichopo kwenye bahari ya Atlantic umbali wa kilometa 12 kutoka mji wa Cape Town, alimotumikia kifungo kwa miaka 18, na mwaka 1982 aliondolewa ndani ya kisiwa hicho na kuhamishiwa kwenye gereza pia lenye ulinzi mkali la Pollsmoor lililopo Cape Town na siku chache kabla ya kuachiwa huru alihamishiwa gereza lililopo mjini Cape Town la Victor Verster.
ENDELEA KUSOMA HABARI HII KWA KUBOFYA HAPA CHINI
Kisiwa cha Robben kwa takriban miaka 400 iliyopita kimekuwa kikitumika kama eneo la kuadhibu watu, kuweka watu katika maisha ya kuwatenga na kuwafunga jela. Ni kisiwa kwa ajili ya watu wasumbufu wa kisiasa, wasumbufu katika jamii na watu wasiotakiwa katika jamii.
Kama ilivyo kwa viongozi na wanaharakati wengine wa ukombozi wa kiafrika waliopata changamoto za Serikali za kikoloni kwa kukamatwa, ambao baadaye walikuja kushika uongozi wa nchi zao, kama vile Kwame Nkrumah wa Ghana, Jomo Kenyatta wa Kenya na Robert Mugabe wa Zimbabwe, Mandela naye alipotoka jela alikuwa Rais wa kwanza mweusi nchini Afrika Kusini.
Gereza la Kisiwa cha Robben, lililofahamika kwa jina la gereza ndani ya gereza, lilikuwa ni gereza lenye zahama na ukiwa. Kufungwa ndani ya gereza hilo maana yake ni muda mwingi kufanya kazi za suluba, lakini kulikuwa na fursa kwa mfungwa kupata muda wa kujisomea, kufanya mijadala na kujipima. Miongoni mwa masharti ya kushikilia maadili ndani ya gereza hilo ni kwa wafungwa kujikita kwenye kusoma na kufanya mijadala. Tabia ya Mandela na uongozi wenye weledi ni matokeo ya maisha ya jela au ‘Chuo Kikuu cha Kisiwa cha Robben.’
“Hakuna zaidi ya kuelekeza akili zako kwa kuwa mtulivu zaidi kwa kukubali ukweli wa jamii yako,” alisema Mandela. Mwanzoni mwa mwaka 1972, alipewa ofa ya kutoka jela kwa sharti la kutangaza kukomesha vurugu dhidi ya Serikali ya Makaburu, ofa mabayo aliikataa akisema kuwa Serikali ndiyo imekifanya chama cha ANC kutumia njia ya uanaharakati.
Maisha ya jela ndiyo yaliyombadili Mandela na kuwa kiongozi mwenye ushawishi, ambapo akiwa gerezani alijifunza kuhusu hisia za binadamu na namna ya kuondoa hofu na mambo yasiyo ya usalama kwa wengine. Akiwa gerezani Mandela aliwavutia askari magereza kwa namna alivyokuwa mtetezi wa haki, mweye heshima na mwenye uelewa wa masuala ya kisheria, ambapo ndani ya gereza la Kisiwa cha Robben alikuwa kiongozi wa wafungwa wenzake.
Kwa mujibu wa taarifa askari magereza walikuwa chini ya uongozi wa wafungwa na wafungwa walikuwa chini ya uongozi wa Mandela.
Mwandishi wa habari Eddie Koch aliandika kwenye magazeti ya Mail na Guardian kuwa selo namba saba alimokuwa akiishi Mandela, lilikuwa eneo lenye harakati nyingi za ulinzi mkali ndani ya gereza hilo kwa kila Jumamosi ya wiki.
Wakati Mandela akiwa ndani ya gereza hilo kulikuwa na mikwaruzano ya wafungwa, kutoka kitengo cha kijeshi cha ANC, chama cha Pan Africanist Congress na wanaharakati wa Steve Biko’s Black. Vurugu ndani ya gereza hilo zilifanyika kwa misingi ya kupingana watu binafsi na tofauti ya itikadi, ambapo vurugu hizo zilikuwa kipimo cha mbinu za uongozi wa kidiplomasia wa Mandela na wenzake.
Taarifa zilisema wafungwa wengi wapya walipelekwa kwenye gereza hilo la Kisiwa cha Robben, kama vile viongozi wa wanafunzi wa Soweto, wawakilishi wa baraza waliochochea vijana hadi wakaazisha vurugu nchini humo mwaka 1976, hawakuwa na ufahamu kuhusu hali ya kisiasa ndani ya gereza hilo.
Hivyo ilikuwa ni jukumu la Mandela na wenzake kuwaelimisha na kuwapa taratibu za gereza hilo wafungwa hao wapya vijana, gereza hilo lilikuwa sehemu huru kwa wasomi kutumia vipaji vyao. Gereza la Kisiwa la Robben lilijengwa kwa namna ambayo limezuia mawasiliano kati ya uongozi, askari au viongozi waandamizi wa harakati.
Wafungwa ambao ni viongozi waandamizi katika vyama vyao nje ya gereza, kila mmoja alifungwa kwenye selo yake iliyokuwa kwenye jengo B. Wahalifu sugu na wapiganaji wa msituni ambao lengo lao ni kuuondoa utawala wa makaburu waliwekwa kwenye jengo A ambalo limetengwa na majengo mengine.
Jengo G limejengwa kwa wafungwa wengi kuishi katika selo moja. Siku za nyuma wafungwa wenye asili ya Kihindi walikuwa wakitenganishwa na wafungwa wenye asili ya waafrika weusi.
Mandela siku zote alipopata fursa ya kuzungumza na askari magereza wa Afrikaner aliwataka kujielekeza kwenye mstari wa fikira za ANC. Hali hiyo ilimsaidia kujiimarisha kwa kuwa na mbinu mpya kila mara za kujenga hoja.
Hata hivyo, rafiki wa Mandela, Walter Sisuli ambaye walikuwa naye gerezani, alichukulia mazungumzo hayo kama mwanzo wa makubaliano na serikali ya kibaguzi.
Mandela pia akiwa gerezani alitumia muda huo kujiendeleza katika elimu ya sheria. Alibaini kuwa elimu hiyo inamsaidia kuweka msingi kwa makubaliano ya mwisho yasiyo ya kumwaga damu, kwa mslahi ya Afrika Kusini ijayo.
Insha na maandiko ambayo hayakuchapishwa aliyoyaandika akiwa gerezani yaliifanya Afrika Kusini iwe kama mshangiliaji, ilionyesha usomi zaidi na uasilia kuliko ule wa awali wakati wa mapambano na wakoloni. Alikuwa na matarajio ya kupata ukweli.
Mandela aliona jela kama vile maabara ya namna rangi tofauti zinaweza kuelewana na kuishi kwa utulivu. Aliona gereza kama mwakilishi wa jamii wa maelewano nchini Afrika Kusini ambayo yanaweza kudumishwa.
Hata hivyo, mkuu wa gereza Colonel Willie mwaka 1971 alizungumzia uwezo na utayari wa Mandela wa kuongoza serikali ya mpito nchini Afrika Kusini: “Mandela ana kariba ya kipekee. Amepata uzoefu wa mabadiliko ya kisiasa. Sidhani kama anasubiri kwa ajili ya kulipa kisasi. Sijaona chuki kwa yeyote miongoni mwao, lakini Mandela ana nafasi kubwa ya kuwashawishi.”
Alisema akiwa gerezani amekuwa akishirikiana na wazungu na wahindi ambapo walimuamini kwa asilimia kubwa, kwakuwa hakuwa anazungumzia kulipa kisasi kwa watu wa rangi nyingine.
Kilichompeleka jela
Mandela ambaye alikuwa kiongozi wa jumuia ya African National Congress (ANC), ambayo ilikuwa ikipinga ubaguzi wa rangi, mwaka 1956 alikamatwa kwa tuhuma za uhaini, lakini aliachiwa huru. Mwaka 1960 ANC ilipigwa marufuku na Serikali ya Makaburu.
Mwaka 1961, Mandela na viongozi wengine wa ANC waliunda jumuia nyingine iliyoitwa Umkhonto we Sizwe (MK), ambayo ilikuwa ni kitengo cha kijeshi cha ANC. Desemba 16, 1961, MK, ambayo Mandela alikuwa mkuu wake wa majeshi, kilifanya shambulio la bomu kwenye maeneo ya Serikali na walianzisha mapigano ya msituni. Mandela alikamatwa Agosti 5, 1962, na alihukumiwa kifungo cha miaka mitano jela kwa kuchochea wafanyakazi kugoma katika mgomo wa wafanyakazi uliotokea mwaka 1961.
Julai 1963 serikali ilishambulia shamba la Lilliesleaf lililokuwa Rivonia, ambalo lilikuwa likitumiwa na ANC kama maficho yao. Viongozi 19 wa ANC walikamatwa na kukutwa na nyaraka zilizoonyesha uhusiano wao na MK na mipango ya kufanya mashambulizi ikiwemo vita vya msituni.
Serikali ya makaburu iliwafungulia mashitaka viongozi 11 wa ANC, chini ya sheria ya uhalifu wa kufanya hujuma ya mwaka 1962. Wakati wa kesi Mandela hakutaka kuwa na shahidi na badala yake alielezea historia ndefu ya malengo ya ANC na MK, ambapo alikiri baadhi ya makosa lakini alijitetea kwa kosa la kutumia vurugu kudai haki. Na Julai 1964 alihukumiwa kifungo cha maisha jela. (NMG).
MWANANCHI