WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda, amesema analipwa mshahara wa Sh milioni 6 kwa mwezi. Waziri Mkuu Pinda alitoa taarifa hiyo bungeni jana, alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Mkanyageni, Mohamed Habib Mnyaa (CUF), wakati wa maswali ya papo kwa papo ambayo huulizwa kila Alhamisi.
Katika swali lake, Mnyaa aliinukuu Ibara ya 43 ya Katiba ya Tanzania inayoeleza namna Rais wa nchi, atakavyolipwa mshahara wake pamoja na posho nyingine pindi anapokuwa madarakani na anapostaafu.
Kwa mujibu wa Mnyaa, kifungu hicho kinalitaka Bunge lipitishe maslahi hayo na hivyo akataka kujua ni lini Bunge lilikaa na kupitisha mshahara wa Rais, Waziri Mkuu na Makamu wa Rais.
Akijibu swali hilo, Waziri Mkuu alisema hakumbuki ni lini Bunge lilijadili na kupitisha mafao ya viongozi hao wakuu wa nchi.
“Siwezi kulijibu hili moja kwa moja, kwa sababu sijawahi kuona mishahara ya viongozi hao ikijadiliwa hapa bungeni. Lakini ninachojua unapokuwa na kifungu kama hicho, lazima itakuwapo sheria inayosimamia hili, lakini kwetu sisi menejimenti ya utumishi wa umma ndiyo inayotusimamia.
“Lakini, pia hivi karibuni niliona mheshimiwa Kabwe (Zitto Kabwe, Mbunge wa Kigoma Kaskazini), akiwa kule Mpanda na kusema mshahara wangu ni Sh milioni 30.
ENDELEA KUSOMA HABARI HII KWA KUBOFYA HAPA CHINI
“Mtu huyo alisema uongo, usahihi wa hili ni kwamba, mshahara wangu kwa mwezi ni Sh milioni 6 na hizi zinaunganishwa na posho za mke wangu.
“Sasa unaposikia mtu anasema nalipwa Sh milioni 30 hujui ana maana gani, huyu alisema uongo na naomba Mungu amsamehe. Siwezi kumsemea Makamu wa Rais na Rais, lakini hata tofauti ya mshahara wangu na ule wa Makamu wa Rais pamoja na ule wa Rais, ni kama shilingi milioni moja.
“Pamoja na mshahara huo, tunachopewa kingine ni nyumba ambayo hatulipii pamoja na chakula… nadhani haya yaliwekwa ili kutuondolea mawazo pindi tunapokuwa kazini.
“Pia nalipwa posho ya Sh 500,000 kwa nafasi yangu ya Waziri Mkuu pindi ninapokuwa bungeni,” alisema Waziri Mkuu.
Pamoja na hayo, Waziri Mkuu alisema yeye ni kati ya watu wanaopenda kukopa fedha benki na kwamba amekuwa akifanya hivyo kupitia Benki za NMB na CRDB.
Alisema baada ya Serikali kuruhusu utaratibu wa kukopa sehemu ya kiinua mgongo, yeye ameshakopa asilimia 50 ya kiinua mgongo chake.
ZITTO
Pinda ametangaza mshahara huo, baada ya aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Zitto Kabwe kudai analipwa Sh milioni 26 kwa mwezi bila kukatwa kodi.
Alisema hoja ya msingi si kiasi wanacholipwa viongozi hao walioajiriwa na wananchi, bali ni usiri unaofanywa juu ya kiwango hicho.
Alisema Katiba ya sasa Ibara ya 43(1), inaeleza kuwa Rais atalipwa mshahara na malipo mengine huku ibara hiyo hiyo kifungu cha pili, ikizuia mshahara na marupurupu kupunguzwa, hali aliyoelezea kuwa ni muhimu Katiba Mpya ikabadilisha sheria hizo kwa manufaa ya nchi.
RAI