Afisa Mradi wa Elimu ya Afya na VVU/UKIMWI kutoka UNESCO, Bw. Herman Mathias akizungumza na washauri wa Vikundi vya Vijana wasikilizaji juu ya masuala muhimu kuhusiana na kuzuia maambukizi ya VVU na Afya ya Uzazi kwa Vijana wenye umri kati ya miaka 15-24 katika warsha ya kuwajengea uwezo washiriki hao katika matumizi ya mwongozo wa ufuatiliaji wa vipindi kwa wasikilizaji walengwa wa Mradi wa SHUGA Redio inayofanyika kwenye kituo cha Redio Nuru FM mjini Iringa.(Picha zote na Zainul Mzige wa MOblog).
Mkufunzi wa warsha hiyo Meneja Mawasiliano kutoka Pangani FM, Bw. Abdullah Mfuruki akiwapiga msasa washauri wa Vikundi vya Vijana kwenye warsha ya siku mbili inayoendelea mjini Iringa.
ENDELEA KUSOMA HABARI HII KWA KUBOFYA HAPA CHINI
Na Mwandishi wetu
Tafiti zimebaini kwamba Vijana hawatumii Kondomu na hutoa sababu nyingi ikiwa ni pamoja na kutopata ladha wakati wa tendo la ndoa na kwamba inapunguza nguvu na visingizio vingine vingi vinavyopelekea kuashiria hatari ya maambukizi.
Hayo yameelezwa na Afisa Mradi wa Elimu ya Afya na VVU/UKIMWI kutoka UNESCO, Bw. Herman Mathias wakati akizungumza na washauri wa Vikundi vya Vijana wasikilizaji juu ya masuala muhimu kuhusiana na kuzuia maambukizi ya VVU na Afya ya Uzazi kwa Vijana wenye umri kati ya miaka 15-24 katika warsha ya kuwajengea uwezo washiriki hao katika matumizi ya mwongozo wa ufuatiliaji wa vipindi kwa wasikilizaji walengwa wa Mradi wa SHUGA Redio.
“Asilimia 40 ya Wasichana na Asilimia 47 ya Wavulana ndio wenye ufahamu wa kina juu ya maambukizi ya VVU huku asilimia kubwa wakiwa hawana elimu ya kutosha na hawajui afya zao kwa kuwa hawana utamaduni wa kupima VVU ”, amesema Bw. Mathias.
Katika warsha hiyo ya siku mbili inayoendeshwa na UNESCO kwa kushirikiana na UNICEF katika kituo cha Redio cha Nuru FM Iringa, Bw. Mathias amesema kuna umuhimu mkubwa wa kutoa elimu sahihi kwa Vijana ya kujikinga na maambukizi ya VVU na Mimba kutokana na uelewa mdogo wa Vijana katika matumizi sahihi ya Kondomu.
Wakichangia mada kuhusu masuala muhimu yanayowahusu vijana katika maambukizi ya VVU vijana wamesikitishwa na mimba za utotoni kwa wasichana zinazochangia vifo vya Mama na Watoto na wasichana kuacha masomo.
Washiriki wa warsha hiyo wametaka hatua za haraka zichukuliwe kuhakikisha kuwa sheria za mtoto zinazoruhusu mtoto wa kike kuolewa katika umri mdogo zinafanyiwa marekebisho ya haraka kulinda haki ya mtoto wa kike.
Mmoja wa washiriki akihoji jambo kwa mkufunzi wakati wa mafunzo hayo.
Wakijadili mada hiyo washiriki wamesema mila na tamaduni pia zinachangia kwa kiasi kikubwa kumkandamiza mtoto wa kike katika masuala mbalimbali ya maendeleo yake.
Wakitoa mifano ya baadhi ya mila zilizowafanya wapaze sauti kuhusu mabadiliko ya sheria za mtoto ni ile sheria ya ndoa na mila inayoruhusu mtoto wa kike kuolewa akiwa na umri wa miaka 14 kwa ridhaa ya wazazi. Umri huo unakinzana na haki za mtoto kufurahia maisha yake na kupata elimu.
Mifano mingine ya kitamaduni ni pale mwanamume anapochumbia mimba wakati akijua wazi mtoto ana haki zake za msingi za kuishi.
Wamezitaja pia asasi za dini kutoa elimu kwa vijana ili kusaidia hali iliyojitokeza ya wazazi kutokuwa na muda na watoto wao kuwaelimisha kuhusu mabadiliko ya miili na afya zao.
Afisa Mradi wa Elimu ya Afya na VVU/UKIMWI kutoka UNESCO, Bw. Herman Mathias akifafanua jambo kwa washiriki.
Akitoa mada kuhusu mbinu mbalimbali za kuwezesha majadiliano katika vikundi vya wasikilizaji, Meneja Mawasiliano kutoka Pangani FM, Bw. Abdul Mfuruki amewataka wawezeshaji kutotumia nafasi walizonazo ili kuendesha mjadala wenye tija.
Amesema washauri wa vikundi hawana budi kuweka mizania kutumia busara, kusoma mazingira na kutoingiza imani au itikadi itakayopelekea kuharibu mjadala unaoendeshwa wa kufuatilia vipindi vya SHUGA Redio, kuwa wavumilivu, kusoma na kuheshimu mawazo ya wengine na kutofungamana na upande wowote ili kumweleza mshiriki wa majadiliano kufunguka zaidi.
Bw. Mfuruki amesema vijana wa vikundi vya wasikilizaji kuwaza mambo mengi ni vyema kuwasikiliza kwa uvumilivu, kupata ushauri wa wengi kwa lengo la kufanya maamuzi sahihi bila kulazimishana na vile vile kuwa wabunifu kwa kutumia mbinu mbadala ili kupata habari iliyojificha.
Mkufunzi Meneja Mawasiliano kutoka Pangani FM, Bw. Abdullah Mfuruki akiwaelekeza jambo washiriki wakati wa mazoezi ya vikundi kazi kwenye warsha hiyo.
Pichani juu na chini ni baadhi washauri wa vikundi vya vijana wakifuatilia kwa umakini warsha hiyo kwa ajili ya kutekeleza Mradi mpya wa SHUGA Redio wenye lengo la kuendeleza kampeni za hamasa kwa vijana kupunguza maambukizi mapya ya VVU kupitia Redio za Jamii nchini.
Pichani juu na chini ni Washiriki wakijidiliana kwenye vikundi kazi wakati wa warsha hiyo.
Mkufunzi wa warsha hiyo Meneja Mawasiliano kutoka Pangani FM, Bw. Abdullah Mfuruki akitoa mwongozo wa kazi za vikundi kwa staili ya aina yake kwa washiriki wa warsha ya siku mbili katika utekelezaji wa Mradi mpya wa SHUGA Redio.
Pichani juu na chini washiriki akitolea maelezo ya picha aliyoichora ikimaanisha nini wakati wa warsha hiyo ya siku mbili inayoendelea mjini Iringa.